Phina awatolea uvivu wanaoponda uvaaji wake

Phina awatolea uvivu wanaoponda uvaaji wake

Na Glorian Sulle

Msanii wa muziki wa kizazi kipya anayetamba na kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la “We Huogopi”, Sarah Michael Kitinga ‘Phina’ amewatolea uvivu wale wanaoponda uvaaji wake akisema kwamba inabidi wamzoee kwani alianza uanamitindo kabla ya kuingia kwenye gemu ya muziki hivyo hawezi kuacha.

Kupitia video na picha zake mbalimbali, Phina amekuwa akionekana na mavazi tata yanayoonesha sehemu kubwa ya mwili wake na kupelekea mijadala kwenye mitandao ya kijamii ambapo wapo wanaomponda.

Kuhusiana na hilo, Phina amefichua kwamba suala la mavazi kwake linatokana na kupenda ubunifu na mitindo lakini pia kama msanii inabidi awe tofauti na wengine.

“Katika suala la mavazi wengi wananiambia niwe kawaida, ila samahani kwa hilo siwezi kuwa kawaida, suala la mitindo sijaanza nikiwa mwanamuziki nilianza zamani, hivyo inabidi wazoee na pia siwezi kumridhisha kila mtu,” amesema sema kwake kiki siyo kipaumbele kama ilivyo kwa wasanii wengine.

Katika hatua nyingine, msanii huyo ambaye ni zao la shindano la kusaka vipaji, ‘Bongo Star Search 2018’ aliyeingia rasmi katika kiwanda cha muziki wa Bongo Fleva mwaka 2021 alipotoa wimbo wake wa kwanza ulioenda kwa jina la “In Love”, mwenyewe amekiri kuwa licha ya wimbo huo kuwa wa kwanza kwake, lakini uliomtambulisha zaidi na kumfungulia milango katika sanaa ni ‘Upo Nyonyo’.

Amesema katika safari yake ya muziki amepitia mengi lakini kubwa zaidi ni lile la kuwashawishi wazazi wake suala la kuingia kwenye muziki.

“Nilipata shida sana kuwashawishi wazazi wanipe ruhusa ya kuingia kwenye muziki," amesema.

Msanii huyo ameeleza kuwa baadhi ya nyimbo alizotoa kama vile “Sisi ni Wale” zinahusu maisha yake moja kwa moja kutokana na visa na mikasa aliyowahi kupitia katika safari yake ya kujitafuta kimuziki.

“Sisi ni Wale ni wimbo ambao unanihusu moja kwa moja kwa sababu napambana mpaka hapa nilipofika kuna vitu vingi nimepitia, tangu nipo shule kuna wakati nilikuwa natamani kukata tamaa, nilipoteza marafiki sapoti ya familia pia ilipungua. Ukiangalia maisha yangu nilipotoka na sasa ni tofauti, Sisi ni Wale inagusa maisha yangu,” amesema.

Mbali na hayo, Phina ametoa ushauri kwa wasanii chipukizi akiwaasa kuwa wavumilivu na kutokata tamaa lakini watumie muda mwingi kuwekeza kwenye muziki wao.

“Ninachoshauri wanamuziki wanaochipukia wasikate tamaa, wapambane na kikubwa wamuombe Mungu,” amesema.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2022 Phina alishinda tuzo mbili za Tanzania Music Awards (TMA) katika vipengele viwili Mwanamuziki Bora Chipukizi na Mtumbuizaji Bora, mpaka sasa msanii huyo ana nyimbo zaidi ya 15 zinazomtambulisha kwenye kiwanda cha muziki Bongo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags