Gharama kubwa chanzo mastaa kukwepa Official video

Gharama kubwa chanzo mastaa kukwepa Official video

Kiwanda cha Bongo Fleva nchini kimeendelea kubadilika kila kukicha zile zama za kufanya video za nyimbo zao kwa (Madiba) Afrika Kusini hazipo tena. Kwa sasa wengi wamejikita kufanya video zenye kuonesha mtindo wa kucheza nyimbo husika (Dancing Video) tofauti na ilivyokuwa awali wasanii kuachia video rasmi ya wimbo.

Utakumbuka kuwa zamani wasanii walikuwa wakiachia video rasmi ya wimbo muda mfupi baada ya kutoa audio. Awali wengi walianza na kufanya matangazo ya nyimbo zao kwa kutoa video zenye maneno 'Lyrics video',lakini kwa sasa wanaonekana kuhamia kwenye mtindo huo wa video zenye kuelekeza namna ya kucheza wimbo.

Kutokana na mabadiliko hayo yamekuwa yakizua mkanganyiko kwa baadhi ya wadau wa muziki kwa kudai kuwa kwa kufaya hivyo kunapelekea video rasmi za nyimbo kutofanya vizuri pindi zitolewapo. Huku kwa upande wa wasanii wanadai mbinu hiyo ndiyo njia bora ya kuwafikia mashabiki.

Utoaji wa video za aina hiyo unaweza kuthibitishwa na mwanamuziki Alikiba ambaye Julai 3 aliachia 'Dancing video' ya wimbo wake mpya aliyomshirikisha Billnass iitwayo ‘Fallen Angel’.

Kutokana na hayo mwanamuziki Freddy Benny ‘Msamiati’ ameeleza kuwa wasanii wengi wanatumia njia hiyo kutangaza nyimbo kutokana na kukwepa gharama za kufanya video rasmi.

“Kwa asilimia fulani tunaweza kusema wanakwepa gharama kwa sababu muziki umekuwa sana, zamani wasanii walikuwa wanawekeza sana kwenye 'promotion' ya nyimbo, ila sasa wasanii tunawekeza kwenye audio.

"Sasa ukiwekeza kwenye audio maana yake msanii lazima uwe mjanja kuweza kuhakikisha unawafikia mashabiki zako, na hapo ndipo unakuta msanii unaamua kufanya video challenge ili mashabiki waweze ku-enjoy muziki. Siku hizi mitandao ya kijamii imechukua sehemu kubwa ya mashabiki.

"Kwa hiyo, wasanii wengi hawatumii tena muda wao kutengeneza official video kutokana na kugharimu vitu vingi, kuanzia story na vitu vingine, ila kwa kufanya dancing video inakuwa rahisi kwa sababu unakuwa moja kwa moja na mashabiki zako,” amesema Msamiati

Naye Director Deo Abel amesisitiza kuwa kufanya official video ni gharama na ndiyo maana wasanii wengi wamehamia kwenye ‘Dancing video challenge’.

“Kweli kufanya official video kunakuwa na gharama, kwa sababu lazima uandae production ya kutosha, ma-model, set na vitu vingine vingi ila kwa ‘Dancing challenge video’ inakuwa ni kitu ambacho hakina gharama kubwa,"amesema

Aidha aliongezea kuwa wasanii wengi wanaamua kufanya hivyo kwa ajili ya kuupeleka muziki wa Tanzania kutambulika zaidi mfano dance challenge ya Diamond ilivyochezwa na Chris Brown

Hata hivyo alifafanua kuwa baadhi ya wasanii wamekuwa wakitumia simu kurekodi video kutokana na kutokuwa pesa ya kutosha huku akiweka wazi kuwa katika dance challenge kuna changamoto zake kwani Dance challenge ikifanya vizuri kuna uwezekano mkubwa official video isipokelewe kwa ukubwa ule.

Aidha kwa upande wa Meneja Made ambaye anamsimamia mwanamuziki ‘Lody Music’ amesisitiza kuwa wasanii wanakwepa kutoa official video kutokana na kukosa 'sapoti'.

“Naweza kusema wasanii wanakwepa kutoa official video kwa sababu ya gharama lakini lipo jambo la kukosa mashirika au kampuni kubwa za kuwasimamia ili waweze kupata video zenye ubora ukija kwenye upande wa video kwa sasa soko, linaushindani mkubwa wasanii wakubwa na walio kwenye label kubwa wana-shoot video 1 mpaka million 50 ukija kwa msanii wa kawaida ni ngumu kupata hiko kiasi unaamua bora afanye video lyrics au video visuals ili kuepuka gharama” amesema Meneja wa Lody Music


Pia ameiomba Serikali kuwasaidia wasimamizi wa wasanii kupatiwa mikopo mikubwa ili waweze kuwasimamia wasanii wao kutoa kazi na mastaa wa muziki kutoka mataifa tofauti ili kukuza muziki wa Tanzania.


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post