Ludigija awataka Wazazi kuwa chachu ya ufaulu kwa watoto wao

Ludigija awataka Wazazi kuwa chachu ya ufaulu kwa watoto wao

Mkuu wa Wilaya Ilala, Ng`wilabuzu Ludigija amesema wazazi wana nafasi kubwa katika kuhakikisha watoto wao wanafanya vizuri darasani na hivyo kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.

Ludigija ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa tuzo kwa shule za msingi za Serikali na binafsi zilizopo katika wilaya hiyo ambazo zimefanya vizuri kitaifa kwenye mitihani mwaka wa masomo 2020/21.

Alisema uzoefu unaonyesha wanafunzi wanapofeli mitihani yao, lawama zote huwaangukia walimu jambo ambalo amesema linapaswa kupingwa kwa kila mtu kutimiza wajibu wake kuhakikisha watoto wanafaulu.

“Wazazi wanawajibu katika kuhakikisha mtoto anafaulu hivyo niwaombe walimu wakuu na wakawaida tuendelee kuwaelimisha wazazi hawa namna ya kufanya ili tuongeze idadi ya wanafunzi wanaofaulu,” alisema na kuongeza

“Tunafanya haya yote tunataka wilaya yetu endelee kufanya vizuri na kushika namba moja kwa ubora wa ufaulu Dar es Salaam, hivyo tukifanya kazi kwa kushirikiana lazima mafanikio yataonekana na tutaweza kutatua changamoto zetu kwa urahisi,” alisema Ludigija

 

Hata hivyo Ludigija alisema ugawaji wa tuzo kwa shule zilizofanya vizuri katika wilaya ya Ilala ni moja ya kutambua mchango wa kila mmoja aliyefanikisha wilaya hiyo kushika nafasi ya nne kitaifa kwa ufaulu kwa mwaka wa masomo 2020/21.

“Kushika nafasi ya nne kitaifa kwa wilaya ya Ilala siyo kazi nyepesi, hii imeonesha wazi kuwa shule za Serikali na binafsi zinafanya kazi nzuri na zinapaswa kupongezwa na kupewa tuzo,” alisema

Naye Ofisa Elimu Wilaya ya Ilala, Sipora Tenga alisema katika wilaya hiyo zipo shule za serikali na binafsi zinazotoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambazo ni Msimbazi Center, Mzambarauni, Buguruni Viziwi, Uhuru Mchanganyiko, Maarifa, Pugu Kajiungeni, Airwing.

“Tunaopia walimu ambao wanatoa mafunzo mbalimbali kwenye kituo cha watoto wenye saratani Hospitali ya Taifa Muhimbili, yupo mwalimu mmoja anayemfundisha mtoto mwenye shida ya kupumua ambaye utumia gesi kupumua,” alisema

Naye Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Tigohane, Ponsiano Ngumburu ameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya shule ili iwe rafiki kwa walimu katika ufundishaji.

“Hatuwezi kuongeza ufaulu bila kuboresha mazingira na miundombinu ya shule, kwa sasa Serikali inajitahidi, tunaomba iendelee kuboresha ili iwe rafiki kwa walimu na tunamatumaini kasi ya ufaulu itaongezeka mara dufu,” alisema






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags