Hakimiliki inazingatiwa wasanii kurudia nyimbo za zamani

Hakimiliki inazingatiwa wasanii kurudia nyimbo za zamani

Na Peter Akaro

Miaka ya hivi karibu imekuwa siyo jambo geni kusikia nyimbo mpya za Bongofleva zikiwa na vionjo vya nyimbo za kitambo, hilo limekuwa likitoa nafasi kwa nyimbo hizo kupendwa kwa haraka kutokana na umaarufu wa nyimbo za awali.

Hata hivyo, kumekuwepo na malalamiko kuwa baadhi ya wasanii hawafauti taratibu za hakimiliki pindi wanapochukua vionjo kutoka kwenye kazi za wasanii wenzao za kitambo.

Baadhi ya wasanii wa Bongofleva waliorudia nyimbo za zamani ni Vanessa Mdee (Jogoo la Shamba) wake Mbaraka Mwishehe, Rayvanny (Mapenzi ya Siri) wake Hussein Jumbe, Ben Paol (Lau Nafasi) wa kwao Kilwa Jazz Band.

Wengine ni Mwana FA (Yalaiti) wake Siti Binti Saad, Harmonize (Show Me the Way) wake Papa Wemba, P Mawenge (Wanangu) wake Marijani Rajab, Ben Pol (Sikukuu) wa kwao George Kinyonga na Orchestra Jabiso, Nandy (Indege) wa kwao Inafrika Band nk.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Utawala kutoka Taasisi ya Haki za Wasanii (TARO), Wakili Joshua Msambila amesema kifungu 5(2)(d) cha sheria ya Hakimiliki na hakishirikisho namba 7 ya 1999 kinalinda kazi ya muziki (mdundo, sauti na maneno).

Kifungu hicho kimeweka ulinzi kwenye mambo makuu manne muundo (form), kinachowasilishwa (expression), ubora (quality) na madhumuni ya kutengenezwa kwa kazi (Purpose of the work created).

Na kifungu cha 8 kinampa mmiliki haki za kiuchumi na kujivunia umiliki dhidi ya wengine, huku kifungu cha 9 kikitoa haki mbalimbali za kiuchumi kwa mmiliki wa hakimiliki ambazo ni usambazaji, kutumbuiza kazi na kuiwasilisha kwenye jamii kwa namna mbalimbali.

Mtayarishaji Muziki, Palla Midundo ambaye amekuwa akirudia kazi za wasanii wa zamani (sampling) katika mtindo wa Rap, amesema wasanii wengi wa zamani ambao baadhi wamefariki hawana hakimiliki ya kazi zao kutokana nyingi zilirekodiwa chini ya Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).

Ikumbukwe Palla ndiye ametayarisha kazi za ZaiiD na P Mawange ambao wamesampo nyimbo mbili za Marehemu Remmy Ongala ambazo ni Muziki Asili Yake Wapi na Fadhili. 

"Miziki mingi ya zamani ilirekodiwa RTD na kipindi kile walikuwa wakimaliza kurekodi na hizi Band wanalipwa na baadhi wanapewa posho, kwa hiyo umiliki wa ile miziki upo RTD japokuwa tunafahamu ameimba Marijani, Mbaraka, Bichuka au Maalim Ngurumu," amesema Palla.

 

"Tukisoma historia ya utamaduni wa Rap chimbuko lake lilikuwa ni kufanya 'sampling', kwa kule Marekani Ma'DJ walikuwa wanafanya hivyo (breakdance) kuzalisha midundo ya Rap. Ndicho nilichokifanya kwa hapa Tanzania kwa sababu tuna miziki yetu ya zamani tunaweza kuitumia," amesema Palla Midundo.

Msanii mkongwe wa Bongofleva, Squeezer ambaye wimbo wake, Bachela ulichukuliwa vionjo na Harmonize kuvitumia katika ngoma yake, 'Wife' akimshirikisha Lady Jaydee, amesema wasanii wa sasa hawapaswi kuchukulia vitu kwa urahisi huo.

"Wanatakiwa kujua wenzao waligharamikia muda na fedha, na muziki ni hazina ya mtu, wanachukulia kirahisi tunafanya wimbo wa huyu sasa hivi atakuwa machokoroni huko, hana lolote akija hapa nitamtuliza na milioni 1 au milioni 2, au nitamdanganya," amesema Squeezer.

Kuhusu iwapo kuna makubaliano kati yake na Harmonize hadi kutumia vionjo vya wimbo wake huo, Squeezer amesema suala hilo ni binafsi na atamalizana naye maana akiongea italeta taharuki!.

"Naomba iwe binafsi kidogo kwa sababu inaweza kuzua taharuki ambayo siitaki na halafu sio maisha yangu hayo ya kiki, kuna madogo hao wenyewe ndio maisha yao, hilo nitalimaliza mimi kama mimi," amesema Squeezer .

Prodyuza Palla Midundo amesema baadhi ya 'sampling' ambazo amefanya, kwa mfano ya Remmy, aliwatafuta watoto wake lakini kukawa na ugumu kwa sababu kuna baadhi ya miziki na wao walisema wanataka wairudie.

"Kipindi cha nyuma kuna moja niliwahi kutumia ya Maalim Ngurumu na niliwasiliana naye na kuna baadhi sijakubaliana nao kwa sababu wametangulia mbele za haki na zile Band hazipo. Pia kuna aina ya kutumia 'sampling' na watu wasijue hadi wewe useme, hivyo unaomba kibali cha kuitumia," amesema Prodyuza Palla Midundo.

Kuhusu wasanii kutumia vionjo wa nyimbo za wenzao bila kufuata taratibu, wakili Msambila kutokea Taro amesema kifungu cha 11 cha sheria ya hakimiliki na hakishirikishi kimempa mmliki wa hakimiliki haki ya zuio au kudai fidia kama kazi yake itatengenezwa tena na kuaribiwa.

Amesema mabadiliko ya sheria namba 3 ya mwaka 2019 yameongeza kifungu cha 15A kwenye sheria ya hakimiliki na hakishirikishi kinachosema; mtu yeyote anayetaka kutumia kazi inayolindwa na hakimiliki lazima aombe ruhusu kwa mmiliki.

Kifungu cha 36, kinampa mmiliki wa hakimiliki haki ya kufungua kesi kudai fidia au zuio kama atahisi hakimiliki zake zinavunjwa au vinataka kuvunjwa.

Amesema mabadiliko ya sheria namba 3 ya 2019 yamebadilisha kifungu 42(1)(a)(b) kwa kweka adhabu za faini zisizopungua milion 20, kifungo sio chini ya miezi 6 na sio zaidi ya mwaka mmoja kwa kosa la mara ya kwanza. Na faini zisizopungua milion 30, kifungo kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miaka 5 endapo kosa litajirudia kwa mara ya pili.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags