Kuna Wanamuziki, Madijei, Mashabiki na muziki

Kuna Wanamuziki, Madijei, Mashabiki na muziki

Wanamuziki wanawaza chapaa, mkwanja, faranga, njuruku, mapene, mawe, ukwasi, fuba na maneno yote yanayomaanisha pesa, fedha au shilingi. Wanavuja jasho kwenye kila kitu kinachohusu muziki ili wapate pesa.

Katika mitikasi yao ya kusaka pesa, ndipo wanapojikuta wanazalisha 'kontenti' kibao kwenye maisha yao. Kuanzia michongo inayohusu ngono, uhusiano wa kimapenzi, familia, urafiki wa kawaidai pamoja na ushirikiano wa wao kwa wao.

Mgongano ama mgogoro wa Konde Boy na Mondi ni katika kusaka pesa. Yes! Hakuna lingine lililosababisha wao wakawa vile walivyo kwa sasa. Machungu ya kutaka pesa ndiyo yanayopelekea washikaji kuwa adui na adui kuwa washikaji.

Na kwenye mishe zao hizo hizo za kusaka pesa, ndipo wanapojikuta wanasahau hata asili, utamaduni, nia, sababu na lengo lao. Na hapa ndipo ambapo wanamuziki wanapoonesha athari zao kwenye jamii husika inayowazunguka.

Konde Boy anasaka pesa siyo utamaduni. Usishangae yeye kuiga amapiano kwa sababu hiyo ndiyo inayompa pesa na siyo asili wala utamaduni wa Kimakua. Sasa anafanyaje ngoma za sindimba katikati ya jamii yenye mizuka na amapiano?

Mondi anahangaikia 'kumenteini' ukwasi wake. Ili aweze kufanya hivyo inabidi azalishe zaidi pesa. Sasa atazalishaje pesa kwa kufanya muziki wa mchiriku wakati ukweli ni kwamba kizazi hiki kinataka swaga za 'Unaija'?

Na kuna 'Madijei'. Hawa jamaa wanachangia kwa kiasi kikubwa sana kina Marioo kujikuta wanakimbilia kwenye 'amapiano' badala ya Bongo Fleva yao. Marioo akiingia klabu ama sehemu yoyote yenye mizuka anasikia 'Dijei' anaungurumisha 'amapiano'.

Na yeye anataka kuona sehemu kama ile mapini yake yanagongwa kama zinavyogongwa 'amapiano' za 'Kwa Zulu Natali'. Kesho yake anamtafuta 'Esi Tu Kizi' anamwambia ''Mwanangu nigongee mdundo wa amapiano moja matata."

'Esi Tu Kizi' anataka mapene anaachaje sasa? Anamnyongea fasta tu anakunja fuba lake anaweka kwenye simu, benki ama anamtumia mrembo wake kisha maisha yanaendelea. Hizo mishe za midundo ya asili sijui ya taifa mtajua wenyewe.

'Projuza' anafanya kazi kulingana na matakwa ya mwanamuziki wake. Na mwanamuziki anataka kazi yake ifanyike sawa na soko linavyotaka kwenye kumbi za starehe, vituo vya redio, mitandaoni, runingani mpaka kwenye korido za shule na 'gesti'.

Mashabiki wao ni walaji, ukiwapa chakula kizuri watakila tu. Wanamuzjki, Madijei na Watayarishaji wa muziki wao wanataka pesa. Kwa hiyo wanapeleka jambo kwa watu ili wapate pesa. Ama kwa kulazimisha ama kwa mahitaji ya watu wao wanapeleka tu.

Hapa huwezi kumnyooshea kidole yeyote kati ya mwanamuziki, mchezeshaji wa muziki na mtayarishaji wa muziki. Hapa ni kama kuku na yai haieleweki kipi kilianza. Ndivyo ambavyo hatujui nani alianza kutuletea amapiano kwenye sikio zetu.

Tunaona tu amapiano yanarindima kila kona ya mtaa hapa Bongo, na wanamuzki na ‘madijei’ wanatugongea tu. Je ni mashabiki waliosababisha ‘madijei’ na wanamuikzi waanze kutwanga amapiano? Ama wanamuziki na ‘madijei’ ndiyo waliosababisha?

Muziki hauna mipaka. Muziki unapoingia masikioni hautoi taarifa kwamba mimi 'amapiano' ama mimi 'zuku' nakuja sikioni kwako. Muziki unapigwa tu ni masikio ya binadamu yanayoamua kuvutiwa nao ama namna gani. Huo ndiyo muziki.

Lakini muziki kupendwa na mtu ni mosi, lakini kuufanya kuwa muziki pendwa na watu wa jamii yao ni jambo mtambuka ambalo linahitaji ushirikishwaji. Yaani watu wa muziki wenyewe ndiyo chanzo cha kufanya aina fulani ya muziki uwe pendwa ndani ya jamii husika.

Kuanzia wanamuziki, ‘madijei’ pamoja na wadau mbalimbali wa muziki ndiyo wanaochangia aina fulani ya muziki kuwa pendwa na watu walio wengi. Kitu kama amapiano hata usipogonga redioni ama kwenye kumbi za starehe utasikia kwenye kumbi za harusi.

 

Kimsingi muziki ni kama 'jini', hauna umbile wala rangi. Muziki ni hisia. Ogopa sana kitu kinachoingiliana na hisia za mwanadamu. Na zipo hisia ambazo zinajitokeza tu zenyewe, na kuna hisia ambazo zinachangiwa na vichocheo vingine vingi.

Hata kwenye mapenzi unaweza kuwa na hisia na mwanamke kwa sababu zako mwenyewe. Na unaweza kuta hisia kali na mwanamke fulani kwa sababu za kuchochewa na huyo mwanamke mwenyewe. Kama vazi ama pozi zikavuruga ubongo wako.

Hata muziki unaweza kuuhusudu kwa kuusikiliza mara moja tu, lakini pia unaweza kuuhusudu kwa sababu ya kuusikia mara kwa mara. Kuna nyimbo nyingi mbaya tulizipenda kwa sababu ya kusikia kila wakati. Tunalazimika kuzipenda.

Kimsingi Wabongo tuna tatizo la mapokeo. Sisi ni watu wa mapokeo. Bahati mbaya ufundi wetu kwenye mapokeo upo kwenye vitu vya kibwegebwege tu. Huwezi kuona tuna vijana kibao ambao wameathiriwa na mapokeo ya teknolojia au uzalendo.

Yaani ni rahisi kukutana na kijana mwenye kuiga kila kitu cha Jay Z. Lakini anazeeka bila kutafuta, kummiliki na kumtunza Beyonce wake wa Ngarenaro. Na kuna dada anaiga kila kitu cha Beyonce lakini hana Jay Z wake wa kumtuliza huko Buguruni.

Yaani tunaiga muziki wao, mavazi yao, swaga zao na hata uongeaji na utembeaji wao. Lakini tabia zao njema tunazipuuza. Yaani Jay Z wa Mikocheni hana upendo na Tanzania kama yule Jay Z wa New York alivyo na upendo na Amerika yake.

Hili ni tatizo hata kwenye nyanja mbalimbali. Wachezaji kibao wanaiga ushangiliaji wa Ronaldo, lakini wanashindwa kuiga bidii, nidhamu, kujituma na kujitunza kwake kunakopelekea aendelee kuwapelekea moto mpaka uzeeni.

Kimsingi wanamuziki, ‘madijei’ hata mashabiki wa muziki wanaukosea heshima muziki wenyewe. Muziki ni muunganiko wa maneno na midundo. Haijalishi maneno yanamaanisha kitu kitu gani. Kwa sababu muziki ni hisia kwanza kabla ya elimu.

Lakini pamoja na yote hayo kuna haja ya uzalendo na uzalendo unakuja kutokana na moyo wa kupenda vya kwetu. Sisi tuna muziki wetu tatizo letu tunapenda visivyo vya kwetu. Tunaishi katika dunia ya mapokeo toka nyakati za kina Dr Livingstone, Carl Peters na wenzao.

Bongo Fleva haipo tena hapa Bongo tusidanganyane. Kilichopo Bongo ni Diamond, Alikiba, Harmonize na wenzao wanaotambulika kama wanamuziki wa muziki wowote. Kwa sababu ndani yao utakutana na Naija, Bolingo, Amapiano, Zuku, Salsa, Hip hop, R&B na nyinginezo.

Miriam Makeba, Oliver Mutukudzi, Angelina Kidjo, Monu Dibangu, Seif Keita hata Pepe Kalle, walijivunia muziki wa kwao wakawa wakubwa duniani bila kuwaiga kina Michael Jackson, Lonie Rich, Marvin Gaye, na Steve Wonder . Tunazingua 'bigi taimu' Wabongo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post