Pogba afungiwa miaka minne

Pogba afungiwa miaka minne

Kiungo wa Juventus, Paul Pogba amefungiwa miaka minne kujihusisha na soka baada ya kukutwa na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu.

Pogba ambaye amewahi kuwa mchezaji ghali zaidi duniani, amekumbwa na kadhia hiyo, na inaonekana kuwa ndiyo mwisho wake wa maisha ya soka.

Mwanzoni mwa msimu huu, taarifa mbalimbali zilikuwa zinasema kuwa Pogba ambaye amewahi kuitumikia Man United, anataka kustaafu soka kutokana na kukumbwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini baadaye aliachana na mawazo hayo.


Mfaransa huyo ambaye mwezi ujao anatimiza miaka 31, alisimamishwa kwa muda baada ya kushindwa kufanya kipimo cha dawa hizo miezi kadhaa iliyopita na mamlaka za soka nchini Italia.

Vyanzo mbalimbali likiwemo gazeti la Daily Mail, vimesema kuwa Pogba alifanyiwa vipimo hivyo mara mbili na mara zote vimeonyesha kuna sampuli ya dawa zisizoruhusiwa michezoni.

Fabrizio Romano alithibitisha: “Paul Pogba amepima doping ya testosterone kuwa chanya pia na sampuli mbadala zinaonyesha hivyo."

Staa huyo alionekana kwenye mchezo kati ya Juventus na Udinese, Agosti 12 na inaelezwa ndiyo siku aliyochukuliwa vipimo hivyo, lakini majibu ya kufungiwa na mamlaka za soka za Italia yametoa leo rasmi.

Hata hivyo, wanasheria wa mwanasoka huyo awali waliigomea adhabu hiyo wakidai mteja wao hatumii dawa hizo, lakini bado amepewa adhabu hiyo huku mlango wa kukata rufaa ukiwa wazi.

Kama atashindwa kwenye hiyo rufaa ina maana kuwa atakuwa nje ya uwanja hadi atakafikisha miaka 35 na unaweza kuwa mwisho wake wa kucheza soka la ushindani akiwa ameshacheza michezo 423 na kufunga mabao 73, kwenye klabu mbili za Man United na Juventus.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags