Gynah: Mwanamuziki Anaye Enjoy kufanya Live Perfomance

Gynah: Mwanamuziki Anaye Enjoy kufanya Live Perfomance

Najua kuwa neno kipaji si jina geni masikioni mwako ila mimi leo nakujuza kuwa ni uwezo wa kuzaliwa nao mtu wa kufanya jambo fulani kwa ngazi ya juu bila kufundishwa au baada ya kufundishwa kidogo tu.

Kipaji hiki kinaweza kuwa cha kimwili au cha kiakili lakini pia kinaweza kuendelezwa au kudumazwa.

Regina Kihwele maarufu kama Gynah binti aliyejaaliwa kuwa na kipaji zaidi ya kimoja ambapo ni mwimbaji, mwanamitindo na muigizaji.

Gynah licha ya kujishughulisha na biashara mbalimbali lakini pia amekuwa akiamini vipaji hivyo vitatu alivyojaaliwa na Mungu ni sehemu ya biashara tosha ya yeye kujiingizia kipato.

Mwishoni mwa wiki, Gynah alifanya onesho kubwa hapa jijini Dar es Salaam aliloliita Kahawa Night ambapo huko aliweza kuzindua  Extended Playlist (EP) yake pamoja na kuonesha mavazi.

Akizungumza na MwananchiScoop, Gynah afunguka na kusema anapenda sana kuperfom live ili mashabiki zake wapate radha bora ya muziki.

“Napenda kuimba hasa kufanya live performance kwani nina amini kuwa kwa kufanya hivyo watu upata kile kilichobora, hata hivyo  nimekuwa nikiwapenda Sauti Soul kutokana na aina ya muziki wanaoufanya.

“Pia licha ya kufanya kazi nina amini vipaji vyangu hivi nilivyojaaliwa na Mungu ni biashara tosha ya kuweza kuniingizia kipato na kujikwamua na maisha,” alisema

Kuhusu mitindo

Alisisitiza kuwa yeye ni mwanamuziki, mwigizaji lakini pia ni mwanamitindo na amekuwa akipenda mitindo tangu mdogo ila alikuwa akitaniwa kuwa ni bonge hivyo hatoweza kutimiza azma yake hiyo.

Gynah alisema kwa sasa mwili wake umekaa vizuri na amekuwa akiifanya kazi hiyo kwa bidii na juhudi kubwa kwani anaamini muziki na uigizaji unategemea pia mitindo mbalimbali ya mavazi.

Alisema moja ya changamoto anayokumbana nayo katika masuala ya mitindo ni mafundi wamekuwa wakiharibu nguo au kushindwa kumaliza kazi za wateja kwa wakati.

“Katika kazi hii ina changamoto kwa mafundi nah ii inatukumba sisi ambao hatuwezi kushona nguo ila tunaendelea kupambana tu, hata hivyo katika haya mambo nimekuwa nikimuangalia Mustapha Hasanali amekuwa akifanya vizuri sana hivyo ninamkubali na nikimuangalia ninasema ipo siku moja nami nitakuwa kama yeye,” anasema

Kuhusu uzinduzi wa EP yake na Kahawa Night

Alisema amekuwa akifanya shoo yake aliyoipatia jina hilo la Kahawa Night ni kwa sababu anakipenda kinywaji hicho na aliona inafaha kulipatia jina hilo.

“Kupitia Kahawa Night tumefanya onesho la mavazi pamoja na kuzindua EP yangu ambayo ina jumla ya nyimbo nane, nina imani mashabiki zangu yatazifurahia kazi nilizowaandalia,” alisema

Ushauri

Hata hivyo amewataka wasanii wachanga hasa wa kike kuendelea kupambana kwani industry hiyo ni ngumu kutoboa kama mtu hana malengo na amekosa kujiamini

Mama mzazi azungumza

Mzazi ni mtu wa kwanza anayeweza kutambua uwezo ama kipaji cha mtoto wake. Hata hivyo ana fursa ya kuendeleza au kutokukiendeleza kipaji cha mtoto.

Baadhi ya wazazi hutambua vipaji vya watoto mapema na kuanza kuviendeleza kwa kuwapatia nyenzo mbali mbali ambazo huwasaidia katika kuboresha uwezo walio nao.

Lakini pia wapo wazazi ambao wanamalengo yao juu ya ni kitu gani wanapenda watoto wao wafanye. Ama yamkini hawana ufahamu wa nini cha kufanya ili kumwendeleza mtoto mwenye kipaji.

Hata hivyo vipo baadhi ya vipaji ambavyo baadhi ya wazazi huona ni upotevu tu wa maadili mfano kuimba na kucheza mziki lakini dhana hiyo ni tofauti kwa Lucy Ngongoseke ambaye ni mama mzazi wa Gynah.

Mama Lucy alisema aligundua vipaji vya mwanaye na kuanza kumsapoti huku akimpa moyo kila wakati na kila saa.

Hata hivyo Lucy alisema wazazi wanapaswa kutowazuia watoto pindi wanapoonesha vipaji vyao badala yake waviendeleze kwa manufaa yao na ustawi wa jamii.

Alisema mtoto wake amekuwa akiimba, kuigiza na ubunifu wa mavazi licha ya kwamba anatambua kuwa sio kazi rahisi kufanya yote hayo lakini ameweza kwa sababu ndivyo anavyopenda kufanya.

“Yeye hivyo vitu vyote anavipenda na amekuwa akifanya vizuri hadi kufanikiwa kuingia katika kinyanganyiro cha tuzo ya mwigizaji bora wa kike ukanda wa Afrika zilizoandaliwa na Lake Internationl Pan Afrika Awards ambazo zitafanyika Novembar 3 Mwaka huu huko Nairobi, Kenya,” alisema

Basata wanena

Naye Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Ibrahim Ibegwe alisema kuwa ameguswa na binti huyo kwa kuwa amedhihirisha kuwa ni sehemu ya wadau wa Sanaa na ameonesha kuwa atafika mbali katika tasnia hiyo.

“Nimeona anavipaji vingi cha kuimba, ubunifu wa mitindo na uingizaji, amekuwa mashuhuli baada pia ya kushiriki katika filamu ya Mlasa na kuchagulishwa kwenye tuzo, moyo wangu unaniambia kuwa atafika mbali,” alisema

Aidha alisema katika kuhakikisha Sanaa inakua, baraza hilo limekuja na mfumo wa kusajili kidigitali                                                                                                                                                                                                                                                                                  ambao unalenga kurahisisha utoaji wa huduma za usajili kwa wadau wake wote muhimu.

Ibegwe alisema usajili huo wa kidigitali kwa sasa utamtaka mtu aliyeko mkoani badala ya kutuma nyaraka zake kuja Dar es Salaam sasa atalazimika kuingia katika mtandao na kujisajili huko.

“Usajili wa kidigitali ni rahisi sana, mtu anayehitaji kusajiliwa na Basata ambaye yupo mkoani hata yule ambaye yupo Dar es Salaam badala ya kuja ofisi za Basata sasa atatumia mtandao wake kuingiza nyaraka muhimu kisha kupata namba ya serikali ya kulipia na hatimaye kupata cheti chake,” alisema

Alisema bado baraza hilo linaendelea kutoa elimu kwa wadau wao wote muhimu juu ya namna ya kujisajili mtandaoni ili kupunguza changamoto walizokuwa wakikumbana nazo.

Aidha alisema baraza hilo litakuwa na mikutano maalum ya kila mwaka yenye lengo kupokea maoni na mapendekezo ya namna bora ya kuendesha shughuli za sanaa hapa nchini.

Amesema mkutano huo utakutanisha wadau wote muhimu kwa maana ya kwamba wasanii kutoka mashirikisho ya sanaa manne ambayo ni Sanaa za ufundi, muziki, maonyesho na filamu.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags