Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimesema kipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mchakato wa kuanza kwa kozi ya urubani wa ndege inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu na itagharimu kiasi cha Sh.70 Milioni.
NIT imesema kati ya fedha hizo kiasi cha Sh. 21 Milioni ni gharama za kozi hiyo ngazi ya awali ambayo itamuwezesha mwanafunzi kusoma masomo ya awali na kuruka angani masaa 50.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete aliyekitembelea chuo hicho kwa lengo la kujifunza vitu mbalimbali.
Profesa Mganilwa alisema mwanafunzi wa ngazi ya awali akihitimu na kupata leseni yake ya kurusha ndege za watu binafsi atapaswa kuendelea kusoma tena miaka miwili na nusu ili kuweza kupata leseni ya biashara ya CPL ambayo itafanya gharama ya kozi hiyo kuwa jumla ya Sh. 70 Milioni.
"Mwanafunzi huyu akiwa na jumla ya Milioni 70 atasoma masomo hayo ya awali na hayo mengine yatakayomuwezesha kupata leseni ya CPL ambayo itamuwezesha kuruka masaa 200 na kufanya masomo mbalimbali ya hali ya hewa, baada ya hapo muhitimu huyu ataweza kuajiliwa na Mashirika ya ndege la kibiashara ambayo yanaweza kuwa ATCL au Precision Air ila atatakiwa kuanza na ndege ndogo zenye abiria 70," alisema na kuongeza
"Hata hivyo baada ya hapo atatakiwa kusoma tena kidogo ili apate leseni inayoitwa ATPL akipata hiyo anaweza kuendelea kusoma zaidi hadi kufikia hatua ya kuendesha ndege aina ya Dreamliner," alisema Profesa Mganilwa
Profesa Mganilwa alisema wanamatumaini kuwa kabla ya mwaka huu kuisha kozi hiyo itakuwa imeanza rasmi hivyo wanafunzi wa kitanzania wataanza kuipata elimu hiyo ya urubani hapa nchini.
Alisema ili kozi hii ianze lazima wapate ithibati kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) hivyo katika mchakato wa kupata kibali hicho wapo kwenye hatua ya nne ambayo inawataka wawe na ndege ambazo amebainisha kuwa tayari Serikali imenunua ndege mbili zinazogharimu Dola za Marekani 600,000 sawa na Bilioni 1.2 za Kitanzania kwa kila moja.
"Ninaimani tutapata kibali hiko kwa sababu malipo ya awali ya ndege hizo tayari yameshafanyika, matarajio ni kwamba mwezi wa saba au wa nane ndege hizo zitafika hapa nchini, lakini pia walimu wapo, mitaala tunayo yaani kila kitu kimekamilika kwa maana maandalizi upande wa kwetu umekamilika," alisema Profesa Mganilwa na kuongeza
"Kwahiyo kabla ya mwisho wa mwaka yaani kabla ya watu kwenda kula krismasi mwaka huu vijana wa kitanzania wataanza kuwa angani kujifunza urubani," alisema
Kwa upande wake Naibu Waziri Mwakibete alisema kuwa mipango waliyonayo NIT kuanza kufundisha marubani ni mizuri na unalengo la kupata wataalamu wakutosha.
"Linalofanywa na NIT ni jambo jema sana kwani ilizoeleka nchini kwetu ukitaka kuwa rubani lazima ukasome nje ya nchi yaani huko Sauzi Afrika au Ulaya, lakini kozi hii sasa itatolewa hapa nchini na ninauhakika chini ya Rais Samia tutapata wataalamu wa kutosha wa kurusha ndege zetu, kuendesha na kusimamia miradi mikubwa ikiwemo ya Reli ya Kisasa (SGR)," alisema
Leave a Reply