Unaweza kusema mwigizaji Joice Mbaga ‘Nicole Berry’ alikuwa na kiu ya kutumia mitandao ya kijamii. Hii ni baada ya kutupia zaidi ya machapisho 10 kwenye ukurasa wake wa Instagram muda mchache baada ya kutoka rumande kwa dhamana.
Nicole baada ya kutoka aliacha ujumbe unaotoa onyo kwa watu kuchangishwa pesa za kumsaidia kama dhamana.
"Sio sahihi kwa mtu yeyote kuweka pua na mdomo wake kwenye kesi inayoendelea mahakamani, waliyopokea pesa wanazidi kurudisha na haki yangu nimepatiwa, nawasihi sana sihitaji michango yoyote kutoka kwa mtu yeyote," aliandika na kuongezea.
"Yamkini kuna mtu yeyote alinisolola kwa namna yeyote ile kuanzia wasanii wanafiki marafiki feki wanaonigeza sauti na wote nakuahidi nitakurudia punde," amesema Nicole.
Hata hivyo, hakuishia hapo aliendelea kuchapisha video na picha mbalimbali kupitia Insta Story yake zikiwemo video za mzaha. Kupitia machapisho yake wapo walioshusha jumbe za kufurahishwa na kurudi uraiani, wapo wa kumdhihaki na wengine wa kushangazwa kwa kuivamia mitandao ya kujamii kwa haraka badala ya kupumzika.
Utakumbuka Nicole aliyekaa rumande kwa siku 15 na mwenzake Rehema Mahanyu (31), wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, waliachiwa jana Machi 17, 2025, kwa dhamana.
Ikiwa ni baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni, Jumatatu Machi 10, 2025, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kutokana na kupokea amana (fedha) kutoka kwa umma bila kibali cha Benki Kuu (BoT).

Leave a Reply