Mlo ulio bora kwa mtoto

Mlo ulio bora kwa mtoto

Huwa ni furaha kubwa katika familia mtoto anapozaliwa, na hata katika tamaduni fulani fulani sherehe kubwa hufanyika kumkaribisha mwanafamilia mpya aliyezaliwa.

Lakini pamoja na familia kuwa katika hali ya furaha, wazazi wa mtoto aliyezaliwa huwa na maswali mengi ya kujiuliza. Tutamleaje mtoto ili awe mwanajamii mwenye tabia njema?

Lishe ya mtoto wetu iweje ili akue akiwa mwenye afya njema ya mwili na akili? Tutamwepushaje mwanetu na maradhi haya yanayotishia maisha ya watoto?

Katika hali ya kutafuta majibu ya maswali haya, wazazi hujikuta katika kila aina ya sintofahamu kutokana na ushauri mbalimbali waupatao kuhusu lishe au malezi ya watoto wao.

Sayansi ya afya inatoa ushauri ambao utasaidia wazazi wapya kuwa na mwanzo mzuri wa lishe ya mtoto ili akue akiwa na afya njema. Katika maisha, jinsi vile tunavyoanza, yaweza kutabiri jinsi vile tutakavyomaliza.

Hii inaamaanisha kuwa lishe bora kwa mtoto katika nyakati zake za mwanzo wa maisha yake, ni muhimu sana kwa afya ya baadae katika maisha yake.

Tafiti zinaonyesha kuwa, lishe bora kwa binadamu katika utoto wake, huchangia sana kuwa na maisha mazuri baadae, kufanya vizuri shuleni, kazini na hata jinsi anavyoweza kushirikiana na jamii inayomzunguka.

Pia aina bora ya vyakula tutakavyokula tukiwa wachanga, vitatusaidia baadae maishani kuwa na miili yenye nguvu na afya, kinga ya mwili iliyo imara na kuwa na umri mrefu wa kuishi.

Chakula muhimu sana kwa mtoto mchanga katika miezi sita ya mwanzo ya maisha yake ni maziwa ya mama.

Maziwa ya mama ni yenye lishe ya hali ya juu, yenye mchanganyiko maalum wa virutubisho na kinga kutoka kwa mama kwa ajili ya mtoto.

Vitu muhimu vilivyomo katika maziwa haya ni kinga ya mwili(antibodies), vijidawa (antimicrobial factors), vimeng’enyo, vitamini, madini muhimu, mafuta na protini (vyote hivi husaidia ukuaji wa haraka wa mwili na ubongo wa mtoto).

Watoto huanzishiwa lishe ya vyakula vingine wanapokua na umri wa angalau miezi 4 hadi 6, kwa kuwa watoto wachanga huwa hawawezi kumeng’enya aina nyingi za vyakula.

Kwa kawaida watoto huanzishiwa vyakula hivi pale uzito wao wa mwili unakuwa mara mbili ya uzito waliozaliwa nao, na hii ni endapo wanaweza kukaa, shingo imekuwa na nguvu, wanaweza kufungua mdomo wanapopewa chakula na wanaweza kumeza vyakula laini, mara nyingi huweza kufanya hayo yote wakiwa na miezi sita.

Vyakula hivi wanavyoanzishiwa watoto huwa ni nyongeza ya maziwa ya mama na siyo mbadala wa maziwa ya mama.

Chakula cha mwanzo cha mtoto ni lazima kiwe cha maji maji na laini.Pata msaada wa kujua ni wakati gani hasa wa kumuanzishia mtoto vyakula, wasiliana na wataalamu au wauguzi katika cliniki mtoto anayoudumiwa.

Usimwanzishie mtoto aina nyingi za vyakula kwa wakati mmoja ila umwanzishie chakula kimoja hadi kingine kwa nyakati tofauti na uchunguze endapo kama kuna chakula chenye kumletea mtoto aleji.

Usimwanzishie mtoto vyakula kama mayai, asali, karanga au siagi ya karanga na aina nyinginezo na nati kwa sababu vyakula hivi ni rahisi kusababisha aleji, asali yaweza kuwa na vijimelea vya bakteria vilivyolala( kwa kitaalam hujulikana kama endospores) ambavyo vinaweza kusababisha maambukizi kwa watoto wachanga kwa kuwa kinga yao ya mwili bado haijaimarika.

Tunapowaanzishia vyakula watoto wachanga, lazima tufuate mtiririko ufuatao; hatua ya kwanza ni kuanza na vyakula vya nafaka kama uji wa mchele au mahindi. Vyakula hivi huendana na mwili wa mtoto na ni nadra sana mtoto kuwa na aleji ya vyakula hivi.

Hatua ya pili ni kumuanzishia mtoto vyakula vya mboga mboga.Vyakula hivi huwa na virutubisho vingi zaidi ya matunda yenye sukari nyingi.

Vyakula hivi vya mboga mboga ni kama viazi vitamu, bitiruti,maboga na karoti ambavyo ni rahisi kupika na kuviponda ponda kutengeneza chakula laini cha mtoto.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags