Siri za matajiri watu wasio na kipato cha uhakika hawazijui

Siri za matajiri watu wasio na kipato cha uhakika hawazijui

  1. Watu wasio na kipato cha uhakika wanapenda kutumia kama vile wana utajiri wakati matajiri huwekeza wakiawalenga watu wa sio na kipato cha uhakika kuja kununua.

Hata ukiangalia watu wanaovaa vito vya thamani, saa za thamani, mavazi ya thamani sana na vitu vya kutumia vya thamani ni watu wasio na kipato cha uhakika wakati matajiri sio watumiaji wazuri wa manunuzi ya vito vya thamani na makocho kocho ya thamani.

Kwao hufikiria zaidi kuhusu uwekezaji na kupanua biashara zao kuliko kufanya matumizi ya kufuru wakati watu wasio na kipato cha uhakika wakipata fedha watahakikisha wanafanya matanuzi ya kufuru kwa kununua vitu ambavyo wala havikuwa na umuhimu kwao na kuandaa hafla za matanuzi ya mwana ukome.

Siyo kwamba matajiri hawafanyi hafla, la hasha, hufanya lakini hafla hizo zinakuwa kwenye ratiba tangu mwanzo wa mwaka wanapaojipangia bajeti za matumizi yao binafsi na familia.

  1. Watu wasio na kipato cha uhakika hupenda kuchangamana au kujenga urafiki na wenzao ambao nao kipato chao ni cha kugongea ulimbo, wote wanalia kilio cha aina moja cha ukata na ugumu wa Maisha hakuna wa kumkimbilia mwenzake akikwama.

Ni vyema kama unajijua kwamba kipato chako siyo cha uhakika basi changamana na watu waliokuzidi kifedha au kimaarifa au kielimu, yaani watu ambao watakuongezea thamani na kukupa changamoto za kujikwamua kutoka hali mbaya ya kifedha uliyo nayo na kuwa na kipato cha uhakika kwa kuwekeza na kuchangamkia fursa.

  1. Watu wasio na kipato cha uhakika lakini wana elimu mujaarabu wanajisahau na kuringia elimu yao wakati elimu yetu haifundishi namna ya kuwa Tajiri bali inatuandaa kuja kuwa waajiriwa baada ya kuhitimu.

Hivyo ni vyema baada ya kupata elimu na kuhitimu kuanza kujiendeleza kwa kujifunza mbinu mbalimbali za ujasiriamali na uwekezaji sambamba na kuanza kufanya biashara au kuanzaisha shughuli za kiuchumi zitakazokuwezesha kuwa na kipato cha uhakika.

  1. Kila mtu awaye yoyoye anaweza kuwa na fedha kama anafikiria kuwa na fedha kwa hiyo kama unataka kuwa na kipato cha uhakika basi fikiria kuhusu utajiri. Wote tunajua kwamba sisi ni kile tunachowaza kwa hiyo mawazo yako na matarajio yako ndiyo yatakayoamua matokeo.
  2. Jambo ambalo ni muhimu sana ambalo watu wasio na kipato cha uhakika hawalijui ni kujali muda tofauti na matajiri ambao hujali sana muda.

Watu wasio na kipato cha uhakika kwao muda siyo kipaumbele chao na ndiyo maana mipango yao mingi wanayoifanya hawaweki mstari mfu (dead line) hufaya tu na kuacha mambo yajiendee yenyewe.

 

  1. Ajizi au kuahirisha mambo bila sababu ya msingi. Je umeshawahi kusikia msemo usemao ‘Ajizi nyumba ya njaa’? msemo huu unamaanisha kwamba ukiwa na ajizi au kupenda kuahirisha mambo unakaribisha umasikini.

Matajiri wengi hupanga mipango na kuanza utekelezaji bila ajizi na ndiyo maana wanafanikiwa tofauti na watu wasio na kipato cha uhakika.

  1. Watu wasio na kipato cha uhakika hutegemea zaidi kipato kutoka katika mkondo mmoja.

Kama ni ajira basi atategemea kipato kutoka katika mshahara wake tu basi na kama ni ujasiriamali basi atakuwa na kabiashara kake kadogo hako hako miaka nenda rudi wala hafikirii kuongeza mtaji na kufungua biashara nyingine ili kupanua wigo wa kujiongezea kipato.

Kwa upande wa matajiri wao hawategemei mkondo mmoja wa wa kujiongezea kipato bali hufungua mikondo mingi ya kibiashara kila anapopata faida ili kujihakikishia kipato cha uhakika.

  1. Huwezi kupata utajiri kwa kutegemea mshahara. Wote tunajua kwamba ni vigumu sana kupata utajiri kwa kutegemea mshahara labda uibe.

Kama unataka kuwa Tajiri tumia mshahara kwa kuanza ujasiriamali kidogo kidogo huku ukipanua wigo kwa mikopo yenye riba nafuu ili kuongeza mtaji.

Matajiri wengi walianza ujasiriamali na kuwekeza kidogo kidogo huku wakitia shime kwenye kile wanachokifanya na hatimaye kuwa matajiri wakubwa.

  1. Ukiamua kujiingiza kwenye ujasiriamali kwa lengo la kutafuta utajiri usitegemee Maisha kuwa Kitonga yaani mteremko.

Mwanzoni utapata tabu sana na Maisha yatakuwa magumu kwelikweli lakini kwa jinsi unavyotenda kwa juhudi kubwa na maarifa hakika utaona matunda ya jasho lako ndiyo pale waswahili wanasema jasho la mtu haliendi bure.

Matajiri wengi leo hii ukiwauliza walipotoka utagundua kwamba walipitia wakati mgumu na walipata vikwazo vingi mpaka kufikia mafanikio waliyo nayo leo hii.

Kama unataka kuanza kuwekeza katika ujasiriamali wakati ukiwa bado uko kwenye ajira basi zingatia haya niliyo yaeleza hapa lakini pia nakushauri usome kitabu cha Cashflow cha Robert Kiyosaki kitakusaidia sana kukufungua kifikra.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags