Melissa, Mbunifu Bora Chipukizi aliyetikisa  2024

Melissa, Mbunifu Bora Chipukizi aliyetikisa 2024

Fashion na mitindo ni miongoni mwa tasnia pendwa ulimwenguni, ingawa katika baadhi ya maeneo bado haijapewa kipaumbele. Licha ya hayo haijawa sababu ya tasnia hiyo kuacha kuzalisha wabunifu wapya kila kukicha.

Melissa George binti mwenye umri wa miaka 23 na Muhitimu wa Chuo cha Fedisa Fashion School kilichopo Cape Town, South Afrika ni mmoja kati ya wabunifu wa mavazi wa kike ambao wanachipukia kwa kasi nchini.

Licha ya kuwa baadhi ya wazazi katika jamii za Kiafrika hupata ugumu kuwaruhusu watoto wao kuingia kwenye masuala ya sanaa hilo lilikuwa tofauti kwa baba wa binti huyo kwani aliamini uwezo wa binti.

"Nilipomwambia mzazi wangu nataka kusomea fashion alipokea vizuri na alikubali japo ni kweli wazazi wengi wa Kitanzania wanategemea mtoto aje kuwa Daktari au Mwanasheria lakini kwangu ilikuwa tofauti sikupangiwa.
"Nafikiri Watanzania inabidi tufunguke kifikra na tukaribishe kila kitu kinachokuja upande wetu, sio lazima kila mtu asome udaktari au ukandarasi kuna vitu vingi unaweza kusomea na kukuongoza tusijiwekee mipaka," amesema Melissa.

Hali ya Melissa kupenda fashion na kuipambania imeendelea kukomazwa na baadhi ya watu ambao wamemtangulia kwenye tasnia hiyo.
"Kwa Tanzania namtazama sana Anjali Borkhataria ambaye brand yake ni Elantik ananivutia zaidi japo kwenye tasnia ameanza 2019. Kimataifa navutiwa sana na Pharrel Willium ambaye ni Create Director wa Loui Vuitton, hao ni kati ya watu najifunza zaidi kutoka kwao," amesema Melissa.
Mwaka 2024 umeweka historia kwa Melissa

Tunaweza kusema mwaka 2024 umemalizika vyema kwa mbunifu huyo kwani Desemba 7 alifanikiwa kunyanyuka kidedea katika Tuzo za Swahili Fashion kama Mbunifu Bora Chipukizi wa Mavazi 2024.

"Ilikuwa mwezi June nikatuma maombi kwenye kipengele cha Mbunifu Bora Chipukizi wa Mavazi kwahiyo nikawapa kazi zangu ambazo nimewahi kufanya, baada ya hapo tukaitwa kwa ajili ya kuchujwa na kushona ndiyo ikaja ugawaji wa tuzo," amesema Melissa.
Inawezekana ubora wa kazi zake katika ubunifu hutokana na umakini ambao amekuwa akiuweka wakati wa kubuni mavazi kwani kabla ya kufanya hivyo hujikita kwenye utafiti .

"Lazima nifanye utafiti kwanza kuangalia rangi gani zinazofanya vizuri kwa mwaka husika. Japo sio lazima kwa hiyo research zangu mara nyingi naenda kwanza WGSN, VORGE au Pinterest baada ya hapo naanza ubunifu ambao huwa unatumia zaidi ya wiki moja mpaka mbili," amesema Melissa.

Aidha aliongezea kwa kusema mavazi yaliyofanya aondoke na tuzo ya Swahili Fashion alitumia wiki tatu kukamilisha.
"Sasa tukiongelea Fashion Tanzania tumezoea vitu vilevile utakuta ni magauni ya harusi lakini mimi napendelea zaidi kubuni mavazi ya mtaani, ndiyo maana utakuta kuna kofia lakini pia nguo zangu mara nyingi zinakuwa na michoro kwa sababu napenda sana kuchora, " amesema Melissa.
Akizungumzia mapenzi yake kwenye uchoraji amesema mbunifu wa mavazi ni muhimu kujua kuchora kwani itamsaidia katika kazi.

Kwanini wanamitindo wengi hupanda jukwaani wakiwa wamenyoa?
“Inategemea mbunifu unataka watu wazingatie nini zaidi, lakini kwa upande wangu nilichagua model ambaye hana nywele ili watazamaji waangalie nguo zaidi maana mtu akiwa na nywele watu wanaweza wasizingatie nguo, wazingatie nywele mimi sikutaka hivyo na lengo langu kubwa nilitaka waangalie ile michoro zaidi," amesema Melissa.

Kila safari yenye mafanikio haikosi changamoto licha ya watu wengi kuchukulia tasnia ya mitindo kama kitu chepesi Melissa amesema kuna changamoto ambazo.

"Watu wanafikiri kushona nguo ni kitu rahisi au kubuni nguo ni rahisi, kushona mpaka kitu kitokee kabisa watu wakipende sio kitu rahisi na kwa kuwa sijaanza kuingia kwenye biashara ya mitindo zaidi lakini zikija naweza kabiliana nazo,"amesema Melissa.
Wanasema mvumilivu hula mbivu na hicho ndicho kilitokea kwa Melissa baada ya kutuma maombi ya kazi kwenye kampuni mbalimbali bila kupata mafanikio.

"Nilikuwa natamani kuajiriwa na kampuni moja wapo ya mavazi mwanzoni mwa mwaka huu nilituma maombi kwenye zaidi ya kampuni 50 lakini hakuna hata moja ilitaka kufanya kazi na mimi nilikata tamaa ila ndio nikapata akili ya kuanzisha kitu changu mwenyewe na najiamini zaidi kwenye harakati nazofanya," amesema Melissa.

Mbunifu huyu ameiambia Mwananchi Scoop ana matamanio ya kufika mbali, 2025 anategemea kuwa na kampuni ya mavazi ikiwa na jina linalotambulika
Aidha ameshauri vijana kupambania ndoto zao kwani kukatishwa tamaa ni jambo ambalo lipo hata yeye aliambiwa hatofika mbali.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags