Safari ya Xouh, Kutoka kuuza duka mpaka kutusua kwenye bongo fleva

Safari ya Xouh, Kutoka kuuza duka mpaka kutusua kwenye bongo fleva

Leo tupo na binti mwenye kipaji kikubwa kwenye upande wa muziki wa Bongo Fleva, si mwingine bali ni Zulfa Mohamed Ibrahim, na jina lake maarufu ni Xouh, wengi walimfahamu kupitia mtandao wa TikTok ambako ndiko alianzia kukiwasha na ngoma yake ya ‘Huyu wa Sasa’ karibu uburudike kwenye jarida hili mwanzo hadi mwisho.

Wakati wengine wakitumia mitandao ya kijamii kwa kujiburudisha, kuna wengine wanaitumia kwa lengo la kupata mafanikio kupitia mitandao hiyo.

Bila ya kutarajia mtandao wa TikTok ukabadili maisha ya mwanamziki wa Bongo Fleva Xouh, pale alipoachia ngoma yake ya kwanza ‘Huyu wa Sasa’ na ikapokelewa kwa mapokezi makubwa na kumtambilisha rasmi msanii huyo kwa wapenzi wa muziki Tanzania na nje ya mipata yake.

Kutambulika kwake kulitokana na kuamini kwenye kipaji chake hadi kufikia hatua ya kutumia hela aliyopata kwa ajili ya ada kununulia simu ili aweze kutengeneza content mbalimbali ya kwenye mitandao ya kijamii.

“Nilipata nafasi ya kwenda chuo baada ya kumaliza form four lakini sikwenda kutokana na matatizo ya kifamilia, unajua mtoto ‘akisapotiwa’ na mzazi mmoja inakuwa changamoto sana, mimi mama yangu ndiyo amenisomesha baba yangu hata kama amechangia lakini ni kwa kiwango kidogo.

Mama alikosa pesa nikaanza kufanya kazi ya kuuza dukani la vyakula, nikawa nachanga hela na mama kwa ajili ya kwenda chuo, hela ilipatikana lakini nilifikiria nikienda chuo kuna vitu vingi vitani-cost kwani itabidi kila siku niwe na nauli nikaona ni bora ninunue simu nitengeneze content na kutumia vizuri mitandao yangu ya kijamii, nilimwambia mama yangu kuwa kwenda chuo itakuwa ngumu mama alinielewa nikanunua simu na kuanza kufanya content. Anasema Xouh huku akilia

Safari ya Xouh kwenye maisha ya utafutaji kwenye muziki  yalianzia hapo, licha ya kujifungulia njia mwenyewe kwenye muziki wake, kwake ni kama ilivyo kwa wasanii wengine ambao wamekuwa wakizungumzia ugumu wanaopata kwa kufanya kazi  bila ya kuwa na management.

Kwa Xouh pia ndivyo ilivyo licha ya kipaji chake kuwashitua wengi, bado tatizo linabaki palepale kwenye management, licha ya kutafutwa na baadhi ya watu wakimuomba wamsimamie.

“Wananitafuta wengi kunisimamia lakini misimamo na vile wanavyokuja kwangu,  mikataba yao migumu unaona kabisa hapa nikiingia nimepotea.

Yupo mmoja aliniambia asilimia 70% achukue mimi anipe 30% na kisha kwenye hiyo ambayo ananipa anataka nivalishe watu wake kuanzia yeye, familia yake na body guard wake, na kwenye nyumba wanakopesha pesa”. Anasema Xouh

Lakini licha ya kukosa management ngoma zake bado zimekuwa zikifanya vizuri kuanzia audio hadi video Xouh anatusanua namna ambavyo anapata pesa kwa ajili ya kusogeza muziki wake.

“Pesa ya kufanya muziki nazipata kupitia digital platform zangu, kuna kitu kinaitwa dashboard nikienda kutoa maokoto na shoot video, mitandao inalipa ukitumia vizuri, unakuta mtu anatumia simu lakini hajui kama simu inaingiza sana pesa, TikTok  na Instagram naziheshimu sana zimeniheshimisha”. Anasema Xouh

Kwa sasa Xouh anatamba na kibao chake kipya kitwacho ‘Usinipelekeshe’ lakini amekuwa na utaratibu wa kuachia ngoma kila baada ya miezi michache, kutokana na hilo  wakati akifanya mahojiano na Mwananchi Scoop anaeleza kuwa amekuwa akipata sapport kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwemo Dulla Makabila, wasanii wanamtia moyo sana kwa kupambania muziki wake.

Maisha ya umaarufu kama ilivyo kawaida ya kuwatesa wasanii huku wakati mwingine hupelekea wasanii kufanya vitu vya ajabu ili waweze kulinda bland zao, ugumu sasa umeanza kumkuta msanii huyu.

“Umaarufu unahitaji pesa, na pesa zikiisha unapagawa, maisha niliyokuwa nikiishi mwanzo, nikiwa na pesa au nisipokuwa nayo ilikuwa sawa lakini kwa sasa siwezi kwenda sehemu sina pesa, lazima niwe nazo za kutosha, kila muda unajiuliza unapata wapi hela nivae vizuri watu wakiniona waseme huyu ni msanii.” Anasema Xouh

Xouh hadi sasa ana zaidi ya ngoma tano ambazo amekuwa akizitoa kwa mfululizo, huku sababu kubwa ya kufanya hivyo ameeleza kuwa hataki kusahaulika kwani anaona kuna baadhi ya wasanii wanaotoa ngoma kwa kuchelewa wamekuwa wakisahauliwa na mashabiki wao.

Kwenye burudani week hii tumemaliza hivyo na msanii Xouh. Usiache kutufatilia kupitia mitandao yetu ya kijamii kwa jina la mwananchi scoop.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post