Majaliwa atia neno danadana za Vazi la Taifa

Majaliwa atia neno danadana za Vazi la Taifa

Wakati danadana za kutafuta Vazi la Taifa zikiendelea, hatimaye suala hilo limefika kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye amemtaka Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Damas Ndumbaro kuhakikisha vazi hilo linapatikana.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo jana Machi 31, 2024 Dar es Salaam kwenye tamasha la Mtoko wa Pasaka amesema ambapo alionyesha kushangazwa na kuchelewa kupatikana kwa vazi hilo, licha ya ahadi kadhaa zilizowahi kutolewa tangu mwaka 2017.

“Nilipomuona MC Eliud alipokuja hapa huwa namuona kwenye kipindi la Cheka, ni mchekeshaji wetu maarufu lakini leo ametoa ujumbe kwa Serikali, ametutaka tuanze kubuni vazi la kitaifa, yeye amekuja alivyovaa, kavaa ameona hilo ndiyo vazi la kitaifa, nimemwambia Mheshimiwa Waziri ‘chalenji’ hiyo.

“Tulishafanya uamuzi toka mwaka 2017 kwa kuiagiza Wizara itafute Vazi la Taifa hili, na wakaahidi watatafuta katika kipindi kifupi. Toka 2017 hadi leo bado kipindi kifupi hicho? Eliud ametukumbusha tena kwamba tunahitaji kupata wazi la kitaifa, wanawake wavae vipi wanaume wavae vipi, kama umeshindwa kabisa basi tuchukue la Eliud, liwe vazi la kitaifa,” amesema Majaliwa.

Suala la kupatikana kwa Vazi la Taifa umekuwa ni mfupa mgumu. Mchakato wake ulianza mwaka 2004, na Desemba 22, 2011, kamati maalumu ya kutafuta vazi hilo iliteuliwa rasmi na Dk Emmanuel Nchimbi ambaye wakati huo ndiyo alikuwa waziri mwenye dhamana.
Kamati hiyo iliundwa na watu nane akiwemo mwenyekiti, Joseph Kusaga, katibu wake,
Angela Ngowi na wajumbe wakiwa ni Habib Gunze, Joice Mhaville, Mustafa Hassanali, Makwaia wa Kuhenga, Ndesambuka Merinyo na Absalom Kibanda ambaye baadaye alitangaza kukaa kando kwenye kamati hiyo.

Hata hivyo, mwaka 2012 baada ya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, kamati hiyo ikiongozwa na katibu wake, Ngowi akiwa na wajumbe Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali na Ndesambuka Merinyo, waliwasilisha ripoti ya vazi hilo kwa Waziri, Fenela Mukangara akiwa na Naibu wake, Amos Makalla.Kamati ilikabidhi michoro sita kutoka michoro 200 iliyowasilishwa na wasanii mbalimbali.

Kamati hiyo ya awali ilivunjwa na kuundwa mpya Julai 20, 2022 ikiwa chini ya mwenyekiti wake Profesa Hermas Mwansoko, katibu akiwa Dk Emmanuel Temu, na wajumbe; Chifu Sangali, Hadija Mwanamboka, Mustafa Hasanali, Mrisho Mpoto, na Masoud Ally (Kipanya).

Januari 31, 2023, mwanga wa kupatikana kwa vazi hilo ulianza kurudi tena kwa wananchi wanaosubiri kwa hamu, baada ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Dk Kedmond Mapana kusema Februari 3, 2023 wangekabidhi ripoti ya muundo wa vazi hilo kwa Serikali baada ya mchakato wa kulitafuta uliofanyika kwa miaka kadhaa.

Si hivyo tu, Februari 7, 2024, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma wakati akijibu swali la Antipas Mgungusi, mbunge wa Malinyi, lililohoji kuhusu upatikanaji wa vazi hilo, alisema kamati ya kitaifa ya kuratibu upatikanaji wa Vazi la Taifa imefanikiwa kukukusanya maoni kutoka kwa wadau na wananchi 20,452 kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani.

Alisema hatua iliyofikiwa sasa, kamati itakutana na kuwashindanisha wabunifu wa mavazi kutoka pande zote mbili za muungano ili wale watakaokuwa washindi kwa upande wa wanaume na wanawake, mavazi yao ndiyo yatapendekezwa kuwa Vazi la Taifa.

“Wabunifu hao watafanya kazi kwa kutumia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau na wananchi ili kukamilisha mchakato wa Vazi la Taifa kwa ufanisi na haraka zaidi, tumetumia njia hii ili kuharakisha mchakato na kupunguza uhitaji wa matumizi fedha nyingi za uratibu wa upatikanaji wa Vazi la Taifa,” alisema Mwinjuma.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags