Matukio ya kupotea waandishi wa habari, Yalivyozima ndoto ya mwigizaji John

Matukio ya kupotea waandishi wa habari, Yalivyozima ndoto ya mwigizaji John

Na Aisha Charles

Wakizungumziwa waigizaji wa Bongo movie wanaokosha mashabiki kwa kuvaa uhusika kwenye kazi zao za uigizaji ni ngumu kuliacha jina la John Elisha maarufu kama Hamadi aliyejizoelea umaarufu katika tamthilia ya Kombolela.

Kwa uhalisia John ni mzaliwa wa Mwanza, elimu yake ya msingi alipata mwaka 2000 katika shule ya Gedeli na mwaka 2013 alimaliza elimu ya O level katika shule ya Munanila,  Kigoma.

Akizungumza na Mwananchi Scoop,  amesema  alikuwa na ndoto ya kuwa mtangazaji mkubwa ambaye angeweza kutambulika ndani na nje ya Tanzania, lakini ndoto hiyo ilikatika baada ya familia yake kuingiwa na hofu ya kumpoteza, kutokana na matukio ya kupotea kwa waandishi wa habari yaliyokuwa yakitikisa kwa kipindi hicho.

 

“Ndoto yangu ilikuwa niwe mwandishi mkubwa lakini  haikuwezekana kutokana na kipindi ambacho mimi nilikuwa nataka kusomea hiyo fani kulikuwa na matukio mengi ya waandishi wa habari kupotea, familia yangu iliingiwa hofu” amesema John.

Baada ya kushindwa kutembelea ndoto zake mwaka 2013 alijiunga na chuo cha Butimba TTC kusomea ualimu amesema alifanya hivyo kwa sababu ya kutowaangusha wazazi wake.

Licha ya kujiunga na chuo baada ya ndoto yake ya kwanza kukatika,  alikuwa na ndoto nyingine ya kuwa mwanasoka hata hivyo nayo ilizimika baada ya kuvunjika mguu akiwa mwaka wa pili chuo, ndipo alipopata rafiki akiwa Mbeya, ambaye alimshauri kuingia katika sanaa ya uigizaji.

“Pia nilikuwa na ndoto ya kucheza mpira nije kuwa mwanasoka mkubwa hapa Tanzania lakini zilizimika nilipovunjika mguu nikiwa uwanjani.

Hata hivyo tulivyokuwa chuoni kuna rafiki yangu kutoka Mbeya ndiye alinishawishi kuingia katika uigizaji kwa sababu yeye alikuwa anajihusisha na masuala ya sanaa basi aliniambia naweza kufanya hivyo” amesema John.

Hivyo basi alianza sanaa kwa ushawishi wa rafiki yake, wakiwa chuo walitoa filamu iliyoitwa ‘The Idea’ hapo ndipo safari yake ya ugizaji ikaanza.

John ameeleza kuwa mama yake ndiye mtu wa kwanza kumuunga mkono kwa sababu baba hakuamini alichokuwa anafanya

“Mama yangu alikuwa mtu wa kwanza kukubali ninachokifanya ila baba kwa kuwa ni mchungaji hakuweza kuamini kwa haraka kwa sababu alihisi ninaweza kumchafua yeye kutokana na sanaa yangu.

Ila namshukuru Mungu baada ya kutoka tamthilia ya kombolela mwaka 2021 mpaka 2022 ndiyo baba akabariki rasmi kuniruhusu kufanya sanaa baada ya kuona nilichofanya kwenye tamthilia ”amesema John.

 Hata hivyo mwigizaji huyo ameeleza kuwa kuna kipindi akiwa katika sanaa aliwahi kukata tamaa na kuona sanaa ya uigizaji ni ngumu.

 

“Nakumbuka ilikuwa mwaka 2020 nilisimama kufanya sanaa kutokana na changamoto mbalimbali kwa bahati nzuri nilipata kazi katika kampuni ya Wachina nikapandishwa cheo ambacho kilinifanya nitoke Mwanza nije Dar es salaam, niliamini siwezi kufanya sanaa kwa kujitolea kwa sababu nina familia ambayo inanitegemea” amesema John.

 Amesema alipofika Dar es salaam alishindwa kujizuia kuendelea na sanaa baada ya kukutana na director Salum Dotto Majagi ambaye aliibua tena kipaji chake.

“ Namshukuru sana Director Majagi maana nilivyofika Dar nilishindwa kujizuia kuonesha kipaji changu ambacho yeye alikiona na hakusita kuniambia kwamba nisipoteze kitu nilichonacho safari yangu ya uigizaji ikaibuka tena hapo” Amesema John.

Aidha amezungumzia tasnia ya uigizaji ilivyoshika kasi kwani kila mwigizaji anatamani kuonesha alichonacho na ndiyo maana wapo wanaotoa tamthilia na filamu fupi.

“ Ni kweli wakati mwingine huwa tunafanya filamu za mtindo huo ili kuonesha kile ambacho tunacho ili atakaye vutiwa anaweza akakupa bajeti ya kazi na ukafanya kitu kikubwa zaidi” alisema John.

 

 

John ameoa na amebahatika kupata watoto wawili wa kike, ameeleza kuna muda inakuwa ngumu   kumuelewesha mke wake kuwa anachofanya ni maigizo hususani katika uhusika wa mapenzi katika filamu.

 

“Kuna muda inakuwa ngumu kumuelewesha mke wangu kuwa yale ni maigizo hususani ukipewa ‘sini’ ya kumkisi mtu kama mpenzi wako unaweza ukawa umemkisi juu ya lips lakini yule anayeenda kutazama asione hivyo basi unakuwa ugomvi ila mimi naamini itafika kipindi ataelewa” amesema mwigizaji huyo.

Kati ya kazi alizoonekana John ni kwenye Tamthilia ya Kombolela, Toboa Tobo, Jangwani, Monalisa, Giza na Nuru.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post