Matukio ya unyanyasaji yanavyochafua majina ya mastaa

Matukio ya unyanyasaji yanavyochafua majina ya mastaa

Ukiangalia kwa jicho la kawaida na kufikiria kwa haraka  unaweza kudhani ni miyeyusho ya mashabiki kutaka kupita na upepo wa mastaa kwa kuwabambikizia kesi za unyanyasaji wa kingono na kimwili kwa kudai walifanyiwa vitendo hivyo miaka mingi iliyopita.

Kutokana na madai ya namna hii wengi hushitushwa pindi tuhuma hizo zinapofika mbali na kuzaa matunda kama ilivyokuwa kwa mwanamuziki wa R&B na Hip-hop kutoka nchini Marekani Robert Sylvester Kelly maarufu kama  R. Kelly, kupigwa mvua (kifungo) ya miaka 31  gerezani baada ya kukutwa na hatia ya unyanyasaji wa kingono kwa wanawake na watoto

Licha ya kuwa washitaki walitoa maelezo ya kufanyiwa vitendo hivyo miaka mingi iliyopita, kama alivyodai Lisa Van Allen kuwa alifanyiwa unyanyasaji  mwaka 1998 na Kitti Jones kufanyiwa mwaka 2011 lakini sheria haikumuacha salama mkali huyo wa R&B na hadi sasa bado anaendelea kutumikia kifungo chake.

Kufufuka kwa kesi za namna hii, hazijaishia tu kwa R.Kelly  siku za hivi karibuni matukio mengi ya unyanyasaji wa kingoni yamekuwa yakiibuka na kuchafua majina ya baadhi ya watu maarufu.

Wiki chache zilizopita imetokea pia kwa mwanamuziki wa hip-hop kutoka nchini Marekani  P. Diddy baada ya kukabwa koo na zaidi  ya wanawake watatu wakidai amewahi kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji  akiwemo Joi Dickerson-Neal ambaye amedai kufanyiwa vitendo hivyo Januari 3, 1991 baada ya Diddy kumlewesha na kutimiza malengo yake .

Mbali na Diddy tuhuma nyingine kwa mwaka 2023 zimejitokeza kwa mwanamuziki wa hip-hop Lil Wayne siku chache zilizopita alijikuta akikalia kuti kavu baada ya mlinzi wake wa zamani Carlos Christian kumshitaki  kwa kumtishia kumpiga risasi na kumpiga ngumi ya sikio  akidai kufanyiwa hivyo Disemba 2021

Kutokana na matukio haya kuibuka baada ya kutendeka kwa miaka mingi Joachim Marunda  (Master J ) akizungumza na gazeti hili la Mwananchi anasema matukio kama hayo yamekuwa yakiibuka sasa hivi huenda kutokana na makubaliano ya mtenda na mtendewa, kwani wapo baadhi ya watu ambao huingia mikataba ya kufichiana siri hata wakifanyiwa unyanyasaji.

“Wanajitokeza sasa hivi kwa sababu mwanzo walijitokeza wakatulizwa  kwa kupewa pesa wenzetu wana kitu kinaitwa non disclosure agreement ni mkataba wa kisheria wa kutozungumzia chochote kwa hiyo ubaya wa mkataba huu huwa na mda wa kuisha”

“Wengine walikaa kimya baada ya kuona wenzao wanaongea na wao sasa wanaanza kuongea lakini walio wengi wanakuwa wanalipwa kutosema kitu hivyo basi mikataba yao inakuwa imeisha ndiyo maana wanaongea kwa sababu ukisaini mkataba hutakiwi kuongea na ukifaya hivyo unakuwa umeingia kwenye matatizo ya kisheria”. Anasema Master J

Master anasema jambo hilo si nje tu hata Tanzania lipo baadhi ya wasanii wamekuwa wakiwafayia vitendo vya kingono  wanawake na kisha kuwalipa kwa mikataba ya kutozungumza kitu juu ya walichofanya.

“Hivyo vitu vipo hadi kwetu naomba Mungu isije ikafunguka ya bongo ni mbaya yaani bora ya nje kulipo hapa Tanzania, kwanza hapa bongo watoto wa kike waliopo kwenye industry wanateseka sana naamini kuna siku wataongea ”. Anasema Master

Aidha kwa upande wake mwanamuziki Mwasiti Almas anasema watoto wengi wa kike wananyanyasika lakini hawana sehemu ya kusemea  hivyo siku wakipata sehemu ndiyo hufunguka na kutokea kama yaliyowakuta P Diddy na R. Kelly

“Inawezekana wapo watu walionyanyasika lakini walikuwa hawana pakusemea,  kama Tanzania wapo watu maarufu wengi wananyanyasika kingono wanakosa pakusemea wakiona mwegine wanaongea nao wanaona bora waongee na ndiyo maana nikaanzisha Kipepeo Mweusi ili watoto wa kike wapate  pakusemea”.

“Mfano kesi ya R.Kelly wengi walijitokeza yaani walikuwa kama wamefunguliwa baada ya kuona wenzao wanazungumza wakaona kumbe na wao wanaweza kusikilizwa kwa hiyo kwa mtu kama Diddy wapo walioogopa umshitaki mwanzo kwa kujiona ni wadogo lakini walisahau kuwa kuna haki za binadamu”. Anasema Mwasiti

Mwasiti anasema hata katika Taasisi yake ya Kipepeo Mweusi tayari wamepokea kesi nyingi sana za unyanyasaji wa kingono, watu wengi wamekuwa wakitoa rushwa ya ngono wakihisi wanafanyiwa upendeleo bila ya kufahamu kuwa inakuwa ubakwaji.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags