Mfumo wa kukata tiketi za mabasi ya abiria kwa njia ya mtandao wazinduliwa

Mfumo wa kukata tiketi za mabasi ya abiria kwa njia ya mtandao wazinduliwa

Watanzania hasa wale wanaotumia usafiri wa mabasi ya abiria wametakiwa kununua tikiti za mabasi hayo ya nchi kavu mtandaoni, kupitia mfumo wa Ticket Rafiki uliyozinduliwa jana.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Light, Raymond Magambo alisema mfumo huo umekuwa ukipigwa vita na mawakala wanaodhani wanakwenda kuchukuliwa kazi zao lakini jambo hilo si kweli kwani watakwenda kufanya kazi pamoja.

Alisema mfumo huo utaenda kuboresha kiwango cha utoaji huduma katika sekta ya usafirishaji wa abiria kwa njia ya mabasi kwa kuwezesha kuwa na njia rahisi, salama na yenye uhakika kwa watoa huduma kufanya shughuli zao kirahisi.

Hata hivyo alisema mchakato wa kuja na maombi hayo uliwachukua miaka sita kutokana na baadhi ya mambo ya kiufundi kutokamilika kwa wakati.

"Dunia sasa inafanya kazi kwa kutumia teknolojia ya kidijitali, halikadhalika, mabasi ya abiria yaendane na mabadiliko ya teknolojia kwa kufanya kazi kidijitali," alisema.

Alisema mchakato huo ulianza mwaka 2015, walilazimika kukamilisha baadhi ya mambo ya kiufundi ya Serikali kwa kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu zitakazohakikisha mfumo utakapoanza, Serikali itaweza kupata mapato yake.

 Alibainisha kuwa tatizo jingine ni changamoto za mfumo wa kuhakikisha wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani wanapata fedha zao kupitia teknolojia hiyo bila matatizo yoyote.

"Baada ya kukamilisha mchakato huo, mfumo utakuwa wazi zaidi ambapo wamiliki wa serikali na mabasi watapata mapato yao" alisema.

Kwa mujibu wake, alisema abiria wataweza kununua tiketi zao kupitia tovuti (online), simu na sehemu ya mauzo kwa wateja wanaonunua tiketi kupitia mawakala.

“Kupitia mfumo huu mtu anaweza kupata huduma ya Tiketi yake akiwa nyumbani wakati wowote iwe usiku au mchana pia Wakala  anaweza kupata  stahiki yake  bila shida yoyote na hata wenye mabasi wanaweza kupata sehemu yao pasipo kupoteza mapato kama ilivyo hivi sasa.

“Mfumo huu hasa upo katika sehemu kuu tatu, kuna Website itakayo muwezesha mtu kukata Tiketi, kwenye APP ya simu  itakayo wezesha pia kukata Tiketi na njia nyingine ni kuwaona mawakala watakuwa na shine maalumu (POS) njia hii wanaweza kutumia ambao hawana simu,” alisema.

Naye Ofisa Usimamizi wa Kodi ya Kanuni za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Munish Evarest, kwa niaba ya Kamishna wa Mapato ya Ndani alisema TRA inasubiri ripoti za mauzo mwishoni mwa mwaka kwa ajili ya kodi.

"Tutakuwa tukifanya kazi pamoja na kampuni ili kuhakikisha mapato ya serikali yanakusanywa," alisema

Wakati huo huo, Ndamba Trans, Mkurugenzi wa mabasi ya Ndamba Trans inayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam hadi Lindi, Musa Ngambo alisema wamiliki wa mabasi wapo tayari kuunganishwa na mfumo huo.

“Tunaamini mfumo huo utafanya miamala yote kuwa ya uwazi na kuwawezesha wamiliki wa Mabasi kupata ‘malipo yao halisi,” alisema.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags