Sababu ya Dj kula sahani moja na wasanii

Sababu ya Dj kula sahani moja na wasanii

Sio ajabu kuona Ma-DJ nchini nao wanakuwa maarufu kama ilivyo kwa wasanii wa Bongofleva.

Wamekuwa wakiandaa shoo zao wenyewe, kushinda tuzo za kimataifa, kuwa na idadi kubwa wa wafuasi katika mitandao ya kijamii, hivyo nao wanatengeneza fedha.

Wasanii wakubwa kama Diamond Platnumz na Harmonize wamekuwa wakizunguka duniani na Ma-DJ wao wao ambao ni Vasley na Seven, hiyo ni ishara ya tasnia kukua katika eneo hilo.

Katika nchi ambazo tasnia ya muziki imepiga hatua kubwa, DJ ni mtu wa muhimu na anapewa thamani yake, ndiye anakusanya muziki kutoka vyanzo mbalimbali na kuucheza kwenye vyombo vya habari, klabu na sehemu nyingine zenye mjumuiko wa watu.

DJ Khaled kutokea nchini Marekani amekuwa mfano wa kuigwa kwa Ma-DJ wengi duniani, amekuwa na nguvu ya ushawishi kwa wasanii wengi wakubwa kama Jay Z, Diddy, Rihanna, Burna Boy, Drake, Cardi B, Nipsey Hussle na Beyonce ambao amewashirikisha katika kazi zake.

Kwa mujibu wa Jarida la Forbes, utajiri wa DJ Khaled ni Dola36.6 milioni, wastani wa Sh84 bilioni, na ni miongoni mwa waburudishaji wanaolipwa fedha nyingi ikiwa ni kati ya Dola300,000 hadi Dola499,000 (Wastani wa Sh699.3 milioni hadi Sh1.1 bilioni).

Wakizungumza Mwananchi, DJ Sinyori, Dj Ommy Crayz na DJ JD

DJ Sinyorita ambaye ni kati ya wanawake wachache nchini wanaofanya kazi hiyo, anasema kwa sasa, jamii imetambua umuhimu wao katika kuburudisha jambo linalowafanya wadau wanaomiliki sehemu mbalimbali za starehe kuwapa nafasi.

Anasema siku za nyuma walikuwa hawaamini kama DJ anaweza kuiongezea thamani biashara kutokana na aina ya burudani anayotoa ila sasa mambo yamebadilika.

“Muhimu ujue kusherehesha, siyo kila mtu anaweza hilo, hivyo ukibamba mashabiki wanabamba na wewe na muajiri wako anapata mlichokubaliana na kila kitu kinakuwa sawa," amesema DJ Sinyorita.

Utakumbuka mwaka jana DJ Sinyorita alishinda tuzo ya DJ Bora Afrika kutoka All Music Africa Awards (Afrima) baada ya kuwabwaga DJ Moh Green (Algeria), Black Coffee (South Africa), DJ Cuppy (Nigeria), DJ Impossible (Angola) ,DJ Kaywise (Nigeria) na DJ Mix Premier (Ivory Coast).

Kwa upande wake DJ Ommy Crazy amesema kwa kipindi cha sasa Ma-DJ wamejizolea umaarufu zaidi kwa sababu nyakati zinabadilika, watu wanataka kuburudika kwa muda mrefu na kusikiliza aina tofauti ya muziki jambo linalowafanya watu wengi kuthamini kazi ya DJ.

“Watu wanakuwa wanaangalia kipi ni sahihi na afadhali, mfano msanii anatumbuiza kwa saa moja au saa moja na nusu halafu anaondoka au DJ ambaye anawaburudisha kwa saa nne na ladha tofauti ya muziki,”alisema DJ Ommy Crayz.

DJ Ommy Crayz ameeleza kwamba, teknolojia ya kisasa imekuwa ikiwarahisishia kazi zao na kuwafanya wao kuwa maarufu kutokana na kazi zao hii yote ni kwa sababu wanapata vifaa bora vyenye uwezo wa kuonesha talanta zao.

“Teknolojia ya kisasa imekuja kurahisisha baadhi ya mambo mfano zamani tulikua tunatembea na CD lakini sasa vitu vyote unapata katika kompyuta mpakato (laptops),”alisema DJ Ommy Crayz.

Nae DJ JD ambaye ni mmoja kati ya Ma-DJ waliosikika sana katika miaka ya 1990 ameeleza katika kipindi cha nyuma hali ya kimaisha ya Ma-DJ wengi ilikua tofauti na sasa kutokana na teknolojia iliyopo kipindi hicho ilikua sio rafiki.

“Katika kipindi cha nyuma ukubwa wa DJ ulikua ni wa eneo au mtaa fulani tofauti na sasa, ambapo teknolijia imefanya ma DJ wengi kujulikana mpaka nje ya nchi,” amesema.

DJ JD ameeleza katika suala la kipato kwa sasa, ni dhahiri Ma-DJ wa sasa wanapata kipato kikubwa tofauti na zamani, hii yote ni kutokana na mabadiliko ya teknolojia.

Amesema kwa miaka ya zamani watu walikuwa wanaamini DJ ni mtu ambaye hana thamani katika jamii jambo ambalo lilikuwa si kweli, watu walikua wanaamini ili usiwe muhuni mpaka ufanye kazi kama kuwa daktari na sio DJ.

Neno kwa Ma-DJ wanaochipukia

DJ Sinyorita amesema kwa Ma-DJ wanaochipukia sasa wanatakiwa kuleta vitu vya tofauti ambavyo vikisikika masikioni mwa watu, viwaburudishe maana kuwa DJ lazima ujue namna gani ya kusherehesha watu.

“Naweza kusema wanaochipukia wanatakiwa wajue wanachokifanya, watengeneze kazi nzuri lakini wasiangalie sana ushindani na badale yake wawe wao kama wao,” amesema.

Ameongeza kwa kusema changamoto ziwe kama mafunzo katika kazi zao, kwa kuwa sio kila mtu anaweza kupenda ulichokifanya hivyo wanatakiwa wasikate tamaa, waamini katika ndoto zao.

DJ Ommy Crazy ameeleza kwamba nidhamu ya muda katika kazi mfano kuwahi eneo la tukio, heshima kwa watu ni vitu muhimu sana, hivyo wanapaswa kuzingatia.

“Kuwaheshimu watu unaowafanyia kazi, na mashabiki zao ni jambo la muhimu, pia kuwa mbunifu katika kazi ni kitu cha kuzingatia sana maana utofauti wako wa kazi ndio utakupa heshima kwa watu na kusema wewe ni bora,” amesema DJ Ommy Crazy.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags