Na Aisha Charles
Naam! watu wangu kwa mara nyingine tena katika burudani tumekutana kupashana habari zinazobamba kwenye upande huu, leo tutamzungumzia mchezaji wa mpira wa kikapu Stephen Curry, mafanikio yake na anavyoendelea kupata fursa kupitia mchezo huo.
Miaka miwili mfululizo mchezaji wa mpira wa kikapu wa NBA kutoka nchini Marekani Stephen Curry anayeichezea ‘timu’ ya Golden State Worriors ameingia kwenye ‘rekodi’ ya kuwa mchezaji aliyepata pesa nyingi zaidi kupitia mshahara wake.
Mwaka 2022, alizidiwa kidogo na Kevin Durant ambaye ndiye alipata pesa nyingi kutokana na ‘madili’ ya nje ya uwanja. Lakini mwaka 2023 hadi mwaka huu 2024 Curry amesimama tena kileleni kwa kupata maokoto mengi zaidi kupitia mikataba ya matangazo mbalimbali anayopata.
Anapigaje pesa?
Bado ameendelea kuwepo kwenye 10 bora ya wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani, mwaka 2023 alishika nafasi ya nane akiwa amepata jumla ya dola 103 milioni, ambapo dola 51 milioni alizipata kwenye mshahara wake ambao ndiyo mshahara mkubwa zaidi kuwahi kulipwa kwa mchezaji wa NBA huku dola 52 milioni akizipata kwenye madili mengine ya nje ya uwanja.
Kwa sasa ‘amesaini’ mkataba mpya na team ya Golden state ambao utamuwezesha kupata dola 215 milioni ndani ya miaka minne ambapo kwa miaka mitatu ya kwanza alipata dola 48 milioni, msimu wa mwaka 2023-24 amepata dola 51.9 miloni, msimu huu wa mwaka 2024 -25 atapata dola 55.7 milioni.
Kwenye sekta ya mikataba mingine minono nje ya kikapu mchezaji huyo ni balozi wa Under Armour tangu mwaka 2013 na mwaka 2017 alirefusha mkataba nao ambao hadi sasa unampa zaidi ya dola 10 milioni kila mwaka.
Mwaka 2015 pia alisaini mkataba wa ubalozi na kampuni iitwayo Brita, pia anaubalozi wa kampuni za Unilever Degree, JPMorgan Chase, Palm, CarMax, Callaway Golf, 2K Sports, na Rakuten zote hizi zinampa zaidi ya dola 30 milioni kila mwaka.
Ukiachana na madili hayo ya ubalozi fundi huyu wa mpira wa kikapu pia anatumia pesa zake kuwekeza na kununua hisa kwenye makampuni mbalimbali amekuwa akipata faida ya zaidi ya dola 5 milioni kwa mwaka.
Nyumba anazomiliki
Anamiliki mjengo unaokadiriwa kuwa na thamani ya dola 50 milioni uliopo Malibu, California, tangu April 2021.
Nyumba hiyo ya kifahari ndani yake kuna bwawa kubwa la kuogelea, ukumbi wa sinema na sehemu ya kuchezea kikapu.
Pia ana nyumba nyingine inayopatikana Atherton, Menlo Park, California ambayo aliripotiwa kuwa yuko mbioni kuiuza.
Pia nyumba yake nyingine yenye thamani kubwa ni ile ya San Francisco aliyoinunua kwa dola 8 milioni.
Magari anayo miliki
Mercedes-Benz G55- dola 156,450.
Tesla Model X 90D- dola 93,500
Infiniti Q50- dola 42,100
Porsche 911 GT3 RS- dola 416,500
Kia Sorento- dola 39,190
Range Rover Sport LWB - dola 211,000.
Cadillac Escalade ESV- dola 79,295
Porsche Panamera Turbo S - dola 190,200
Msaada anaotoa katika jamii
Ni balozi wa kampeni mbalimbali za kusaidia jamii kama Animal Rescue Foundation, Boys & Girls Clubs of America, Brotherhood Crusade, Eat. Learn. Play. Foundation.
Pia kuna taasisi kubwa ambazo zinamtumia kama balozi wao ambazo ni United Nations Foundation, V Foundation for Cancer Research NBA Cares, Nothing But Nets, Partnership for a Healthier America,
Amewahi kuchangia dola 100,000 kwa shule moja iliyopo Ohio ambazo zilitumika kununua vifaa na kulipa makocha wa kufundisha mpira wa kikapu.
Bata na uhusiano
Yupo kwenye ndoa tangu mwaka 2011 na mrembo muigizaji Ayesha Curry ambaye wamefanikiwa kupata watoto watatu ambao ni Riley Elizabeth Curry, Ryan Carson Curry na Canon W. Jack Curry.
Kwa mantiki hiyo mwanetu wa nguvu wa Magazine yetu pendwa ya Mwananchi Scoop, kupitia mchezaji huyo wa kikapu unaweza ukahamasika kama ulikuwa na ndoto ya kuwa mwanamichezo unaweza kupata fursa nyingi kuna msemo usemao safari moja huanzisha nyingine.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi
Leave a Reply