Sina mpango wa kufungua kanisa, biashara ya muziki wa injili imekua

Sina mpango wa kufungua kanisa, biashara ya muziki wa injili imekua

Sanaa hubeba, uhalisia wa mambo ambayo yanaizunguka jamii, haijalishi ni sanaa ya aina gani, inaweza kuwa uchoraji, uchongaji, uigizaji, au muziki. Uhalisia huo ndiyo unapelekea wasanii kupata mashabiki wengi kwa kuwa mambo yaliyomo kwenye kazi za sanaa yanagusa jamii moja kwa moja.

Hii inajionesha kwa mwimbaji wa nyimbo za injili, Walter Chilambo, ambaye ameamua kutumia uhalisia wa mambo anayopitia kwenye maisha na kuyaweka kwenye mistari ya nyimbo zake.

Wakati akizungumza na Mwananchi Scoop amesema mood ya kuandika nyimbo huwa anaipata kutokana na situation anazopitia, inaweza kuwa furaha au huzuni.
Walter amesema ana nyimbo nyingi ambazo huwa zinafanya apate wakati mgumu kwenye kuziachia.

“Kabla sijaachia wimbo huwa napata wakati mgumu sana kwa sababu nina nyimbo nyingi nzuri, lakini pia huwa nazingatia Mungu anipe amani ya moyo kwa wimbo ninaotaka kuachia,
Mfano kwenye wimbo wangu ‘Sijawahi ona’ nilikuwa na nyimbo kama tatu nimezichagua lakini bado nikawa sina amani ya kuziachia, nikapata wimbo sijawahi ona kichwani mwangu nikapata amani, nikauachia na haukuwepo kwenye list.” Amesema Walter

Licha ya kuzingatia amani ya moyo amesema anaangalia pia kipindi husika cha kuachia wimbo kutokana na mambo yanavyoenda.
Ametimiza ahadi kwa mama yeke
Imekuwa kawaida kwa wasanii kuachia ngoma zinazohusu malezi ya mama kwa familia, ndivyo ilivyokuwa kwa msanii huyu wa nyimbo za injili, anasema alimuahidi mama yake kumuandikia wimbo na sasa ametimiza ahadi yake.

“Wimbo wa mama una miaka mitatu nyuma na video ina miaka miwili ndani nilirekodi muda mrefu, nilimuahidi mama ipo siku nitamuandikia wimbo mzuri na alivyoona nimeandika alifurahi hadi alilia, kwangu ilikuwa kitu kikubwa sana.”Amesema

Anasema baadhi ya mistari ambayo ipo kwenye wimbo wake mpya uitwao ‘Mama’ unaendana na yale aliyopitia yeye na mama yake.
“Baadhi ya maneno ambayo nimeimba ikiwemo kutembea umbali mrefu , ni kati ya moment nyingi ambazo mama yangu alikuwa anazipitia, kuna muda alikuwa anatembea kwa miguu umbali mrefu anaenda kukopa,hapo labda ada inatafutwa.

Alikuwa anapitia wakati mgumi, anafanya kazi za kiume kabisa, alikuwa anafanya kazi kwenye kiwanda cha seruji (cement) ni mwanamke anatengeneza cement, anavaa mabuti unasema hizi kazi angekuwa anazifanya baba, lakini namuona mama anafanya ”. Amesema Walter
Wimbo wa mama umetoka juzi Machi 13, hadi sasa una watazamaji 5.6k kwenye mtandao wa YouTube

Hali ya biashara ya muziki wa Injili nchini
Anasema kwa sasa muziki wa Injili umeanza kukua watu wanaoimba muziki huo wameanza kujiongeza ni tofauti na miaka nya nyuma.
“Biashara ya muziki wa injili siku hizi imekuwa nzuri kwa waelewa ambao A list na wanaochipukia, siyo kila mtu anajua biashara ya muziki, mimi ni mzoefu wa biashara hiyo, gospel imechelewa kufahamu kuwa hata huku tunaweza kujipatia kipato, lakini sisi wengine tulishajiua tangu 2012.

Namshukuru Mungu imeanza kukua watu wanajiongeza wanafanya live , event wanaweka kiingilio kikubwa na kizuri wanapata mafanikio makubwa maisha yetu yanabadilika tunanunua nyumba, magari na tunaishi vizuri na familia zetu Mungu anatubariki kwa sababu tunamtumikia.” Ameeleza Walter

Pamoja na hayo amesema anaamini roho mtakatifu wakimtumia vizuri wanaweza kwenda kimataifa kama wasanii wengine wa nje ya nchi, anatolea mfano wimbo wa ‘Ekwueme’ watu wanauimba bila hata kuelewa maana yake. Anasema hata wao kwa Kiswahili wanaweza kufika kimataifa

Kutokana na tabia ya baadhi ya wasanii kuiga nyimbo za wengine, Walter anawasihi kuacha kufanya hivyo badala yake wasanii wazidishe ubunifu na kuweka Utanzania kwenye baadhi ya nyimbo zao.

Walter kufungua kanisa
Kama ilivyo kawaida kwa baadhi ya wasanii wa muziki wa injili kufungua makanisa yao, Walter amesema kwa upande wake hajawahi kufikiria jambo hilo, kwa sasa anawaza kufanya muziki wake zaidi.

“Kufungua kanisa sijawahi kufikiria, mimi nafikiria ku-brand muziki wangu, kuufanya uimbaji wangu uwe mkubwa zaidi, tunajua mwisho wa wasanii wa muziki wa injili ni kuwa wachungaji lakini si kila mtu anaweza kubeba hiyo karama maana ni nzito sana.

Kuna mtu mwingine ana hiyo kitu inside Mungu ameiweka inakuwa vizuri, lakini mwingine Mungu amempa karama ya uimbaji, mwisho wa siku Mungu akiniandikia nifanye hicho kitu atanisafishia njia na atanipa njia za kufanya.” Ameeleza

Kuanzisha label ya muziki wa injili
Kama utakuwa mfuatiliaji wa mwanamuziki Walter Chilambo, ‘Love Music’ itakuwa siyo jina geni masikioni na machoni, mwako, mkali huyu wa muziki wa injii anasema mwakani au mwaka huu anatarajia kuifanya iwe ‘Love Music’ iwe label.

“Love Music bado haijawa record label rasmi lakini nafikiri mwakani au mwaka huu nitaifanya iwe record label kwa sababu nataka niitoe nje ya sehemu ambayo nimeiweka.

Sasa hivi ni studio kubwa tu ya video na audio production ambayo inafanya vitu vingi, kwa hiyo kwa sasa bado hatujasaini wasanii japo nimewahi kuwasanidia wasanii wakafikia hatua fulai nina mipango mingine mwakani ikikaa vizuri tunaweza kukiamsha.” Ameeleza

Matamasha ya Injili kuwa na kiingilio
Kumekuwa na baadhi ya mijadala kwenye mitandao ya kijamii ikionesha baadhi ya watu kutofurahia malipo ya kiingilio yanayotolewa kwenye matamasha ya muziki wa injili, Walter amesema kwa upande wake haoni kama kuna ubaya kwani kiingilio kinakuwa kama sadaka.

“Matamasha ya injili kuwa na kiingilio ni vizuri ni kama sadaka kwa sababu majengo yale watu wamelipa ni kama sadaka kanisani, tusipokuwa tunathamini vitu vya Mungu, alafu watu wanalipa viingilio baa na klabu inakuwa siyo vizuri na sisi inabidi tuwekeze.” Amesema

Makali huu wa nyimbo za injili ambaye anafanya vizuri na vibao vyake kama vile Only you.Shwari, Sijawahi ona na vingine amesema kumtolea Mungu kwa njia ya sadaka ni kitu cha kawaida sana .


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post