Mastaa waliokabidhi mikoba kwa watoto wao

Mastaa waliokabidhi mikoba kwa watoto wao

Waswahili wanasema vya kurithi vinazidi. Ni kawaida kuona watoto wakifuata nyayo za wazazi wao na kuendeleza urithi wa vipaji. Ingawa wapo baadhi ya wasanii ambao hawapendi kuona watoto wao wakifanya kazi ya sanaa kama wafanyavyo wao lakini inaonekana kuwa ni rahisi mtoto wa msanii kutengeneza jina kwa haraka na kupendwa na mashabiki kama ambavyo imetokea kwa baadhi yao.

Will Smith ni mmoja wa waigizaji maarufu duniani, ambaye alijizolea umaarufu kutoka kwenye kazi za sanaa, awali muziki na sasa uigizaji, kati ya kazi zake ni "Men in Black" na "The Pursuit of Happyness.


Ukubwa na uwezo wa Will inawezekana ikawa na mchango mkubwa kwa wanaye kwani wote wawili Jaden Smith na Willow Smith, nao wamedondokea katika tasnia ya sanaa na wamefanikiwa kwenye hilo kwa kiasi kikubwa. Jaden ni muigizaji na rapper, wakati Willow ni mwimbaji anayetamba na wimbo kama "Whip My Hair."

Demi Moore ni miongoni mwa waigizaji wakongwe wa Hollywood. Watoto wake, Rumer, Scout na Tallulah Willis, wote wamefuata nyayo za mama yao. Rumer alishinda Tuzo ya "Dancing with the Stars," na wamejizolea umaarufu kupitia kazi zao za sanaa kwenye muziki na filamu.



Lenny Kravitz
, mwanamuziki wa rock, naye ni baba wa mwigizaji maarufu Zoë Kravitz, ambaye ameonekana katika filamu kama "Big Little Lies" na "Mad Max: Fury Road," akionyesha uwezo wake wa kuigiza na kutunga nyimbo.


Billy Ray Cyrus
ni mwanamuziki maarufu ambaye pia aliigiza katika kipindi cha runinga cha "Hannah Montana." Aidha binti yake, aitwaye Miley Cyrus, amejizolea umaarufu kutokana na kazi ya maigizo na muziki wa pop.


Cindy Crawford
ni mwanamitindo maarufu ambaye binti yake anafahamika kama Kaia Gerber, ambaye pia amekuwa model na mwigizaji. Kaia anajulikana kwa mvuto wake na mafanikio yake katika tasnia ya mitindo.


Ron Howard
ni mwigizaji, mwongozaji na mzalishaji filamu maarufu, mtoto wake wa kike anaitwa Bryce Dallas Howard, naye amechukua mikoba ya baba yake pia ni mwigizaji, anayefahamika kwa kazi zake katika filamu za "Jurassic World" na "The Help."


Ethan Hawke
ni kati ya waigizaji wenye mafanikio, watoto wake ni Maya Hawke na Levon Hawke, wote wamefuata nyayo za baba yao. Kati ya filamu alizocheza Maya ni "Stranger Things" .

Mbali na hayo hata Tanzania pia wapo baadhi ya wanii waliofanikiwa kurithisha vipaji kwa watoto wao ikiwemo Natasha Mamvi ambaye ni mama wa mwigizaji Monalisa ambaye naye ana mtoto anayefahamika kwa jina la Sonia naye siku za hivi karibuni ameonekana akijikita kwenye sanaa ya muziki.


Pia mfano mzuri unaonekana kwa mwanamuziki mkongwe Zahir Zorro ambaye ni baba mzazi wa Banana Zorro na marehemu Maunda Zorro ambao wote ni waimbaji.

Hao ni baadhi, lakini wapo wengi waliochukua mikoba ya wazazi wao, hilo linatoa mfano wa jinsi talanta inavyoweza kuhamasishwa na mazingira ya familia. Na kupelekea Kila mmoja kuonesha uwezo wa kipekee, na kuendeleza urithi wa sanaa na kujipatia majina makubwa.

Watoto hao wanajenga historia yao katika tasnia na kuonyesha kwamba vipaji vya familia vinaweza kuendelea kwa vizazi vijavyo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post