Jux anamtumia Priscilla kumrusha roho Vanessa Mdee

Jux anamtumia Priscilla kumrusha roho Vanessa Mdee

Kati ya mastaa Bongo walioteka mazungumzo mtandaoni wiki hii, ni Jux, 34, mara baada ya kumtembelea nyumbani kwao Nigeria mpenzi wake mpya, Priscilla Ojo, 23, ambaye ni muigizaji na mshawishi wa chapa.

Jux amekutana na familia ya Priscilla au Priscy akiwemo mama yake mzazi, Iyabo Ojo, mmoja wa waigizaji wakongwe kutoka Nollywood akiwa ameshiriki katika filamu zaidi ya 150 na kutoa zake binafsi 14.

Kwa namna jambo hilo lilivyowekwa katika mitandaoni ya kijamii, kuna hisia na maoni mseto yanayodai kuwa Jux anatumia uhusiano wake na Priscilla kumrusha roho mpenzi wake wa zamani Vanessa Mdee au Vee Money,

Jux, mwanamuziki aliyevuma na kundi la Wakacha, tangu ameanza kuweka hatharani sehemu ya maisha yake binafsi kutokana na umaarufu wa kazi zake, uhusiano wake na Vanessa ndiyo uliodumu kwa kipindi kirefu zaidi.

Wawili ambao walishirikiana katika nyimbo mbili, Juu (2016) na Sumaku (2019), uhusiano wao ulianza mwaka 2014 hadi 2019 walipoachana wakiwa wamefanya mambo mengi pamoja kama kuandaa tamasha lao la Inlove & Money Tour 2018.

Mbali na Vanessa, Jux alishakuwa na uhusiano na warembo wengine kama Jacqueline Wolper, Jackie Cliff, Nayika Thongom kutokea Thailand na Karen Bujulu huku akihusishwa pia na Huddah Monroe wa Kenya.

Je, kwanini Jux anahisiwa kutumia uhusiano wake na Priscilla, msomi wa Chuo Kikuu cha Babcock kumrusha roho Vanessa?. Hiyo ni kwa sababu baada ya kuachana kwao, Vanessa alienda kuwa na Rotimi mwenye asili ya Nigeria.

Vanessa na Rotimi kwa mara ya kwanza walikutana Julai 2019 katika tamasha la Essance nchini Marekani ambapo wote walitumbuiza, baada ya show wakabadilishana namba za simu na mengine sasa ni historia.

Rotimi ambaye ni muigizaji na mwanamuziki alimvisha pete ya uchumba Vanessa hapo Desemba 2020, wawili hao wanaoishi wote huko Georgia, Marekani, tayari wamejaliwa watoto wawili ambao ni Seven (2021) na Imani (2023).

Hivyo Jux naye kaamua kwenda kimataifa kama Vanessa, kama umeamua kwenda Nigeria, taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika, nami nakuja huko huko tuoneshane makali.

Ndicho anafanya Jux kwa kumtumia Priscilla ambaye alipokuwa na umri wa miaka 14 aliteuliwa kuwania Tuzo ya Muigizaji Bora wa Kike katika Tamasha la Filamu Nigeria 2015 baada ya kufanya vizuri katika filamu ya Beyond Disability (2014).

Inaonekana hivyo kutokana na tangu Jux ameachana na Vanessa akili yake bado ipo kwa mrembo huyo, kupitia nyimbo zake zilitoka baadaye tunaona ukweli wa jambo hilo.

Mwanzoni mwa video ya wimbo wake, Sio Mbaya (2020) unasikika wimbo 'Sumaku' aliofanya na Vanessa, huku ndani yake akionekana mrembo aliyefanana kabisa na Vee ambaye Jux anamwimbia kwa kusema kwake sio mbaya hata akimpigia simu.

Pia katika wimbo wa Rayvanny, Lala (2021) ambao Jux alishirikishwa, analitaja kabisa jina la Vanessa na kusema alishamsahau kabisa na kusitisha mawaliano naye.

Na mara baada ya Vanessa kuweka wazi kuwa anatarajia mtoto wake wa kwanza hapo Septemba 2021, Jux hakupoteza muda, akaingia tena studio na kumtolea wimbo maalamu wa pongezi 'Sina Neno' ambao cover lake lina picha ya mama mjamzito.

Hayo ndiyo maisha ya Jux tangu ameachana na Vanessa, mambo mengi anayofanya yanamlenga mwimbaji huyo aliyetoka kimuziki na wimbo wake, Closer (2013) chini ya B'hits Music Group na kumpatia tuzo ya muziki Tanzania (TMA) 2014 kama Wimbo Bora wa RnB.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags