TBT za mastaa ni hamasa kwa mashabiki

TBT za mastaa ni hamasa kwa mashabiki

Kila ifikapo siku ya Alhamisi watu hupamba mitandao ya kijamii kwa picha na video za matukio yaliyopita. Matukio hayo hugusa sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye michezo, familia na hata upande wa burudani ya muziki na filamu.

Katika upande wa sanaa siku hiyo ndiyo picha na video nyingi za wasanii huchapishwa kwenye kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii. Uchapishwaji huo huenda sambamba na dhamira mbalimbali.

Wapo wanaoamini kuwa kufanya hivyo ni kukumbusha matukio muhimu ambayo yaliwahi kutokea huku wengine wakichukulia kama vituko ama vichekesho wanapoona TBT za wasanii mbalimbali hasa kutokana na mionekano yao ya kipindi hicho.

Kutokana na mawazo mseto juu ya uchapishwaji wa matukio hayo ya zamani yanayohusu watu maarufu nchini. Mwanamuziki mkongwe Precious Nkoma maarufu kama Domokaya amesema TBT ni kumbukumbu inayoleta funzo katika jamii kupitia wasanii.

“Unajua sasa hivi dunia ipo kiganjani kila kitu kinakuwa wazi, kupitia hilo jamii inahitaji kupata mafunzo mbalimbali kupitia kwa wasanii au wanahabari, sasa TBT ni kumbukumbu inayotoa funzo kwa maana watu wanapoona mimi nilipoanzia na nilipo sasa inakuwa inampa moyo na inamtia nguvu ya kupambambania kile anachokiamini,” amesema Domokaya.

Aidha mwanamuziki Nedy Music amesema kwa sasa TBT imekuwa kama fasheni kwa wasanii na ni moja ya kuweka kumbukumbu zao.

“Wasanii wangi wamekuwa wakiweka TBT kwa lengo la kumbukumbu za maisha yao yaweza kuwa kabla ya kuingia katika sanaa na baada ya kuingia katika sanaa lakini wakati anajitafuta na ni jambo zuri,” amesema.

Hata hivyo mdau wa muziki Athumani Palla, maarufu kama Palla Midundo ameeleza kuwa ni jambo zuri na ukuaji wa wasanii kushiriki kumbukizi zao na mashabiki.

“Kuweka TBT ni kuonesha ukuaji ambao msanii fulani anaonesha historia yake ya mwanzo kulinganisha na sasa japo siku hizi mtu aki-post picha yake ama video za zamani anaonekana kama mshamba au kituko katika jamii,” amesema na kuongeza.

“Kila kitu kina mapito yake, hivyo siyo kitu kibaya wasanii kuonesha historia zao za zamani kwa sababu inaweza kwa kuhamasisha katika jamii hata watu waliokata tamaa katika utafutaji kupambana na kuona kila kitu kinawezekana.”

Pia mwigizaji John Elisha anayetamba katika Tamthilia ya Connection, amesema TBT inahamasisha watu kuwa kila kitu kinawezekana.

“TBT inahamasisha jamii kuwa kila kitu kinawezekana kwa sababu kwenye hiyo TBT kuna mambo mawili kuwa na mabadiliko ya kiuchumi au mabadiliko ya kimwili ambayo yanamuonesha msanii alivyokuwa mwanzo na sasa, mfano mafanikio aliyokuwa nayo leo tofauti na mwanzoni,” amesema Elisha.

Naye rapa Rashid Rais 'Maarifa Big Thinker' ambaye amekuwa akirudia ngoma za wasanii wa zamani na kuzichapisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii kila ifikapo Alhamisi, amesema TBT inawekwa kwa ajili ya kukumbushana matukio.

“TBT ipo na itaendelea kuwepo kwa ajili ya kukumbusha matukio au historia fulani ya mwanamuziki huwenda ikawa kabla ya muziki alishawahi kukutana na changamoto fulani au muziki wake wa zamani ulikuwaje ukilinganisha na sasa,” amesema Maarifa.

Kwa upande wa Sara Njiku, mfanyabiashara wa vifaa vya Electronic amesema TBT za wasanii zinatia moyo.

“Mimi huwa napenda sana zile TBT za wasanii kwa sababu zinatia moyo watu kuchakarika katika maisha ya kila siku, mfano leo hii tunamuona Diamond anavyoruka kimataifa wakati mwanzo hakuna hata aliyetamani kujua alikuwa na nani lakini kupitia picha yake ya zamani mtu anavyoiona mtandaoni kwanza anashangaa na kujiaminisha kila kitu kinawezekana na ni suala la muda,” amesema Sara.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags