Mwanafunzi kidato cha tatu ajinyonga

Mwanafunzi kidato cha tatu ajinyonga

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lumbira iliyopo Kata ya Luanda Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Jafari Mwashitete (16) amekutwa amefariki shuleni akidaiwa kujinyoga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe ACP Theopista Mallya amethibitisha kutokea kwa tukio la kujinyonga kwa mwanafunzi huyo.

ACP Mallya amedai kuwa walipokea taarifa ya kujinyonga kwa mwanafunzi huyo jana Jumatatu Julai 3, 2023 saa 10 jioni na kwamba ilikutwa karatasi mfukoni kwa mtoto huyo yenye ujumbe unaoeleza kutokutaka kusoma shule ya Lumbira badala yake anataka kusoma katika shule ya Myovizi.

“Ujumbe huo unaeleza kwamba marehemu alitaka kusoma Myovizi lakini wazazi wake walimhamisha na kumpeleka Shule ya Sekondari Lumbila jambo ambalo hakulitaka” amesema Mallya.

Aidha ametoa wito kwa wazazi kuwa wanapaswa kuwasikiliza watoto wao na kujua mawazo yao ili kuepusha matukio ya aina hiyo. Mwenyekiti wa Kijiji cha Lumbira, Kawawa Mwashilindi amesema alipata taarifa za tukio na kuwa mwanafunzi huyo alijinyonga katika jengo la maabara lililopo shuleni hapo.

Amesema Jafari alikuwa akisoma kidato cha tatu ambapo alihamia shuleni hapo akitokea Shule ya Sekondari Myovizi na kwamba mpaka umauti unamkuta alikuwa eneo la shule akiwa amevaa sare za shule.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags