Madudu afunguka tamthilia ya ‘Nazi Bubu’ kuwania tuzo Senegal

Madudu afunguka tamthilia ya ‘Nazi Bubu’ kuwania tuzo Senegal

Tamthilia ya Tanzania iitwayo ‘Nazi Bubu’ imechaguliwa kuwania tuzo za Dakar International Drama Festival zitazotolewa Senegal kupitia kipengele cha ‘Best Short Drama’.

Tamthilia hiyo yenye jumla ya Epsode 31 iliyokuwa ikirushwa katika kisimbuzi cha Azam kwenye chaneli ya ‘Sinema Zetu’ inaenda kushindana na tamthilia zingine tisa kutoka Cameroon, Burkina Faso, Senegal, Morocco, Afrika Kusini, Nigeria na Kenya ambazo zitaenda kuoneshana uwezo Octoba 8 mpaka 12 mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi, mwogozaji wa filamu hiyo Khatibu Madudu ameweka wazi kuhusu tamasha hilo kwa kueleza kuwa ni mahususi kwa ajili ya tamthilia zinazotengenezwa Afrika.

“Katika kipindi chote hicho hapakuwa na tamasha ambalo limejikita zaidi katika kuangazia series peke yake, na utaona kuanzia mwaka juzi na mwaka jana, zimejikita katika utoaji wa series peke yake,” alisema Madudu.

Hata hivyo, Madudu aliongezea namna tamthilia hiyo ilivyoweza kupenya na kuwania tuzo hiyo kwa kueleza kuwa aliwasilisha tamthilia hiyo baada ya nafasi kutangazwa.

“Utaratibu wao ni kwamba huwa wanatangaza kwa ajili ya watu kuwasilisha kazi zao, kwa hiyo zilivyotangazwa na sisi tukawasilisha, ikapitia mchujo na mpaka sasa tumeingia kwenye nafasi hiyo ambayo tunakwenda kushindana na nchi nyingine kama Cameroon, Burkina Faso, Senegal, Morocco, Afrika Kusini, Nigeria na Kenya,” alisema Madudu.

Ukiwa umebakia mwezi mmoja kuelekea kwenye tamasha hilo, Madudu amewataka waongoza filamu nchini kuzingatia misingi muhimu ya kupeleka kazi kimataifa.

“Kitu cha kwanza ambacho tunapaswa kuzingatia ni kuonesha utaalamu na kuwa na hadithi ambazo zinaweza kuvuka mipaka na kueleweka na watu wengine, walipo nje ya mipaka yetu, vilevile waongoza filamu wanapaswa kuongeza wigo wa ushindani,” alisema Madudu.
Aidha aliongezea kuwa tamasha hilo limebeba vitu tofauti kwani licha ya kuwepo kwa tuzo pia kutakuwa na mafunzo, maongezi ambayo yanahusu tasnia, kuonesha filamu mbalimbali.

‘Nazi Bubu’ ni tamthilia ya ucheshi, ambayo inaelezea hadithi ya binti anayeitwa Malikia, ambaye anamaliza chuo kikuu na kurudi nyumbani akiwa ana matarajio mengi sana kutokana na ndoto zake.

Lakini anapokuja nyumbani anakuta tayari familia ilikuwa na mipango mingine juu yake na hivyo analazimika kuwa na machaguo mawili tu, kwamba ni aidha aweze kuendesha biashara ya familia ambayo ni mgahawa au kuolewa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags