Niaje niaje matajiri wangu, kama kawaida kila wiki tunakutana kwenye chimbo letu la Biashara ambapo tunafundishana mambo mbalimbali kuhusiana na biashara, ujasiriamali nk.
Na leo nimekusogezea biashara unayoweza kuifanya na ikakuingizia maokoto ya kutosha. Hii ni biashara ya Achari.
Ni wachache jina hili litakuwa geni masikioni mwao, lakini wengi naamini mmewahi kusikia, kuona na pengine kuitumia kabisa.
Kama umewahi kula ubuyu au embe na ukaridhishwa na ladha yake, sasa ukithubutu kuonja lililotengenezwa kuwa achari hutajutia.
Biashara ya achari mara nyingi hufanyika kwenye maeneo ya karibu na shule, yenye watu wengi na asili ya kuuzwa katika maeneo hayo ni kwa sababu inapendwa na watu wengi.
‘Achari’ ni snack au tunaweza kuita ubuyu unaotengenezwa kwa kutumia embe na mara nyingi watu wanapenda kula wakati ambao wanahisi hamu ya kutafuna kitu fulani.
Bila kupoteza muda ungana nasi mwanzo mpaka mwisho kujua namna ya kutengeneza snack hiyo.
Mahitaji
- Maembe mabichi 2-3
- Unga wa ubuyu robo
- Sukari robo
- Rangi nyekundu ya chakula kijiko kimoja au viwili
- Hiriki ya unga kijiko kimoja
- Chumvi kiasi
- Pilipili mtama (ukipende nusu kijiko)
Namna ya kuandaa Achari zako
Ø Chukua maembe yako yaoshe na uyamenye vizuri
Ø Ukishamaliza kuyamenya anza kwa kukata vipande vidogovidogo ndogo ndogo (hapa utakata mfumo kama wa chipsi lakini hizi zinatakiwa kuwa nyembamba sana)
Ø Baada ya kukata maembe yako yote, chukua bakuli kubwa na uanze kutia vitu vyako, anza na chumvi, hiriki, pilipili mtama kiasi, rangi ya ubuyu kisha sukari na Mwisho weka unga wa ubuyu.
Ø Kisha anza kwa kuchanganya mchanganyiko wako hadi rangi ya maembe asili isionekane, yaani ionekane tu rangi ya ubuyu, pia hakikisha sukari inakolea.
Ø Ukishamaliza hapo chukua sinia kubwa, anza kuzisambaza, ukishaona ziko sawa tafuta kitu kinachoweza kupitisha jua kwa juu mfano wavu na ufunike.
Ø Baada ya kufunika nenda kaweke juani usiku ukiingia zitoe weka ndani kesho yake weka tena hadi pale zitakapokauka, inategemea na mkato wako ukikata nene sana zitachelewa kukauka lakini nyembamba zinawahi kukauka. Zinachukua siku mbili hadi tatu kukauka.
Kufikia hapo ubuyu wako wa embe utakuwa tayari kinachofuata ni kuanza kuupaki kwenye package ulizoziandaa na mara nyingi bei yake inaanzia Sh1,000 hadi Sh2,000 kwa pakti moja.
Ukiwa na pakti 20 uko mbali sana chukua fursa hiyo mwanangu wacha kukaa kizembe.
Leave a Reply