Nyimbo zake za mwanzo kama Mafungu (2009) na Nivute Kwao (2011) ndizo zilimpatia umaarufu kimuziki Dayna Nyange na hadi sasa anaendelea na kazi yake hiyo ya kutoa burudani kwa mashabiki huku akiuza sanaa yake.
Huyu alianzia muziki Dodoma alipokulia na sio Morogoro kama wengi wanavyodhani, Moro alienda baada ya kuolewa na huko ndipo alianza kuwika kimuziki hadi leo tunaye Dayna katika Bongo Fleva. Fahamu zaidi.
Kwa miaka mashabiki wengi wamekuwa wakiamini Dayna Nyange ndio jina lake la kuzaliwa na ameamua kulitumia tu kwenye muziki wake, lakini ukweli, jina lake halisi ni Mwanaisha Saidi Nyange.
Dayna kabla ya kujikita katika muziki, aliwahi kushiriki mashindano ya urembo, Miss Dodoma na kushika nafasi ya nne, hiyo ni sawa na Lulu Diva ambaye alishinda Miss Kibaha kisha Miss Pwani ila alishindwa kuendelea baada ya kifo cha baba yake.
Kipindi anaanza muziki, Dayna Nyange alikuwa akifanya rap na siyo kuimba kama ilivyo sasa na huyu si msanii pekee wa kike kutoka kwenye rap hadi kuimba hapa Bongo, kuna Vanessa Mdee, Lady Jaydee na Aika wa kundi la Navy Kenzo.
Rapa kutoka kundi la Weusi, Nikki wa Pili ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, ndiye alimshauri Dayna kuachana na rap kwa sababu wasanii wa kike kwenye rap ni vigumu kutoka na kufanya vizuri.
Dayna Nyange alipenda rap kwa sababu wasanii waliomvutia kimuziki ni AY na Fid Q ambao wameshirikiana katika ngoma kama Shimo Limetema (2009), Jipe Shavu (2013), Ujio wa Verse (2014), Upo Hapo (2017), Microphone (2018) n.k.
AY alimvutia Dayna kwa namna anavyochana (flow/rap style), huku Fid Q kwa namna anavyoandika na kupangilia mistari katika nyimbo zake ingawa anakiri ilikuwa inamchanganya sana ila alitamani naye aje kuwa na uwezo kama huo.
Tuzo ya kwanza kwa Dayna kushinda katika muziki ni kutoka Mlima Uluguru Awards zilizotolewa Morogoro na baadaye alikuja kushinda tuzo mbili za BEA 2017 kutoka Nigeria ila hadi leo hajawahi kuzipata maana hakuhudhiria hafla yake.
Wasanii wa kike ambao waliwahi kufanya vizuri miaka ya nyuma ambao Dayna anatamani kuwasikia tena kwenye Bongo Fleva ni Enika, Farida na Stara Thomas ambaye alitoa albamu mbili, Nyuma Sitorudi (2000) na Hadithi (2002).
Wakati Enika na Farida wakifanya vizuri kwenye muziki huo, ni kipindi ambacho Dayna bado alikuwa akirap na alikuwa akishangaa wanawezaje kuimba vizuri kwa kiasi hicho, hakudhania na yeye kuna siku ataimba hivyo.
Wimbo wa kwanza wake Dayna kufanyiwa video yake nje ya nchi, ni Chovya (2017) ambayo ilishutiwa Afrika Kusini na Director Msafiri wa Kwetu Studio ambaye alishuti pia video ya Dogo Janja, Banana (2018) ambayo pia ilikuwa ya kwanza kwa msanii huyo.
Dayna Nyange ambaye alimshirikisha Davido katika wimbo wake, Elo (2021), ni msanii wa tatu kutokea Tanzania kufanya kazi na staa huyo wa Nigeria baada ya Diamond Platnumz, Number One Remix (2014) na Joh Makini, Kata Leta (2017).
Utakumbuka Davido alianza muziki katika kundi la KB International nchini Marekani, alipata umaarufu alipoachia wimbo wake 'Dami Duro' ambao ni wa pili kutoka kwa albamu yake ya kwanza, Omo Baba Olowo (2012) chini ya HKN Music.

Leave a Reply