KIWEMBE: Sehemu ya kwanza

KIWEMBE: Sehemu ya kwanza

KIGOMA MJINI, MACHI, 2005

ALIPOCHEKA, alipendeza. Tabasamu lake zuri, tabasamu linaloshawishi na kubembeleza, huwafanya watu, hususan wanawake wamsogelee na kumsalimia. Baadhi ya wanawake hao husisimkwa miili pindi tu waisikiapo sauti yake na huchanganyikiwa pale wanaposhikana mikono.  Pia, alikuwa na sauti ya kipekee, sauti iliyogusa hisia  zao na kuamsha gharika la maraha kwenye michipuo ya fahamu zao.

Ni kijana wa kiume, mwenye sura ya ucheshi na macho ya upole. Hakuwa mwoga wa kutazamana na mtu, lakini hakupenda kutazamana na mwanamume mwenzake. Kwake, macho ya mwanamume mwenzake yalikuwa na kitu asichokijua, kitu kisichopendeza. Yalimtisha!

Hata hivyo, hali hiyo ilikuwa kwa wanaume tu, siyo kwa macho ya wanawake. Aliyapenda macho ya wanawake na ilipotokea akakutanisha macho na kiumbe yeyote wa kike, katu hakuyabandua macho yake. Ndani ya mboni za mwanamke yeyote kulikuwa na kitu fulani kisichoelezeka, lakini kilichomvutia na kumsisimua.

******    

ALIPOZALIWA wazazi wake walimpa jina la Maftah, jina ambalo baada ya miaka kadhaa lilipotea na kuzaliwa jina lingine, jina la Kiwembe ambalo alipachikwa kutokana na yale ayapendayo na ayatendayo, yale aliyokwishayageuza sheria badala ya kawaida.

Ni katika kitongoji cha Ujiji mjini Kigoma ambako Kiwembe alizaliwa. Wazazi wake  walikuwa na nyumba katika Kata ya Kasingirima, na katika ndoa yao walibahatika kupata mtoto mmoja tu, huyo Kiwembe.

Kiwembe hakubahatika kufaidi vilivyo malezi ya baba na mama. Mwaka 1978 Mji wa Kigoma ulitikiswa na maradhi ya kipindupindu, maradhi yaliyowakumba wakazi wengi, na wengi wao wakafariki dunia. Wazazi wa Kiwembe walikuwa miongoni mwa waliofariki dunia kwa maradhi hayo. Walimwacha Kiwembe akiwa na umri wa miaka kumi na miwili.

Mzigo wa kumlea mtoto Kiwembe ulihamia kwa mama yake mdogo ambaye aliishi mtaa wa tatu kutoka kwao Kiwembe. Hayakuwa maisha yaliyostahili kwa mtoto wa rika la Kiwembe. Huyo mama yake mdogo hakujali kuwa mtoto huyo kala nini au kama anahudhuria masomo ipasavyo. Hivyo, mara nyingi Kiwembe akawa anazurura mitaani. 

Akiwa ni mtoto ambaye alijaaliwa kukua harakaharaka, Kiwembe alikadiriwa na wengi kuwa ana umri wa miaka kumi na minane au ishirini. 

Ni umbo lake hilo kubwa ndilo lililomfanya Mama Kadala wa mtaa wa pili amtazame mtoto wa watu kwa macho yenye kila dalili ya njaa dhidi yake. Mama huyo aliyekuwa na umri wa kutosha kuwazaa kina Kiwembe wengine kama watatu, hakuwa mtu wa kujali eti huyu ni kijana aliyekwishabalehe au bado.

Alichopenda yeye ni ‘kupakata dogodogo.’ Na baada ya kumwona mtoto Kiwembe akiwa hana uangalizi mkubwa, akaamua kumwinda taratibu. Jimama hilo tipwatipwa likawa haliishi kujipitishapitisha jirani alikoishi mtoto Kiwembe.

Jimama hilo lilimpenda na kumtamani Kiwembe. Likawa tayari kufanya jambo lolote na mtoto huyo potelea mbali hayo matokeo yake yatakavyokuwa. Na hata kama matokeo hayo yatakuwa ya kumfedhehesha, hakujali. Aliapa kuwa ni lazima ‘aanguke naye kisahani.’

Ndipo ikaja siku ambayo Kiwembe alijikuta akiingia kwenye anga za Mama Kadala.






Comments 3


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post

Latest Tags