Uoga wa uzee watajwa sababu mastaa Bongo kudanganya umri

Uoga wa uzee watajwa sababu mastaa Bongo kudanganya umri

Kutokana na tabia ya baadhi ya wasanii kudanganya umri na kutaja mdogo zaidi uoga wa uzee na ubaguzi unataja kuwa chanzo cha kufanya hivyo.

Akizungumza na Mwananchi Scoop mwanamuziki wa Bongo Fleva Benard Paul Mnyang’anga maarufu kama ‘Ben Pol’ amesema mastaa wengi anashindwa kujiamini ndiyo maana wanadanganya.

“Shida kubwa ni kutojiamini na kutojikubali, na hiyo inatoka mbali kwenye malezi, mtu alikuwa anaambiwa hajui chochote, unaambiwa maneno ya kukatishwa tamaa wewe siyo mzuri, siyo mrembo hujui kuigiza, hujui kucheza, huna akili kwa hiyo katika kuambiwa hayo yote inapelekea kumuua mtu ujasiri.

"Hivyo muda wote unajiona unakosea ndipo unaamua kuficha vitu vyako unaanza kudanganya umri, lakini pia kinachofanya wadanganye umri ni kuwa na wasiwasi kwamba hajafanya vitu vingi, hajatimiza malengo ukilinganisha na umri wake mtu anafikiria ana miaka 43 hajajenga, hajanunua gari kwa hiyo anaona adanganye tuu umri,” amesema Ben Pol

Aidha aliongezea kuwa si vyema mastaa kutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii kwani ndiyo chanzo cha kudanganya kutokana na kujilinganisha na watu wengine.
Kwa upande wa mwigizaji, Heleina Herman ‘Love Juakali’ amesema umri ni kitu binafsi hivyo siyo lazima kila mtu ajue.

“Kwanza umri ni kitu binafsi siyo kila mtu ajue umri wako, kwa sababu kuna mwingine anakuuliza una miaka mingapi unamwambia 30 anakwambia mbona huonekana kama unamiaka hiyo na ndiyo maana waigizaji wengi hatupendi kutaja umri tulionao.

"Tukisema umri wetu wa kweli watu hawaamini. Sawa ni msanii kioo cha jamii lakini hayo ni maisha yake binafsi mimi sidhani kama kuna ulazima wa mashabiki kujia umri. Mimi binafsi sipendi watu wajue umri wangu japo 'am still children',” amesema Love Juakali
Naye mwanamuziki chipukizi Hadatha amesema wasanii wengi wanadanganya umri kwa sababu hawapendi kuzeeka.

“Nadhani wanadanganya miaka kwa sababu watu wengi hawapendi kuzeeka, ukiachana na wasanii hata watu wengine pia hawapendi watu wajue kuwa wamezeeka kwa hiyo nafikiri wasanii nao wanadanganya ili jamii iwatambue kama bado wana umri mdogo kwa sababu imani za wanajamii wanatamani kumuona msanii wao wakiwa na umri mdogo na muonekano mzuri,"amesema

Hata hivyo mwanasaikolojia Saldeen Kimangale amesema mastaa wengi wanadanganya umri kwa sababu ya changamoto zitokanazo na shinikizo la jamiii.

“Watu maarufu, katika tasnia ya burudani, mara nyingi huficha umri wao halisi kutokana na changamoto zitokanazo na shinikizo la kijamii, ingawa suala la kutojikubali huwezi kulipuuza. Katika sekta ya uigizaji wa filamu kwa mfano, mara nyingi vijana wanapewa kipaumbele hivyo baadhi yao huficha umri ili kuepuka ubaguzi wa umri.

“Hii pia huwasaidia kudumisha mvuto kwa mashabiki wa rika zote, bila kuzingatiwa umri wao. Kwa kuwa taswira yao ni muhimu kwa umaarufu wao, kuficha umri huwasaidia wasanii maarufu kuepuka kuwekwa kwenye majukumu yanayohusishwa na umri fulani, kama vile kupitwa na wakati,” amesema Kimangale

Hata hivyo amesema hakuna shida kisaikolojia kwani baadhi yao wanaamua kufanya hivyo kutokana na kuficha faragha zao ili wasisumbuliwe.
Mbali na hayo mwanamuziki Lina Sanga kupitia ukurasa wake wa Insta ameonekana kuwatolea uvivu baadhi ya watu wanaojadili kuhusu umri wake.

“Nashangazwa sana na watu wanavyoshambilia wenzao kuhusu kuzeeka dah!, tena mtu anacheka kabisa ‘umezeeka’ swali ni kwamba kwani wenzetu nyinyi mpo pale pale? Umri hausogei? au mlishushwa tu hamjazaliwa? Yaani mtu baada umshukuru Mungu unaishi miaka mingi unaanza kutia kasoro duh!, am very happy na 34 yangu kikubwa pumzi jamani,” ameandika Linah






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post