PURA kutoa uelewa wa fursa sekta ya Petroli kwenye Maonesho ya Bidhaa Zanzibar

PURA kutoa uelewa wa fursa sekta ya Petroli kwenye Maonesho ya Bidhaa Zanzibar

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema kuwa imejipanga kuwafikia wananchi na kuendelea kutoa uelewa wa masuala yahusuyo sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini pamoja na fursa zilizopo kwenye sekta husika.
 
Hayo yamebainishwa na Mjiolojia wa PURA, Ebeneza Mollel wakati wa 
maonesho ya Sita ya bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanayoendelea visiwani Zanzibar.
 
Mollel amesema PURA imejipanga kutoa uelewa huo kwenye maonesho hayo na kuongeza kuwa 
utasaidia kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli na hivyo kuongeza tija kiuchumi kwa taifa kuanzia ngazi ya mwananchi mmoja mmoja.
 
“Moja ya majukumu ya PURA kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 ni kuhakikisha inasimamia ushirikishwaji wa wazawa kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli, hivyo maonesho haya ni moja ya njia za kuwafikia wananchi na kuwapa uelewa wa namna bora ya kuwa sehemu ya shughuli hizo,” alifafanua.
 
Mollel aliongeza kuwa Watanzania wanaweza kushiriki kwenye shughuli hizi kwa kupata nafasi za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kuuza bidhaa na kutoa huduma kwa kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na kujengewa uwezo kutumia fursa zinazotokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali.
 
“Natoa wito kwa Watanzania wote watakaoweza kufika kwenye maonesho haya kutembelea banda la PURA ili kufahamu fursa zinazopatikana kwenye miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa nchini pamoja na namna bora ya kupata fursa husika,” aliongeza.
 
Kwa upande wake, Mjiolojia Faustine Matiku amesema tofauti na kutoa uelewa wa masuala ya fursa na ushirikishwaji wa wazawa kwenye sekta, watakaotembelea banda la PURA watapata fursa ya kujifunza kuhusu masuala ya mnyororo wa thamani katika sekta ya mafuta na gesi, utafiti na uzalishaji unaoendelea kwenye vitalu mbalimbali nchini, hali za leseni za utafutaji, mradi wa usindikaji gesi asilia kuwa katika hali ya kimiminika (LNG) na masuala mengine ya kiufundi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags