Hili hapa chimbuko la jina Chaz Baba

Hili hapa chimbuko la jina Chaz Baba

Mwanamuziki wa Dansi nchini Charles Gabriel Mbwana 'Chaz Baba' amefunguka kuwa jina analotumia sasa ambalo watu wanalitambua alipewa na aliyewahi kuwa mwanamuziki nyota wa dansi, marehemu Ramadhani Masanja 'Banza Stone'.

Chaz ameyasema hayo wakati akizungumza na Mwananchi kwenye tamasha la Faraja ya Tasnia baada ya kuulizwa swali kuwa ni msanii gani aliyemgusa na kuweka wazi kuwa ni marehemu Banza Stone.

“Kama ulivyosema wote wamenigusa lakini aliyenigusa zaidi ni kaka yangu Banza Stone kwanza yeye kwa wasiojua mimi naingia Twanga Pepeta mwaka 2004 nilikuwa naitwa Charles Gabriel lakini baada ya kuingia ndani ya bendi Twanga nilivyoanza kufanya kazi kwa mara ya kwanza Banza alinibadili jina na kuniita Chaz Baba kutokana na uwezo wangu wa kazi.

"Najivunia kila mtu kuniita Chaz Baba lakini kinywa cha Banza ndio kilitoa hili jina kwa wasiojua hiyo nawapa exclusive” amesema Chaz Baba.

Mbali na hayo pia amezungumzia kuhusiana na ukuaji wa tasnia ya muziki wa dansi huku akiwataka wasanii wenzake katika muziki huo kukesha katika mitandao ya kijamii ili kusukuma muziki wao.

“Dansi imekuwa sana, imeamka kwanza dansi huwezi kuipoteza pengine labda uuliwe na wanamuziki wenyewe kwenye bendi lakini dansi ni mziki mkubwa na una mashabiki wengi sana. Nasema hivyo kwa maana moja, tumefanya tamasha Super Dom Masaki umeona muitikio pamoja na Twanga Pepeta tulivyojipanga.

"Kwa hiyo muziki nauona mbali sana tukiongeza kukesha katika mitandao ya kijamii. Tupeleke kazi zetu kwa wingi, nzuri, fupi na tamu tupambane katika mitandao yote ya kijamii na social network naamini tutatoboa,” alisema mwanamuziki huyo.

Licha ya kuwataka wasanii wenzake kutumia mitandao kusukuma kazi zao pia ametoa neno kwa baadhi ya wasanii wanaohama au kuanzisha bendi zao kujipanga kabla hawajafanya uamuzi wa kuondoka kwenye bendi fulani kwa kuanza na kuwa na vyombo vyake vya muziki vitakavyomuwezesha kusimama mwenyewe.

Hata hivyo amefunguka kuhusiana na maisha yake binafsi baada ya kuulizwa swali mwandishi kama ameoa au bado hajaoa ambapo amejibu kuwa yeye ni mume wa mtu na ana watoto watatu.

“Mimi ni mume wa mtu mke wangu ni Mkurya anaitwa Rehema Sospeter. Mimi ni mume wa mtu na nina watoto watatu ambao ni Jack, Carina na Carson,” amesema Chaz Baba.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags