Na Aisha Charles
Sura yake imejaa hisia kali kuwasilisha anachomanisha, anapofumbua mdomo wake kuimba mashairi yanayosisimua moyo, huku akifumba na kufumbua macho kusisitiza umuhimu wa ujumbe wake, hapa namzungumzia msanii wa bongo fleva, Sunday Moshi Mangu 'Linex ' aliyewahi kutamba na kibao cha Mama Halima.
Ni miongoni mwa wasanii usioweza kutilia shaka kusikiliza nyimbo zake mahali popote ama kuangalia video zake mbele ya mtu yeyote, kutokana na kuzingatia maadili ya Kiafrika, ukiachana na hilo asilimia kubwa ya tungo zake zina visa vinavyoishi na kusisimua.
Linex ni msani ambaye amekuwa akijitahidi kutoonekana kwenye kiki yoyote mjini ingawa yeye ni mtu maarufu ila nyimbo zake zina kiki zaidi ya kiki zinazofanywa na baadhi ya wasanii hapa nchini, wanaokuwa wanatanguliza matukio wakati mwingine yanakuwa hayana maadali ya Kitanzania ili wazungumziwe ndipo waachie ngoma zao.
Mwananchi Scoop imeweza kukutana nyota huyu na kufunguka mengi kwa kuelezea vitu muhimu anavyozingatika katika uandishi wa nyimbo zake ambao unafanya nyimbo zake kuishi na kusikilizwa kwa zaidi ya miaka 10.
"Nipo ndani ya jamii, ninaimba uhalisia wa maisha yanayoendelea kwenye jamii yetu, ndiyo maana hata nikiimba nakuwa makini kutuliza akili ili ujumbe unapotoka uwe sehemu ya maisha yao, pia napenda kuandika ujumbe unaoishi ili mashabiki wangu wanaosikiliza nyimbo zangu wapate kitu kizuri” anasema Linex.
NYIMBO ZAKE ZA HISIA
Anasema kutokana na matukio anayoyaona kila siku kwenye jamii, yanampa umakini wa kukaa chini na kutafakari ni kitu gani anapaswa kukifanya kama kioo cha jamii, hivyo wakati wa kuwasilisha ujumbe anakuwa anaimba kutoka rohoni.
Hata hivyo ameeleza kuwa ndani ya nyimbo zake anaibua tatizo na kuweka ushauri ama kutoa moyo, anakoamini atawafikia wanyonge wanaohitaji faraja ya mtu kuwathamini.
"Mara nyingi ninapokuwa kwenye morali ya kufanya kazi, huwa nazingatia kuwa hawatasikiliza siku moja ama mbili, najua wanakuwa kwenye raha na matatizo, lakini wale wenye matatizo nakuwa nawaletea faraja ili kuwapa hisia," anasema na kuongeza kuwa;
"Pia inatokana na kulelewa na mama yangu ambaye ni mkulima wa jembe la mkono ambaye alipambana kuhakikisha tunakuwa hadi tulipo, hivyo kila ninachoimba kina maana halisi iwe ndani ya familia ama nje ya familia na huwa simtaji baba mara kwa mara kwa sababu sijawahi kuwa karibu na yeye, sijui mengi kumhusu na hajui mengi kunihusu,"anasema.
NYIMBO INAYOHUSU MAISHA YAKE
"Wimbo ulionitambulisha kwenye muziki ni ‘Mama Halima ‘ ambao ndiyo ulinitambulisha kwenye muziki, awali wimbo ulikuwa unaitwa ‘Halima’ lakini uimbaji ndiyo ukafanya niongeze mama ili usaundi vizuri, huo una uhalisia wa maisha yangu ya sanaa, ingawa zote kwangu zina umuhimu mkubwa," anasema ‘staa’ huyo.
MUZIKI UMEMLIPA
amesema kuwa muziki ni biashara anapoona inaenda sivyo ndivyo anatuliza akili kujipa muda wa kusoma ramani itakayompa muelekeo wa nini afanye ili umlipe kama anavyotaka na kufichua kwamba ndiyo sababu ya kukaa kimya kwa muda mrefu bila kutoa ngoma.
"Huwa hainipi hofu kukaa muda mrefu bila kuachia ngoma, kwani najua nina kipaji kikubwa nilichopewa na Mungu, najua nikirudi nakuwa na jambo jipya la kuwafurahisha mashabiki wangu ambao wanapenda kazi zangu,"anasema Linex.
ANARUDI KWA KISHINDO
Anasema albamu yake mpya ipo mwishoni kukamilika, anayoielezea itakuwa na nyimbo za dini zitakazosikilizwa na mtu yeyote kutokana na ujumbe uliomo kwenye nyimbo zake baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu.
"Nimefanya hivyo baada ya watu wengi kuniomba nifanye hivyo, kutokana na kusikiliza baadhi ya nyimbo nilizowahi kuziimba za dini kama ‘Kaa Nami’, ndiyo maana albamu inayokuja itakuwa haibagui mtu kwa maana ya mkristo ama muislamu, kijana na mzee, watasikiliza na kuburudika"anasema.
Anasema lengo la kuimba nyimbo za dini siyo biashara, badala yake anachukulia kama ibada ya shukrani kwa Mungu wake, huku akiwakumbusha wasanii wenzake kwamba kazi wanayofanya haimanishi wasiwe wanaenda mahali patakatifu pakuabudu.
"Narudi kwa kishindo, itakuwa bandika bandua, ukiachana na hizo za dini nina ujio mwingine wa nyimbo za bongo fleva nimeziandaa kwa kutuliza akili, nimezingatia wakati navuma kilikuwa kizazi kingine na hiki ni kizazi kingine, lakini yote hayo sijaenda nje ya maadili yakufanya watu wasiwe huru kuangalia popote,"anasema.
TUKIO LA MAUMIVU
Anasema alikuwa na kaka yake mtoto wa mama yake mkubwa alikuwa anaitwa Sunday, ambaye ndiye aliyemkuta kwa mara ya kwanza akiwa amejifungia chumbani kwake anaimba, akiwa hataki mtu amsikie kama ana kipaji, kwani alikuwa hana uhakika wa kuungwa mkono.
"Baada ya kuingia alistajabu sana, nikajua labda ananishangaa kumbe anafurahia aina ya uimbaji wangu, akaniambia niimbe tena nikaimba, ndipo akaniambia niende Dar es Salaam nitatoboa na kufika mbali, nikafanya hivyo, lakini kabla hajaanza hata kula matunda ya kunipambania akaaga dunia, hiyo inaniumiza hadi kesho, tulipendana sana, majina yetu yalikuwa yanafanana, mimi Sunday mdogo yeye mkubwa,"anasema.
Anasema alishamwambia mama yake mzazi kwamba anataka kuwa mwanajeshi, hivyo ikawa inamuwia vigumu kuimba hadharani kwa wakati huo, anasisitiza kwamba hiyo ndoto bado ipo moyoni mwake.
AMTAJA DIAMOND
Anaitaja kolabo ya nyimbo ya Halima aliyomshirikisha mwanamuziki anayetamba ndani na nje, Diamond Platnumz, kwamba ndiyo ilikuwa kubwa kutokana na mapokeo kwenye vyombo vya habari na jamii kwa ujumla na kwamba huenda inatokana na nguvu aliyonayo msanii mwenzake.
"Nashukuru vyombo vya habari vilivyo ‘usapoti’ wimbo huo, hata Diamond mwenyewe kukubalia kufanya kazi na mimi, kutokana na hatua aliopo kwa sasa ni kubwa ndani na nje ya nchi ana mamilioni ya watu wanaofuatilia muziki wake, yaani hadi sasa ndiyo wimbo unaoangaliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii,"anasema.
ELIMU YA NDOA
Baadhi ya nyimbo zake zina ujumbe unaohusu kulinda ndoa, analifafanua hilo kwamba linatokana elimu ya Biblia anayoisoma mara kwa mara tangu akiwa mtoto mdogo, hivyo inampa upana wa kufanya vitu vyenye maana za kuishi katika jamii, inayozisikiliza kazi zake na kuziunga mkono.
"Sijaoa ila nimefanikiwa kupata mtoto mmoja anaelekea kuwa na miaka minne, ila nina uwelewa wa mambo ya ndoa, familia yangu ni mama yangu, mama zangu wadogo, wadogo zangu na marafiki wa kweli wanaonizunguka," anasema na anaongeza kuwa;
"Kwa sehemu nina ufahamu wa neno la Mungu, nilianza kufundishwa tangu nikiwa mtoto mdogo, najikuta ninakuwa na ujumbe mzito wakati wa kuandika nyimbo zangu, ndiyo maana nyingine naomba mwisho mwema, kukumbuka ibada vitu kama hivyo,"anasema Linex.
Pengine kuna mtu anawaza kuimba lakini anahofia kuwa kutetereka kwa maadili aidha ya dini au alivyolelewa lakini kupitia msanii huyu utakuwa umepata kitu cha kuanzia katika namna ya kuimba bila kukengeuka kwenye kile unacho kiamini.
Leave a Reply