Mc Pilipili: Ageukia Uchungaji, Kusaidia Watu Wasiojiweza

Mc Pilipili: Ageukia Uchungaji, Kusaidia Watu Wasiojiweza

MC Pilipili si jina geni masikioni mwa watu hasa wanafunzi wa vyuo. Ni wazi kuwa wengi wenu mmekuwa mkimfuatilia na kumsikiliza.

Kwa jina halisi aliyopewa na wazazi wake Mc Pilipili anaitwa Emmanuel Mathias kijana huyo mwenye uso wa uchekeshaji kama kazi yake ilivyo, alizaliwa mtaa wa Airport Dodoma.

Akipiga story na MwannachiScoop, Mc Pilipili anafunguka na kusema kwa sasa anawaletea wananchi Pilipili mwingine ambaye ni mtumishi wa Mungu, Mchungaji na mtu anayependa kuisaidia jamii iliyokumbwa na matatizo mbalimbali.

Alisema kifo cha mama yake mzazi Mariam Matebe ndicho kilisababisha kuibuka kwa Mc Pilipili mpya ambaye ni mtumishi wa Mungu, aliyeokoka na anayesaidia watu wasiojiweza.

“Zamani nilikuwa nikihubiri na baada ya kifo cha mama yangu hali ilizidi ndani ya moyo wangu, kila nilipomkumbuka mama nilimtendea wema mtu mwenye uhitaji niliyekutana naye njiani.

“Yote ninayoyafanya ikiwemo ya kusaidia jamii isiyojiweza ninafanya kwa sifa na utukufu wa Mungu hivyo sihitaji kujibrand katika kazi yangu hii nyingine ambayo Mungu amependa niifanye,” alisema

Asisitiza hawezi kuacha uchekeshaji

Hata hivyo Mc Pilipili alisema pamoja na sasa kuwa mchungaji lakini kamwe hawezi kuacha uchekeshaji kwani jambo hilo kwake si kazi tu bali ni maisha yake.

“Sasa hivi tutafanya Gospel and Comedy ni uchekeshaji ambao hauna matusi bali uelimisha zaidi hivyo mashabaki zangu wasubiri mambo matamu na mazuri yanakuja,” alisema

Aidha alisisitiza kuwa yeye bado anaendelea na Standup Comedy na amekuwa akiwafundisha vijana wengi namna ya kufanya kazi hiyo ili kukubalika katika jamii.

“Mimi ninaendelea kuwa kama Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ambaye maneno yake na vitu alivyovifanya vinaishi mpaka leo na wengi wanatamani kuwa kama yeye.

“Hivyo nami naamini kuwa kazi zangu nilizowahi kufanya na ninazoendelea kufanya vitaishi na vijana wengine watapata fursa za kuziangalia na kujifunza,” alisema

Alisema vijana wengi wanaofanya vizuri sasa katika Standup comedy anawaona kama wanawe maana wengi wao amewafundisha na kuwajengea msingi ya ufanyaji kazi hiyo.

Mc Pilipili alisema katika suala la ushehereshaji pia anaendelea nalo na yeye ndio mc namba moja na Mc wa Taifa.

“Ndugu zangu mimi bado nipo ila kilichonisababisha nipokee hapa katikati, ni masuala ya corona, kufariki wa mama yangu na kifo cha Hayati John Magufuli.

“Wakati nimejipanga kuandaa shoo kubwa nikalipia kila kitu zimebaki kama wiki mbili corona ndo ikapamba moto na serikali ikazuia mikusanyiko, nikaacha nikajipanga upya nilipoanza maandalizi ya shoo nyingine na kukamilisha bado siku kadhaa mama yangu akafariki, heee tulipomaliza hayo nikaanza tena maandalizi ya shoo nyingine tumemaliza bado siku kadhaa tufanye Rais Magufuli anafariki,” alisema Mc Pilipili na kuongeza

“Nikasema hiki ni nini kinatokea basi nikaona bora nipumzike kidogo ndipo watu wakaona kama nimepotea lakini si kweli ni mambo kama hayo ndiyo yaliingiliana,” alisema

Mipango aliyonayo kwenye comedy

Alisema mpango aliyonayo sasa ni kufanya shoo kubwa ya Standaup Comedy hivyo amewataka mashabiki zake wakae mkao wa kula wakati ukifika.

“Tunayo mipango mingi lakini mmoja wapo ni kufanya shoo kubwa sana ya comedy na ninamini itafanikiwa kwa msaada wa Mungu, mashabiki zangu kaeni mkao wa kula mambo mazuri yanakuja,” alisema

Kuhusu biashara ya samaki

Mc Pilipili alisema anajipanga vizuri na hivi karibuni atarejea katika bishara yake hiyo ya samaki aliyodai ilifanya vema tangu alipoianzisha tofauti na matarajio yake.

“Biashara hii ya samaki ilituokoa sana kipindi cha Corona, kwani wakati ule hakuna harusi wala shoo za standup comedy, kupitia samaki maisha yaliendelea kama kawaida,” alisema

Changamoto

Alisema moja ya changamoto anayokumbana nayo ni baadhi ya watu kumwambia anafanya suala la kuisaidia jamii kimaslahi jambo ambalo amelipinga na kusema kuwa si kweli.

“Niwaambie tu watu wanaofanya kazi ya kuwasaidia wengine wenye uhitaji ni wachache sana, wala hakuna fedha ninayotarajia kupata katika hili bali nimeamua kusaidia wahitaji kwa kadiri Mungu atakavyonijalia,” alisema na kuongeza

“Tunafanya haya yote kwa sifa na utukufu wa Mungu, licha ya kukumbana na changamoto mbalimbali lakini tunasonga mbele,” alisema






Comments 2


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags