Jinsi ya kupika bagia za dengu

Jinsi ya kupika bagia za dengu

Niaje niaje, wiki ya kuchakarika ndiyo imeanza, huku hatujamaliza ada huku kodi, kule bill zingine, unalipaje mahitaji yote hayo, jibu ni kujishughulisha, na kama kawaida yetu @Mwananchiscoop hatukai kizembe katika biashara tumekuletea namna ya kupika bagia za dengu.

Bagia za dengu ni kitafunwa ambacho watu wengi hupendelea kunywa na juice, chai ya maziwa na hata ya rangi, ni wewe tuu kuchagua unataka kula na nini, bei zake ni kuanzia sh 200 mpaka 300 haswa ukipata sehemu yenye mzunguko wa watu utauza zaidi.

Siku zote naleta ujuzi huu mdogo mdogo watu wanaweza kudharau lakini ndiyo biashara ambazo zinalipa, kuuzika na zenye faida kuliko hata watu wanavyofikiria cha muhimu ni kutafuta sehemu ambayo inamzunguko wa watu, mfano Kariakoo, Kigamboni Feri, Mbezi stand, Mbagala, sehemu za shule nk.

Mahitaji

             Unga wa dengu nusu

             Chumvi kijiko cha chai

             Maji baridi- 1 glass.

             Baking Powder kijiko 1 cha chai

             Majani ya kotmiri, unatakiwa kuyakata size ndogo ndogo

             Kitunguu maji kilichosagwa vijiko 2

             Kitunguu saumu kilichosagwa au ya unga- kijiko cha chai

             Pilipili mtama nusu kijiko

             Mafuta ya kukaangia

 

Namna ya kutayarisha na kupika

             Chukua bakuli kubwa kiasi ambalo litatoshea vitu vyako vyote, weka unga, viungo vyote anza kuchanganya kwa pamoja mpaka uji wa dengu uwe mwepesi kiasi, hakikisha usiwe mzito wala mwepesi sana uwe katikati.

             Acha mchanganyiko wako kwa muda wa dakika 15-20

             Weka karai lako jikoni mimina mafuta yaache yapate moto kiasi kama unataka kupika maandazi, angalizo mafuta yasipate moto sana kuepusha kubabua bagia zako.

             Anza kuchoma bagia zako na hapa unaweza kutumia upawa kutengeneza shape ya bagia yako ukiwa unaweka kwenye mafuta.

             Ziache mpaka ziwe rangi ya brown kisha ziweke katika chujio kwa ajili ya kuchuja mafuta.

Mpaka kufikia hapo vitafunio vyako vitakuwa tayari, na katika biashara yako unaweza kuweka naksinakshi kidogo kwa wateja, ukaweka tomato, pilipili ili hata mteja akija na kuulizia basi asikose.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags