Na Aisha Charles
Mambo vipi watu wangu wa nguvu kama kawaida tunaendelea kulisukuma gurudumu katika ulimwengu wa Fashion, siku zote ili uwe smart unatakiwa usipitwe na mitindo.
Na leo katika upande huu tutaangazia makosa ya uvaaji yanayoweza kuharibu mwonekano wako.
Hakuna mtu asiyependa kupendeza, hiyo ndiyo sababu inayopelekea watu kufanya mambo mbalimbali ili kupata mwonekano wa kuvutia wengine pamoja ana kusifiwa.
Katika mchakato wa kutafuta mwonekano huo classic baadhi ya watu hujikuta wamefanya makosa mbalimbali ambayo yanapelekea kuharibu ulichokipigilia mwilini
* Nguo za kubana
Nguo za kubana sana zinaweza kuunda mistari au vijitundu, zikisisitiza maeneo ambayo huenda yasionekane na mavazi yaliyowekwa vizuri zaidi, hii inaweza kupoteza uzuri wa nguo na shepu isiyo ya kawaida hasa kwa wale watu wanene nguo za kubana haziwafai hata kama vazi liwe zuri vipi haliwezi kuonekana.
Hata hivyo nguo za aina hiyo zinakufanya usiwe huru na haziwezi kuficha asili ya mwili na huongeza wingi wa kuonekana mwili pamoja na umbo.
* Kuvaa nguo zenye kukaba shingo
Nguo ambazo zina fika juu ya shingo na kubana, zinaweza kukufanya ukose mwonekano mzuri kwani mara nyingi nguo hizo humfanya mtu aonekane na shingo fupi.
Wakati wa kuchagua mavazi yako unatakiwa kuangalia haswa ni nguo gani huwa inakupendeza zaidi, wapo baadhi ya watu wakivaa nguo hizi wanapendeza na kuwapatia mwonekano mzuri, hivyo ukiona nguo yenye kubana shingo haikupendezi achana nayo tafuta vazi linguine litakalo kutoa zaidi.
* Kujaza cheni shingoni
Kuweka cheni au mkufu zaidi ya moja shingoni au kuvaa kitambaa kutakufanya upoteze mvuto machoni mwa watu, sawa ni mpenzi wa kuvaa mikufu na cheni ukivaa moja inatosha kabisa kufanya upendeze na kuwa nadhifu.
* Kujaza hereni masikioni
Mara nyingi wanawake wengi huona kama ni fashion nzuri kujaza hereni masikioni, bila kujua kuwa unapoteza muonekano kabisa kwa sababu urembo ukizidi sana unakuwa uchafu.
Kama waswahili wasemavyo kuwa tunakwenda na ushahidi basi na sisi tunakusogezea mtaalamu wa masuala ya urembo aitwaye Jackline George ameweka wazi kuwa moja ya kosa ambalo wadada wengi wanalifanya katika uvaaji wao ni kujaza 'Accessories' nyingi.
“Kuna msemo unasema too much is hamfully, msemo huu unatumika hata katika masuala ya mitindo, unapotaka kupata muonekano classic basi jiepushe na uvaaji wa accessories nyingi,"anasema Jackline.
Aidha aliongezea kwa kuwataka watu kuacha kuiga mitindo mbalimbali ambayo wanaiona katika mitandao ya kijamiii mfano kutoboa sikio zima kuvaa vipini vya aina tofauti kwani vinawaondolea muonekano na kupewa tafsiri mbaya katika jamii.
Hata hivyo hatukuishia hapo tukapata wasaha wa kuzungumza na mmoja wa mwanadada aitwaye Amina Salum mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam ambaye yeye anajihusisha na uuzaji wa accessories mbalimbali ambapo ameweka wazi kuwa wateja wanapokuja kununua bidhaa hizo huwa anawashauri ni accessories ipi itampendeza zaidi.
“Kwanza kabisa mimi sipendelei kuvaa accessories nyingi hivyo basi mteja wowote akija dukani kwangu huwa namshauri kwanza kabla ya kununua vitu anavyo vihitaji” amesema
Aidha aliongezea kwa kudai kuwa huwa anawashauri watu kutokana na baadhi ya wavaaji wa vito hivyo kutafsiriwa kama wahuni.
Wakati Amina akiwashauri wateja wake matumizi ya accessories ili kunogesha mwonekano wao, Mwanampenda Saidi wa Kiwalani yeye aliweka wazi kuwa hupendelea zaidi kuvaa urembo mwingi akiwa kwenye mitoko mbalimbali
“Yani bila kuvaa cheni zangu tatu ndefu na fupi bado sijatoka, sikio langu kujaza hereni na pete zangu zisizopungua nne najiona bado sijapendeza,”anasema.
Mambo ndiyo hayo sasa usiseme hatuja kwambia jambo baya katika Fashion ni kufanya makosa ya jinsi ya kujipangilia mwonekano wako na kufanya hivyo inakuwa ni dhambi ya fashion, na ili usionekane kituko basi fanya kufuata tips hizo.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi
Leave a Reply