MFAHAMU NELSON MANDELA BABA WA DEMOKRASIA AFRIKA

MFAHAMU NELSON MANDELA BABA WA DEMOKRASIA AFRIKA

Mpendwa msomaji wetu leo katika listi tumekusogezea kwa uchache historia ya Nelson Mandela ambaye ni moja kati ya wapigania uhuru nguli wanaopendwa Afrika.

Mwanasiasa huyu aliyekuwa machachari alitumikia kifungo cha miaka 27 jela, na baadaye kuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika ya kusini. Alisaidia kuiongoza nchi yake, kutoka kwenye siasa za ubaguzi wa rangi kuwa za kidemokrasia.

Mandela alizaliwa katika eneo la milimani la Transkei, nchini Afrika Kusini mwaka 1918.

Alikwenda kusomea sheria katika Chuo Kikuu cha Fort Hare nchini humo. Mwaka 1944, alijiunga na chama cha siasa cha African National Congress, kilichoundwa kwa lengo la kukabiliana na sera za ubaguzi wa rangi za serikali ya wachache ya nchini Afrika Kusini iliyoongozwa na watu weupe.

Na baadaye, mfumo huu ukabadilika na kuwa mapambano ya muda mrefu dhidi ya ubaguzi yaliyoongozwa na Mandela. Alikuwa rais wa kwanza wa Afrika Kusini, baada ya kukomeshwa kwa utawala wa kibaguzi, na alistaafu baada ya miaka mitano.

Hata hivyo Mandela alifariki Desemba 5, 2013, akiwa na miaka 95.

Atakumbukwa kwa hili

Nelson Mandela aliunda tawi la kijeshi ndani ya ANC lililojulikana kama "Umkhonto we Sizwe" au "Mkuki wa taifa" ili kukabiliana na serikali iliyoko mamlakani na sera zao za ubaguzi wa rangi. Alishitakiwa kwa hujuma na kupanga njama za kuipindua serikali mnamo mwaka 1964, na ndipo alipofungwa kifungo cha maisha katika gereza lililopo kwenye kisiwa cha Robben, ambako alitumikia kifungo kwa miaka 27. Baada ya kuachiwa mwaka 1990, Mandela alikuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, mwaka 1994.

Mandela alikivutia kizazi cha Afrika Kusini kwa kuwa ingawa alikuwa kifungoni kwa muda mrefu, utu wake na mtizamo wake juu ya ulimwengu ulipenya hadi nje ya kuta za gereza.

Miongo kadhaa aliyotumikia kifungo haikumvunja nguvu, bali ilimjengea mchango wake wa kihistoria katika mapambano ya kusaka uhuru wa taifa hilo. Baadhi ya nyimbo za kupinga ubaguzi wa rangi zilitoa mwito wa kuachiwa huru kwa Nelson Mandela, na miongoni mwa nyimbo hizo ni ule wa Johnny Clegg na Savuka ulioitwa, "Asimbonanga" ukiwa na maana "Hatujamuona".

Nelson Mandela anaheshimika kwa lipi?

Licha ya miaka kadhaa ya ugumu na kifungo, Mandela hakuwahi kupoteza maono yake kuhusu amani, jamii iliyo na usawa nchini Afrika Kusini na nafasi yake katika kulitumikia taifa lake.

Aliamini katika taifa la kidemokrasia, ambalo kila raia anakuwa na haki ya kupiga kura. Aliiongoza Afrika Kusini kwa awamu moja, na kufungua njia kwa raia kushiriki haki ya kidemokrasia ya kuchagua kiongozi atakayefuata, kuliongoza taifa hilo.

Alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobeli mwaka 1993, pamoja na rais wa zamani wa taifa hilo, F.W. de Klerk. De Klerk, awali aliondoa zuio la chama cha ANC na kumuachia huru Nelson Mandela kutoka kifungoni. kwa pamoja walishirikiana kuliondoa taifa hilo kutoka katika utawala wa kibaguzi.


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post