Jinsi ya kupika urojo kwa ajili ya biashara

Jinsi ya kupika urojo kwa ajili ya biashara

Ubaya ubwela, yaani ni mwendo wa ku-force mambo tuu, wiki hii kupitia biashara tumeangazia, namna ambavyo  biashara ya urojo inaweza kukuingizia kipato endapo utaifanya kwa umakini.

Urojo unafaida sana pale tuu utakapotilia maanani kuifanya biashara yako ikue zaidi kwani baadhi ya maeneo wanauza bakuli moja kuanzia Sh 15,00 hadi 2,000 .

Hivi ni vitu ambavyo unatakiwa kuchanganya na urojo wako

  • Viazi mbatata vya kuchemsha (hivi utavikata saizi utakayo havitakiwi kukatwa vipande vikubwa sana)
  • Mayai ya kuchemsha
  • Bagia
  • Chatne (pilipili)
  • Chipsi za muhogo
  • Mishikaki
  • Kachori
  • Uji wa urojo wenyewe

Ili kufanikiwa kutengeneza chakula hichi kwa ufasaha basi utatakiwa kuanza kuandaa baadhi ya vitafunwa. Mfano kachori na bagia hazitakiwi kuwa kubwa zinatakiwa kuwa za saizi ya kati kwakua tulishafundisha kutengeneza hivyo basi leo tutakujuza namna ya kupika uji wa urojo tuu. 

MAHITAJI

  • Unga wa ngano nusu kilo au robo inategenea na wingi wa urojo wako
  • Ndimu au limao zilizokamuliwa 2
  • Maji lita 2
  • Chumvi kiasi
  • Binzari kijiko cha chai 1
  • Pilipili mtama kiasi

 

JINSI YA KUPIKA

  • Chukua sufuria kubwa kiasi na ubandike jikoni, weka maji na chumvi kiasi pamoja na pilipili mtama
  • Acha maji yaendelee kupata moto, chukua bakuli weka maji kidogo korogea unga wa ngano kisha mimina na binzari yako na ukoroge mchanganyiko huo mpaka utakapo korogeka vizuri.
  • Chukua binzari yako mimina kwenye sufuria uliyobandika jiko na ukoroge taratibu, acha uchemke kidogo kisha mimina ndimu yako na ukoroge kidogo.
  • Acha uchemke onja chumvi na ndimu kama zipo sawa mpaka kufikia hapo utakuwa tayari na ikiwa urojo ni mzito sana ongeza maji acha uchemke kidogo kisha uepue

Angalizo:

Kama urojo ukiwa mkali (umekolea sana ndimu) au una chumvi nyingi ongeza maji kidogo kidogo mpaka upungue ukali, pia hakikisha huuachi jikoni kwa muda mrefu mpaka ukaungua kwa sababu utakuwa mbaya. 

Jinsi ya Kuuandaa

  • Chukua bakuli lako weka viazi mbatata kuanzia vipande vitatu, yai lisiwe zima unaweza kulipasua mara mbili au tatu.
  • Kisha weka, chipsi za mihogo, bagia, chatne, pilipili kiasi, kachori na kitafunwa chochote ambacho umekiandaa.
  • Malizia kwa kuweka mishikaki na umimine uji wako wa urojo.

Mpaka kufikia hapo urojo wako utakuwa umekamilika, na upo tayari kwa ajili ya kuliwa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags