Nyota mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Malu Stonch amefariki dunia usiku wa jana baada ya kuanguka ghafla jukwaani katika ukumbi wa Target uliopo Mbezi Beach wakati akiimba pamoja na bendi anayoifanyia kazi ya FM Academia.
Akizungumza na Mwananchi, Kiongozi wa FM Academia, Patcho Mwamba amesema, mwanamuziki huo wakati anaimba alidondoka ghafla na kuangukia uso na kupoteza fahamu huku damu zikimtoka masikioni na kung'ata ulimi ndipo wakampa huduma ya kwanza kabla ya kumuwahisha Hospitali ya Masana.
Patcho amesema Maluu alipopelekwa Masana walipompokea tu, wakaambiwa wamuwahishe Hospitali ya Lugalo kwa kuwa mgonjwa ameshafariki.
"Ni kweli Maluu Stonch amefariki akiwa anaimba jukwaani, alianguka chini na kuangukia uso hapo hapo damu zikawa zinamtoka masikioniwakati tunapambana kumsaidia apate matibabu ndipo tukaambiwa amefariki na kuhamishiwa Hospital ya Lugalo hivyo ikafanyika utaratibu wa kupelekwa chumba cha kuhifadhiwa maiti," amesema Patcho Mwamba.
Patcho ameendelea kusema, Maluu kwa mwezi mzima hakuwa sawa kiafya kwani alikuwa anaumwa na kupona hadi akampa likizo ya mwezi mzima ili ajisikilizie hali yake baada ya hapo akipona arudi kazin,i na Likizo ilipoisha akaanza kazi kama kawaida lakini bado alikuwa hajakaa sawa kiafya.
"Baada ya kumuona hali yake kiafya sio nzuri sana, nilimpa likizo ya mwezi mmoja ajiangalie afya yake na akipona arudi kazini, baada ya hapo kweli alirudi kazini lakini bado hakuwa amekaa sawa kiafya kwani alikuwa mtu wa mawazo muda mwingi, hasira wakati mwingine lakini tulikuwa tunaenda naye sawa hivyo hivyo hadi kufariki jana Jumamosi," amesema Patcho.
Patcho amesema Maluu alikuwa anaishi Salasala jijini Dar es Salam kuhusu msiba na mazishi yatakuwa wapi watatoa taarifa hadi hapo mchana watakapokaa kikao na mke wa marehemu.
Maluu enzi za uhai wake aliwahi kufanya kazi bendi nyingi zikiwemo Stono Musica, Stono Mayasika na nyingine nyingi.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi
Leave a Reply