Umuhimu wa mkataba kazini

Umuhimu wa mkataba kazini

Niaje niaje wanangu sana, I hope mko guudi kabisa, leo sitowachukulia muda wenu kwa sababu najua wengi wenu mtakuwa mmefunga so manahitaji kupewa vitu laini laini, Leo kwenye kazi niko na mada muhimu ambayo itakusaidia pindi mambo yatakapoenda kombo ukiwa kazini.

Kama tunavyojua kila siku watu wanamaliza vyuo na kila siku watu wapo kiguu na njia kutafuta ajira kwenye kampuni tofauti tofauti, Mwananchi Scoop katika kulitambua hilo, leo upande wa kazi tumekusogezea umuhimu wa mikataba ya ajira sehemu ambayo utabahatika kupata kazi.

Tambua kuwa sheria ya kazi ya Tanzania inahitaji wafanyakazi wapewe mikataba isipokuwa kwa wale ambao wanafanya kazi chini ya siku 6 kwa mwezi.

Katika mkataba utakaopewa lazima ueleze maelezo yafuatayo, Jina, umri, anwani ya kudumu, jinsia ya mfanyakazi, mahali pakuajiriwa, ufafanuzi wa kazi, tarehe ya kuanza, aina na muda wa mkataba, mahali pa kazi, saa za kufanya kazi, ujira (maokoto/mshahara), pamoja na maelezo ya malipo yote.

Mkataba ni muhimu kwa muajiri na muajiriwa, kwa sababu husaidia pande zote mbili kupata wanachotaka nikimaanisha muajiri kuhakikisha shughuli zake zinaenda vizuri na maendeleo katika kampuni/ofisi yake yanaonekana.
Kwa upande wa muajiriwa, anafurahi kufanya kazi katika kampuni au ofisi ya muajiri bila adha yoyote kwa mfano kucheleweshewa mshahara, mazingira mabovu kazini.

Aidha ni muhimu kuwa na mikataba ya maandishi kuliko kufanya mikataba ya maneno kwani inakuwa rahisi kufanya maamuzi kwa muajiri na muajiriwa kutokana na uwepo wa nyaraka zinazoweza kuwa na miongozo sahihi.

Muajiri na muajiriwa wakiandikishiana mkataba kwa njia ya maandishi inakuwa rahisi kwa pande zote mbili kufanya kazi vizuri na kukidhi matakwa na malengo ya kampuni ikiwa ni pamoja na muajiri kujua majukumu yake na muajiriwa pia kutekeleza majukumu yake ili hali akitambua changamoto atakazoweza kuzipata kama hatotimiza majukumu yake kama ilivyoandikwa katika mkataba.

Pia kupitia mikataba, siri za kampuni au ofisi huwa ni vigumu kutoka nje ya ofisi na kuwafikia washindani katika tasnia husika, na hii ni kwa pande zote mbili muajiriwa na muajiri. Ikitokea mmoja kati yao amekiuka hilo, basi muajiri au muajiriwa huruhusiwa kuchukua hatua za kisheria.

Kuhusu mapumziko au likizo, ruhusa na mambo yanayoendana na hayo muajiri na muajiriwa huwekeana maelezo katika mkataba ili kuepusha sababu zisizokuwa na msingi zinazoweza kutokea mara kwa mara hasa katika upande wa muajiriwa.

Kwa mfano, ikitokea muajiri na muajiriwa wamesaini mkataba inakuwa rahisi kwa muajiri kujua haki za mtu aliyemuajiri na nini kifanyike iwapo mfanyakazi wake anaomba sana ruhusa na kiasi gani inaleta shida kwa ofisi.

Ni muhimu kwa muajiri kumkumbusha mfanyakazi mara kwa mara mambo ya kuzingatia hususani yaliyopo katika mkataba ili kuepukana na hatua mbadala ambazo zinaweza kuumiza pande zote mbili.

Aidha, mfanyakazi anashauriwa kusoma kwa makini mkataba kabla hajausaini ili kuepuka shida yoyote huko mbele kama atahitajika kufanya mambo ambayo yapo nje ya uwezo wake. Lengo la mkataba siku zote huwa ni kuhakikisha pande zote mbili, zinakubaliana na zinafurahia kufanya kazi pamoja na si vinginevyo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags