Jinsi mfumo dume unavyowaponza wanaume

Jinsi mfumo dume unavyowaponza wanaume

Hivi karibuni nilibahatika kukutana na ripoti ya Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) ya mwaka 2015. Najua ni ya siku nyingi lakini ilinifikirisha sana.

Mbali na mambo mengine niliyoyaona katika ripoti hiyo nilivutiwa na taarifa ya idadi ya watu waliohukumiwa kunyongwa wanaosubiri kutekelezwa kwa hukumu yao baada ya kukidhi kwa matakwa ya sheria kabla ya utekelezwaji wa hukumu hiyo.

Mwaka huo wa 2015 kulikuwa na watu waliohukumiwa kunyongwa wapatao 472 na kati ya hao wanaume walikuwa ni 452 na wanawake walikuwa ni 20 tu.

Tofauti hii ni kubwa sana ukiangalia uwiano kati ya wanaume na wanawake waliohukumiwa kunyongwa kwa mwaka huo wa 2015 hasa ukizingatia kwamba  kwa mujibu wa sensa idadi ya wanawake ni kubwa kuliko wanaume.

Je mnadhani kwamba wanaume ni katili kuliko wanawake?

Je ukatili huo unasababishwa na nini hasa?

Naomba wote tufikiri nje ya box maana kuna jambao ambalo kwa akili ya kawaida tunaweza tusilione.

Sina uhakika sana na makosa ya wanaume yaliyopelekea kuhukumiwa kunyongwa, lakini naamini miongoni mwao wapo waliohukumiwa kunyongwa kutokana na visa vya mapenzi.

Kama siyo wivu, basi inaweza kuwa ni katika kutafuta fursa kwa njia zisizo za halali ili kuweza kuwaridhisha wenzi wao au wapenzi wao.

Wote tunajua kwamba wanawake kwa ujumla wao wanavyo vibweka vyao katika swala zima la mapenzi, lakini ukija kwa wanaume naamini nao wanavyo vibweka vyao tena vya hatari ukilinganisha na vile vya wanawake.

Kwa mfano, hivi ni mara ngapi tumeshawahi kusikia baadhi ya wanaume wakiamua kujinyonga kwa sababu ya kushindwa kuwashawishi wanawake wanaowapenda? Hapa ni wale walioshindwa kuchukua maamuzi ya hatari dhidi ya binadamu wengine ili kuwaridhisha wanawake wanaowapenda.

Naamini kuwa matukio ya aina hiyo yapo sana na sio kwa hapa nchini tu bali pia hata katika nchi zilizoendelea. Linapokuja swala la mapenzi kuna baadhi ya wanaume wanakuwa kama Nyati waliojeruhiwa, na ndio sababu unaweza kukuta baadhi ya wanaume wanajiingiza kwenye vitendo viovu kama vile vya wizi au ujambazi kwa lengo la kuwashawishi wanawake wanaowapenda ili wawakubali.

Si kuwakubali tu bali pia kuwashawishi wasiwaache pale wanapokabiliwa na mgogoro wa kiuchumi.

Wote tunajua kwamba kila mwanaume anapenda kuonekana ni shujaa mbele ya mwanamke na ndiyo maaana mwanaume yuko tayari kuhatarisha maisha yake au hata ya wengine ikiwezekana hata kuuwa ili kuhakikisha anakuwa shujaa kwa mpenzi wake.

Tatizo hili ya wanaume kuhatarisha maisha au hata kupoteza maisha ni la tangu enzi za kale. Kuna simulizi nyingi tulikuwa tukisimuliwa enzi za utoto wangu huko nyumbani kwamba kuna wakati wanaume walikuwa wakipigana ili kumgombea mwanamke na shujaa anayeshinda katika ugomvi ndiye anayemchukua mwanamke anayegombewa.

Inaonekana wazi kwamba uwezekano wa mwanaume kufa mapema au kuhatarisha maisha yake ni mkubwa ukilinganisha na ule wa wanawake.

Na hiyo inatokana na wanaume kupenda sifa na kutaka kuwamiliki wanawake wawapendao. Kuna matukio mengi ya kusikitisha ambayo huwa tunayasoma katika vyombo vyetu vya habari ambapo matukio kama yale ya mwanaume kumuua mwanaume mwenzie ili kumpata mwanamke ampendae ni vya kawaida kabisa.

Ni aghalabu sana kusikia mwanamke kamuua mume baada ya kumfumania au kumuua mgoni wake tofauti na wanaume. Kama ukipima jambo hilo kitakwimu basi utapata idadi ya wanaume ya kutosha ukilinganisha na ile ya wanawake, na hii inathibitishwa na hiyo idadi ya wanaume wanaosubiri kutekelezwa kwa hukumu yao ya kunyongwa kwa mujibu wa takwimu hapo juu.

Kimsingi wanaume wamewageuza wanawake kama mali zao wanazozimiliki na hiyo ndio sababu inapotokea kumfumania mkewe au mchumba wake akiwa na mwanaume mwingine mambo mawili yanaweza kutokea, kwanza atamuadhibu mgoni wake au hata kumuua kisha mke naye atasulubiwa au hata kuuawa.

Lakini, pale anapofumaniwa mwanaume mambo huwa ni tofauti sana. Kuna uwezekano mkubwa wa mke huyo kusulubiwa kwa sababu amemfumania mume na wakati mwingine hata huyo mgoni anaweza kushirikiana na mume huyu kumuadhibu huyo mwanamke aliyefumania.

Nadhani kuna haja ya wanaume kujikagua upya na kubadili mwenendo wao mzima juu ya matendo yao ili kuepuka kupoteza maisha kwa jambo ambalo wangeweza kuliepuka.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags