Nandy kuandikiwa nyimbo, Yupo vizuri!

Nandy kuandikiwa nyimbo, Yupo vizuri!

Kama kuna wasanii wengine wa Bongo Fleva wanaandikiwa nyimbo na kuzitendea haki, basi Nandy ni namba moja, hadi sasa ameandikiwa nyimbo zaidi ya 10 na wasanii wenzake zaidi ya watano na zote aliporekodi na kuzitoa zimefanya vizuri.

Hata wimbo wake mpya ‘Dah!’ unaofanya vizuri sasa ambao umetoka hivi karibuni kwa ajili ya shughuli ya Haji Manara kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake Zaiylissa, nao Nandy kaandikiwa.

Utakumbuka Nandy alitoka kimuziki chini ya Tanzania House of Talent (THT) kupitia wimbo, Nagusagusa (2016) ikiwa ni muda mfupi baada ya kushika nafasi ya pili katika shindano la Karaoke Afrika, Tecno Own The Stage nchini Nigeria.

 Mume wa Nandy, Billnass ndiye ameandika wimbo huo mpya ‘Dah!’ ukiwa ni wimbo wa tatu kumuandikia mkewe ambaye walifunga ndoa Julai 2022 na tayari wamejaliwa mtoto mmoja, Naya. 

 Nyimbo nyingine ambazo Billnass kamuandikia Nandy ni Bugana (2019), walioshirikiana, pia kuna New Couple (2021) kutoka katika EP yake ya pili, Taste (2021). Hivyo Billnass ameungana na Jay Melody, Marioo, Kusah na Lody Music kwa kumuandikia Nandy.

 Hadi sasa Jay Melody ndiye msanii aliyemuandikia Nandy nyimbo nyingi na zote zikafanya vizuri. Jay kamuandikia nyimbo nne ambazo ni Kivuruge (2017), Njiwa (2018) ft. Willy Paul, Hallelujah (2019) ft. Willy Paul na Do Me (2020) ft. Billnass.

Marioo amemwandikia Nandy wimbo wake, Wasikundanganye (2017), ila huu wimbo tayari Marioo alikuwa ameshaurekodi ila Nandy alipousikia ukaupenda na kuomba aurudie uwe wake na ombi lake lilikubaliwa.

Ikumbukwe Marioo ameshawahi kuwaandikia nyimbo wasanii kama Christian Bella (Pambe), Gigy Money (Papa),  Dogo Janja (Banana), Lyyn (Chafu), Shilole (Mchakamchaka), Mwasiti (Bado), Amber Lulu (Jini Kisirani), Ditto (Nabembea) .

Kwa upande wake Lody Music amemuandikia Nandy wimbo, Napona (2022) ft. Oxlade, huu ndiyo wimbo uliofanya vizuri zaidi katika EP yake ya tatu, Maturity (2022), huku Kusah akimuandikia Nandy wimbo, Nibakishie (2020) ft. Alikiba.

Nandy alijizolea mashabiki wengi pindi alipoachia albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018) chini ya Epic Records ikiwa na nyimbo maarufu kama Aibu, Hazipo, One Day, Wasikudanganye, Kivuruge, Ninogeshe.

Ukiachana na Nandy, wasanii wengine walioandikiwa nyimbo na wenzao ni Shilole, Malele (2014) na Say my Name (2016), Mwasiti, Siyo Kisa Pombe (2011), Vanessa Mdee, Siri (2015), Ruby, Na Yule (2015) n.k, zote hizo zimeandikwa na Barnaba.

Wengine ni Lulu Diva (Ona) kaandikiwa na Rich Mavoko, Benson (Hauzimi) - Jay Melody, Peter Msechu (Nyota) - Amini, Lulu Diva (Usimwache) - Daxo Chali, Ruby (Ntade) - Kusah, Diamond Platnumz (Sijaona) - Rich Mavoko, Jux (Sisikii) - Mabeste, Ben Pol (Moyo Mashine) - Godluck Gozbert.

Licha ya kuandikiwa nyimbo baadhi ya wasanii wanaonekana kutopenda kuweka wazi nyimbo walizoandikiwa na kuwataja waandishi wao.

Kutokana na hayo, mzalishaji wa muziki nchini, Bob Manecky ameliambia Mwananchi kuwa msanii akiandikiwa wimbo haki yake inahesabiwa kama mtumbuizaji tu lakini aliyeandika anabaki kuwa na haki ya uandishi, hivyo kila mtu anakuwa na asilimia ambazo anachukua kwenye wimbo huo.

Manecky anasema kwa kawaida kunatakiwa kuwa na maandishi ya makubaliano kati ya msanii na muandishi, ili ikitokea changamoto muandishi aweze kupata haki yake, pia kwenye mikataba hiyo kuna kipengele kinachotaka msanii kutomtaja popote muandishi wake, hivyo kama wakikubaliana msanii analipa anachukua wimbo na hatomtaja aliyeandika.

“Mimi nitaongelea baadhi ya wasanii ambao nimefanya nao kazi wanaona kama wakitaja mtu aliyemuandikia nyimbo mashabiki watamchukulia poa, lakini nadhani siyo kitu kizuri kama mtu amekuandikia wimbo ni vizuri kumtaja ili na yeye aweze kupata michongo mingine,” anasema Manecky.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post