Pamba kali za kutupia ukiwa vacation

Pamba kali za kutupia ukiwa vacation

Mambo vipi, najua mko poa watu wangu wa Fashion kama kawaida tunakutana tena hapahapa katika magazine yetu ya Mwananchi Scoop kujuzana yanayojiri kwenye fashion.

Leo tumekusogezea aina ya nguo za kuvaa ukiwa vacation,  kikubwa unatakiwa ujue kila nguo ina sehemu yake ya kuvaa.

Kutokana na pilika za watoto shule na kufanya kazi mwaka mzima, baadhi ya familia huamua kusafiri na  kwenda mapumzikoni kwa lengo la kuachana na yale waliyokuwa wakipambana nayo mwaka mzima.

Hata hivyo, ili mapumzo yaende vizuri kama umeamua kwenda nje ya nchi, mkoani au kukaa hotelini kwa muda fulani kulingana na matakwa ya mtu, uchaguzi wa mavazi ni kitu cha muhimu.

Inawezekana una nguo za aina nyingi na nyingine haujawahi kuzivaa bado lakini cha kujiuliza ni mavazi ya aina gani utavaa pindi ukiwa mapumziko na marafiki zako, mke, mumeo, ndugu au watoto?

Kwa mujibu wa wanamitindo wa mavazi, epuka kuvaa mavazi rasmi (official) kwa sababu ni kipindi ambacho mwili na akili yako inataka kuwa huru.

Fulana nyepesi

Kwa upande wa wanaume, hizi ni nguo ambazo hutakiwi kukosa wakati wa mapumziko kwa sabubu zitakupa mvuto wa kipekee na uhuru wakati wote unapokuwa sehemu za kustarehe hasa ukivalia na kaptula huku viatu ukapigilia sendo.

Mwanamitindo Mwamvi Daniel anasema fulana nyepesi zinamvuto ambao humfanya mvaaji kupendeza na kupata hewa.

Nguo za kuzungusha ‘wrap dresses’

Hizi ni nguo ambazo hupendelewa kuvaliwa na wanawake kwa sababu huwafanya wanaovaa kuwa huru. Unapokuwa mapumziko vaa nguo hizi hasa zilizoshonwa kwa kitambaa chepesi kinachowezesha hewa kupita na mwili kuwa huru. Nguo hizi zinaweza kuwa sketi au gauni kwa upande wa sketi vaa na ‘crop top’ au blauzi ya mikono myembamba.

 Pia, kama upo sehemu za fukwe unaweza kuvaa sketi za kuzungusha za kitambaa cha Bahama kwa sababu kina pamba laini.

Veronica Mambwe anasema nguo za kuzungusha humfanya ajihisi huru na humpa urahisi kuivaa hata akiongezeka mwili.

Anasema kwa kipindi hiki ambacho yupo mapumziko anaona ndiyo wakati wake wa kuwa huru.

Bwanga

Vazi hili hunoga likiwa limeshonwa kwa kitambaa chepesi.

 Nguo hizi hazichagui umbile la wanene na wembamba wote wanavaa kwa staili mbalimbali.

Mmoja wa wabunifu wa mavazi anayejukana kwa jina la Frivola anasema bwanga ni nguo huru kwa maumbile yote ya wanawake hasa ukilipatia kitambaa chenye maua mazuri na yenye rangi inayovutia.

 Hili vazi siyo lakukosa kipindi hiki kwa sababu huuachia mwili na wakati wowote ule linapovaliwa mvaaji huwa huru.

Vazi hili huvaliwa sehemu yoyote na unaweza kuvalia na topu kulingana na rangi za bwanga utakalovaa.
Kimono
Hili ni vazi ambalo huvaliwa juu ya nguo, muundo wake umetengenezwa kwa uwazi wa mbele na kuipa nafasi nguo iliyovaliwa ndani kuonekana vizuri. Katika mapumziko baadhi ya watu hupendelea kwenda sehemu za fukwe huhitaji kujikinga na upepo, hivyo kimono ni vazi sahihi kwa sababu huwapa wanawake muonekano wa kipekee.

Mwajuma Selemani anasema licha ya kipindi cha mapumziko lakini kujistiri kwa mwanamke kupo palepale.

“Mimi nikitinga kimono changu ndani nikavaa na taiti ndefu juu vesti imeisha hiyo(vazi lake limekamilika,” anasema Mwajuma.

Nguo za kufanana ‘two pieces’
Hizi ni aina ya nguo ambazo zimeushika ulimwengu wa mitindo mwaka huu japo awali ziliwahi kuvaliwa.


Baada ya kutambulishwa na kuvaliwa na watu wengi zimeendelea kubamba, hivyo katika kipindi cha mapumziko usiache hii fasheni ikupite.

Jackson Jorwa anasema akiwa mapumziko hupendelea kuvaa kaptula na shati la mikono mifupi .

Zulfa Hussein anasema akivaa suruali na shati ambazo zimeshonwa kwa vitambaa vya kufanana hujiona amependeza na huwa huru.

Vazi hili huvaliwa na jinsia zote, kwa upande wa wanaume huwa shati na kaptula na wakati mwingine suruali japo kwa kipindi cha mapumziko kaptula ndiyo hufaa zaidi.


Sendo na kandambili ‘slippers’
Siyo kipindi cha kuvaa viatu na soksi kama unaenda ofisini au shughuli rasmi unatakiwa uvae viatu vitakavyo kupatia hewa na kukuacha huru bila kuathiri muonekano wako wa kuvutia.
Tydo Master, mbunifu wa mavazi na mwanamitindo, anasema sendo na kandambili zinavutia zaidi unapokuwa upo sehemu za fukwe kwa sababu ya kutoupa nafasi mchanga kukaa kutokana na uwazi uliopo.

Ni vyema kuvaa sendo au kandambili kipindi hiki cha mapumziko kuendana na aina ya nguo utakazovaa.


Vinjunga (kaptula)
Ni kipindi cha kujiachia na kupendeza zaidi, siyo wakati wa kujibanabana kutokelezea na kinjunga katika mtoko wako wa mapumziko. Kwa wanawake unaweza kuvaa kinjunga kinachoachia mwili au wakati mwingine kubana kwa juu na kuvalia na topu au shati huku ukiwa umevaa viatu aina ya sendo.
Pia, wanaume wanaweza kuvaa vinjunga na shati au vesti.

Akizungumza na Mwananchi Scoop Mkaile Jamal anasema kinjunga ni vazi linalowapa uhuru wavaaji hasa kutokana na joto kuongezeka kwa kiwango cha juu, hivyo huwafanya wawe huru na kupata hewa.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags