Nancy Sumari na biashara ya vitabu

Nancy Sumari na biashara ya vitabu

Ni wazi kuwa kila binadamu ana kile anachopenda kufanya ili kupata burudani na liwazo katika mwili wake.

Wengine hupenda kutembea ufukweni na kupunga upepo, wengine hupenda kutoka sehemu za starehe na marafiki au wenzi wao na wengine hupenda kukaa nyumbani na kujisomea vitabu mbalimbali vikiwemo vitabu vya taaluma, hadithi, Afya, na vingine vingi.

Utumiaji wa vitabu kama sehemu ya kutuliza akili sio moja ya tamaduni kubwa sana katika jamii za kiafrika lakini bado matumizi ya vitabu yamezidi kuongezeka kutokana na uwepo wa shule na tassisi mbalimbali za kielimu.

Licha ya kuwepo uhitaji wa vitabu vya taaluma bado uwekezaji katika masuala ya maduka ya vitabu ni mdogo sana. Hii inatokana na kutokuwepo kwa mkazo mkubwa na hamasa kwa wafanyabiashara kuwekeza katika biashara hii.

Hata hivyo kwa mrembo Nacy Sumari imekuta ni tofauti kidogo, mwanadada huyu aliyewahi kuwa Miss Tanzania 2005 na mwaka huo huo alikuwa Miss World Afrika ameamua kujikita zaidi katika kuandika vitabu.

Mlimbwende huyo ambaye hivi sasa ni Mkurugenzi wa Bongo5 na Taasisi ya Jenga Hub ambayo inatoa mafunzo ya matumizi ya vifaa vya teknolojia pamoja na ujuzi wa Kompyuta kwa watoto wa miaka 7 hadi 12, amefunguka leo ndani wa Mwananchiscoop anawezaje kuifanya biashara hiyo.

Hivi karibuni, Nancy amezindua kitabu chake kinachojulikana kwa jina la ‘Samia’ kinachozungumza na watoto wote hasa mtoto wa kike moja kwa moja kupitia historia ya maisha ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Sumari anafunguka na kusema biashara ya vitabu hairidhishi kwa sababu taifa bado halijafikia sehemu ya kusema kwamba kusoma vitabu ni tamaduni ya nchi.

“Hata hivyo hii changamoto naitazama kama fursa, kwani  wazazi au walezi, tukiweza kushirikiana nao kwa ukaribu zaidi pamoja na wanafunzi katika kubuni hadithi mbalimbali zitakazowafurahisha na kuwaelimisha watoto, wanaweza kujenga utamaduni wa kusoma vitabu mara kwa mara” anasema

Anasema jamii hasa watoto kama watajenga utamaduni wa kusoma vitabu itazaa haja ya uhitaji wa vitabu vingi zaidi madukani na kuongeza tija katika biashara hiyo hapa nchini.

Hata hivyo anasema moja ya faida ya usomaji wa vitabu mara kwa mara ni pamoja na kuongeza uwezo wa ufikiri, inasaidia kupunguza msongo wa mawazo, kuamsha akili, kuongeza maarifa, kuwa na uwezo wa kujua misamiati mingi ya lugha.

Kwanini aliamua kuandika kitabu cha Samia

Anasema ameamua kuandika kitabu kinachomuhusu Rais Samia ili watu waweze kujua kuwa ni binadamu kama walivyo mwingine amepitia changamoto mbalimbali lakini amefika hapo alipo kwa utashi, uwezo na uzoefu.

Pia anasema ameamua kuandika kitabu hicho kwa lengo la kumuenzi, kumsherehekea lakini watoto hasa wa kike waweze kujifunza kupitia historia ya Rais Samia.

“Ninaamini binti yeyote wa kitanzania, kiafrika na dunia akisoma hiki kitabu cha ‘Samia’ ataweza kuhamasika na kuwa na mtazamo tofauti wa kuchapa kazi, kuamini katika uzoefu na kukubali kushirikiana na watu mbalimbali,” anasema

Hata hivyo anasema wazo la kuandika kitabu hicho lilikuja siku ambayo Rais wa awamu ya tano John Magufuli alifariki dunia na lilikolea zaidi wakati wa uapisho wa Rais Samia.

“Unajua siku ambayo Rais Samia anaapishwa sikumruhusu mwanangu yule wa kike kwenda shule kwa kuwa ilikuwa ni siku ya historia kubwa sana na nikawaza ni tukio la kipekee na hapo wazo la kuandika lilianza,” anasema

Anasema kitabu hicho cha Samia ni cha tatu kuandika kwani cha kwanza ni ‘Nyota yako’ kilichojikita kangazia wanawake wanaoshiriki katika maendeleo ya jamii zao na cha pili kinajulikana kwa jina la 'Haki' ambacho ni maalumu kwa ajili ya watoto ili wazijue haki zao.

Nancy alipoulizwa anampango wa kuandika vitabu vingapi, ajibu ni ngumu kujua kwani hata hicho cha sasa hakuwahi kufikiria kama atakuja kukiandika lakini wazo lilimjia na amelitekeleza.

“Mimi napenda vitabu na nina amini katika nguvu ya hadithi hivyo siwezi kusema nitaandika vitabu vingapi ila nachojua nitaandika vingi tu kadiri nitakavyojaaliwa,” anasema

Kuhusu vitabu vyake kuingia katika mtaala wa elimu

Anasema yeye kama mwandishi aandiki kitabu kwa kutarajia kwenda moja kwa moja kwenye mitaala ya elimu ila mawazo hayo uja baadae na ndio maana kitabu chake cha Haki kipo kwenye taratibu za kuingia katika mtaala.

“Kitabu kuingizwa kwenye mtaala ni kitu nyeti na kinastaili muda na uzito husika, kwa hiyo inachukua muda mpaka Serikali ijiridhishe kwamba kinafaa au kifanyiwe mabadiriko ili kiweze kuiingia, natumani kitabu change cha Haki kinaweza kuigia maana ushirikiano upo mkubwa,”anasema

Mambo matano awashauri wanafunzi wa chuo

Nancy anasema wanafunzi wote waliochuoni wanapaswa kutambua uwezo wako katika ufanyaji wa biashara mvakunvaki

“Watu wamejaaliwa uwezo mbalimbali, wapo wanaoweza wa kuongea vizuri na kushawishi wengine jambo fulani, hivyo tunasisitiza kila mtu kutambua uwezo wake,” anasema

Anasema pia mwanafunzi anapaswa kuwa na mahusiano mazuri na wanafunzi wenzake ikimbidi hata ana wale kutoka vyuo mbalimbali.

“Pia wanafunzi wanapaswa kuacha kumdharau mtu, bali waheshimu kila mmoja wao hata wale wanaofanya usafi sak funi na chooni maana ujui kwamba baraka zako zimefichwa kwa watu hao, kesho yako ni nani ataweza kukusaidi katika matatizo,” anasema.

Anasema wanapaswa pia kujifunza maisha ya kuishi popote na watu wa aina mbalimbali.

Wanaotaka kufanikiwa

Anasema wanawake na wasichana wanaohitaji kufanikiwa wanapaswa kuwa watu wa kujichanganya, wepesi kusikiliza wengine na kutafuta ushauri kwa wale waliofanikiwa bila kuwadharau walio chini yao.

“Hakuna mtu ambaye ni jeshi la mtu mmoja na hiyo inajidhihirisha kwenye hadithi ya Rais Samia ambaye alipata muongozo kutoka kwa watu mbalimbali na imemsaidia kufika hapo alipo.

“Kama unahitaji kufika mbali usipende kwenda mwenyewe shirikiana na watu mbalimbali kutumiza malengo yangu, mfano mimi  nashirikiana na watu na shughuli hizi ninazofanya zinampa fursa ya kujihusisha zaidi na miradi ya kuwawezesha wanawake, kutoa mafunzo kwa vijana na kusaidia katika kuboresha elimu nchini. ,” anasema

 

 

 

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags