Mkuu wa Wilaya Ubungo aagiza kuondolewa kwa Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi NIT

Mkuu wa Wilaya Ubungo aagiza kuondolewa kwa Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi NIT

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kheri James ameagiza kuodolewa kwa Mkuu wa Kitengo cha ulinzi wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SumaJKT), katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

James ameagiza kuondolewa kwa mkuu huyo kufuatia kusambaa kwa video mbili mitandaoni vikionesha askari wa SumaJKT wanaosimamia masuala ya ulinzi na usalama NIT, wakipigana na mwanafunzi pamoja na mtoa huduma ya chakula chuoni hapo kitendo ambacho amedai ni udhalilishaji.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam  wakati wa kikao kilichokuwa kikijadili video hizo za udhalilishaji wa wanafunzi uliyofanywa na askari hao wa SumaJKT.

Amesema pamoja na uongozi wa SumaJKT kuwachukulia hatua za kinidhamu askari waliohusika na vitendo hivyo pia anaagiza kuondolewa pia kwa Mkuu wa Kitendo hicho chuoni hapo.

“Wamuondoe huyo mkuu wa kitengo ambaye alikuwa akisimamia ulinzi wa chuo, nataka aondoke na yeye kama walivyoondolewa askari wale wengine waliofanya makosa, aletwe mkuu mpya na askari wengine wapya ili wasimamie makubaliano ambayo yamewekwa sasa,”amesema

Amesema Suma JKT kwa kipindi hiki ambacho bado wameaminiwa kuwa walinzi wa chuo hicho, ni lazima wahakikishe askari wanaowaleta hapo ni wale wenye weledi, wanayoyaishi maadili ya ulinzi lakini wanaoheshimu utu wa mtu na taratibu zilizowekwa katika taasisi ya umma.

“Endapo likatokea tukio lingine katika eneo hili  na ikabainika limesababishwa na askari, tutakielekeza chuo hiki kifanye mbadala wa mkataba na chombo kingine cha ulinzi,” amesema

Awali akifafanua matukio yaliyotokea chuoni hapo, James amesema mara baada ya kufika NIT, walibaini kuwa ni kweli matukio yaliyosambaa mitandaoni yalifanyika ambapo tukio la kwanza ni la mwanafunzi ambaye alizuiliwa kuingia chuoni kwa sababu hakuwa na kitambulisho.

“Na huo ndio utaratibu wa chuo hiki kuwa mtu asiyekuwa na kitambulisho haruhusiwi kuingia kwa sababu za kiusalama walizojiwekea hivyo mvutano uliyotokea baina yake na askari ulitokana na mwanafunzi huyo kukaidi amri ya kutokuingia bila kuwa na kitambuliko,” amesema

Amesema katika tukio la pili lilikuwa ni baina ya askari wa Suma JKT na mwanamama anayefanya kazi ya kutoa huduma ya chakula chuoni hapo ambapo alizuiliwa kwa sababu alikuja muda ambao sio wa kazi na alivaa mavazi ambayo yanazuiliwa hapo chuoni.

“Kwahiyo katika Kuzuiliwa kwake akaingia kwenye mvutano mkubwa na askari na picha yake ikasambaa katika mitandao ya kijamii, pamoja na kwamba askari walikuwa wakitekeleza majukumu yao namna ambayo walidili na watu hao wawili  haikubaliki…

“Sisi kama kamati ya ulinzi na usalama tunakemea vitendo hivyo na kuwaelekeza Suma JKT kwamba pamoja wamechukua hatua kwa askari waliofanya kitendo hicho, iwe mwanzo na mwisho kwenye taasisi za elimu na nyingine askari kuchukua jukumu la kupambana na mwananchi katika eneo ambalo anaweza kumdhibiti bila kutumia nguvu kubwa,” amesema

Hata hivyo amesema jambo lingine ambalo wamelibaini ni wanafunzi kupata shida ya kuingia chuoni kwa sababu ya kitu kinachoitwa muongozo wa mavazi.

“Muongozo huo unawataka wavae soski na nguo zingine za heshima, sasa tumezungumza na chuo kwamba upo mwongozo wa wizara unaotumika vyuo vyote, vipo baadhi ya vitu tumeona sio vya muhimu sana kwa mfano kipengele cha kuvaa soski tumeelekeza kuwa kisitumike kumzuia mtu asiingie darasani…

“Tumebaini pia askari hawana uelewa wa kutosha kwamba ni lipi vazi linalofaha mtu kuingia nalo chuoni na lipi siyo, tumekielekeza chuo kwamba kama mtu amevaa nadhifu na anamuonekano wa kinadhifu soski kisiwe ni kigezo cha yeye kutokingia darasani,” amesema.

Kwa upande wake Rais wa Serikali ya Wanafunzi NIT, Jeremiah Stephen amesema wanatoa shukrani kwa Mkuu wa Wilaya kufika katika chuo hicho baada ya changamoto hiyo kujitokeza na kutoa maagizo kwa lengo la wanafunzi kuwa katika hali ya usalama.

“Niwahakikishie kwamba wanafunzi wapo katika hali ya usalama na tukio hilo limeshatatuliwa na kwa sasa vijana wanaendelea vema na mitihani yao,” amesema

Naye Rais wa Shirikisho la Serikali za Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya juu nchini (TAHLISO) Frank Nkinda amesema video hizo zilizua taharuki kwa wazazi na watanzania kwa ujumla lakini kupitia kikao cha leo wamejua kilichosababisha na hatua tayari zimeshachukuliwa.

 

 

 

 

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags