Ushirikiano wa filamu za Tanzania na Korea ulivyowaibua waigizaji

Ushirikiano wa filamu za Tanzania na Korea ulivyowaibua waigizaji

Ikiwa zimepita saa chache tangu mchekeshaji Steve Nyerere kutoa taarifa juu ya Tanzania kuchaguliwa kuwa nchi ya kwanza kufanya filamu na South Korea baadhi ya waigizaji nchini wameonesha kufurahishwa na jambo hilo.

Akizungumza na Mwananchi mwigizaji Steven Charles 'Dr. Alsmasi' amesema jambo hilo ni zuri endapo uwekezaji utafanyika.

“Kwa upande wangu ni jambo zuri na serikali inaweza kupata pato kubwa endapo uwekezaji huu utafanyika, pili itatupatia wasanii fursa ya kufanya kolabo na wasanii wa Korea Kusini ambao kwa sasa wanafanya vizuri sana katika soko lao la filamu” amesema Dr. Almasi

Hata hivyo aliongezea kuwa jambo hilo litafanya wasanii wa Tanzania watambulike pamoja na kukuza lugha ya kiswahili.

Kwa upande wake mwigizaji Eddie Ngwasuma aliyewahi kuonekana kwenye filamu ya ‘Chini ya Kapeti’, ‘La Familia’, ‘Karma’ na nyinginezo amesema jambo hilo linaongeza mwamko kwa Watanzania.

“Kwanza kabisa hii nafasi inatupa Watanzania elimu, msisimuko, mwamko wa kuweza kuboresha kazi zetu, hapo mwanzoni labda pengine producer walikuwa wanatengeneza kazi wakiamini kwamba ni kazi ambazo zinatizamwa na Watazania tu, lakini kupitia hii kutatanua tasnia ya filamu kuipeleka mbele zaidi,"amesema.

Naye mwigizaji Idriss Kassian ambaye anaonekana katika tamthiliya ya ‘Juakali’ akitambulika kwa jila la Zakayo ameonesha kufurahishwa na jambo hilo.

“Ni jambo la kheri ni muda wa tasnia ya filamu kufika mbali zaidi duniani kote, kwani soko letu la filamu halijawahi kufanya vizuri sana duniani na siyo duniani tu hata Afrika hivyo naamini jambo hili endapo likatokea basi litatusogeza mbali sana.”

Mbali huyo, mwigizaji mkongwe Hidaya Njaidi amepongeza suala hilo huku akiwataka wasanii na waongozaji filamu kuongeza umakini katika kazi zao.

“Kwanza inatia moyo, inatia nguvu inatufanya tufanye kazi kwa weledi na kwa umakini wa hali ya juu kwa sababu tumeshafika viwango vya kimataifa na suala hilo mimi naliona kwa upande wangu ni suala zuri sana endapo litafanikiwa," amesema Hidaya.

Kwa upande wa mwigizaji Rose Patrick ‘Clara Nampunju’ ambaye kwa sasa anatamba na tamthiliya ya ‘Nuru’ akitumia jina la 'Sikudhani' ameeleza kuwa jambo hili endapo litatimia waigizaji wa filamu watakuwa wamejipata.

“Mimi kwangu naona tumepata bahati kubwa sana niseme tu wasanii wa filamu ni kama tumeshajipa kwa sababu tutaenda kujifunza vingi pia kutangaza kiswahili kwa ukubwa zaidi” amesema Clara

Utakumbuka kuwa mwigizaji Steve Nyerere kupitia ukurasa wake wa Instagram alidai kuwa Rais wa Filamu Korea Kusini Yang Jongkon, wakati akifanya mazungumzo nao alisema Tanzania imechaguliwa kuwa nchi ya kwanza Afrika kufanya filamu na Korea ya Kusikazini kwa ajili ya kuunganisha soko la filamu la Tanzania na nchi hiyo.


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post