From waste to worth: A young lady using waste to make beauty products speaks!

From waste to worth: A young lady using waste to make beauty products speaks!

HERENI, bangili na cheni ni moja ya mapambo yanayovaliwa sana na wanawake na kwa kiasi kikubwa yanachangia kuongeza mvuto na muonekano mzuri kwa mtu.

Kuna aina nyingi za hereni, cheni na bangili katika tamaduni mbalimbali. zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia vito vya thamani kama vile dhahabu, Almasi, Shaba au Kopa, vilevile zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia malighafi za asili kama vile ubao, vifuu vya nazi, mifupa, kioo na shanga ambazo zimekuwa zikivaliwa sana na wanawake wa kimasai.

Kwa kutambua umuhimu wa urembo katika biashara, kijana Mariam Hamis (20) anatumia malighafi ya karatasi ngumu kutengeneza mapambo mbalimbali ikiwemo hereni, mikufu na bangili za kuvaa mikononi na shingoni.

Mariam ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Vijana la Adoado, lililopo Tabata jijini Dar es Salaam, kwa sasa ameamua kujiajiri kwa kutengeneza hereni, bangili na cheni kwa kutumia karatasi ngumu jambo ambalo kwa mtu wa kawaida anaweza kushangaa.

Historia yake inaweza kuwa ya kufurahisha na ya kuhamasisha kwakuwa Mariam anasema alianza kutengeneza urembo huo mwaka 2012 wakati akiwa kidato cha pili, katika Shule ya Sekondari Migombani, iliyopo Ilala.

Aliweza kujua kutengeneza hereni, cheni na bangili kwa kutumia karatasi baada ya kujifunza kutoka kwa mama yake mzazi ambaye ndiye aliyekuwa akiifanya kazi hiyo.

“Nimeanza kuifanya kazi hii tangu nikiwa kidato cha pili na nilifanikiwa kujua mapema baada ya kuwa makini wakati mama yangu anatengeneza, muda mwingi niliutumia kumsaidia kazi zake mpaka nilipoelewa jinsi anavyofanya,” alisema.

Mariam aliongeza kuwa, “Nilipomaliza shule ya Sekondari nilifaulu kwenda kusoma uwalimu lakini sikuupenda kwa kuwa nilitamani kuwa mwanasheria, hivyo, nikajikuta nikiangukia kwenye ujasiriamali wa kutengeneza urembo.”

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kazi hiyo anayoifanya ni ya kurithi kutoka kwa mama yake ambaye aliisomea, na yeye akawafundisha watoto wake ambao na wao wamekuwa walimu kwa vijana wengine wanaopenda kuifanya kazi hiyo.

 

 

Jinsi anavyotengeneza urembo huo

Biashara hii imekuwa yenye upekee sana, kwani ni mara chache kukutana na watu wanaoweza kuwa na ubunifu wa ziada kama Mariam na mama yake.

Malighafi Mariam anazotumia kutengeneza mapambo hayo ni karatasi ngumu, rula, gundi ya maji, kisu na vanishi inayotumika kung’arisha.

“Malighafi nyingine kama vyuma vya kuning’inizia hereni, shanga na viungio vya mikufu, nanunua kwenye maduka ya urembo wa asili yaliyopo Kariakoo,” alisema.

Vilevile amekuwa akikusanya kalenda zilizokwisha muda wake au vitabu mbalimbali vilivyochakaa ambavyo ndivyo anavitumia katika utengenezaji wa mapambo hayo ya wanawake.

“Nikienda kwenye maonesho au mikutano mbalimbali mikubwa nimekuwa nikiokota na kukusanya vipeperushi vinavyokuwapo mahali pale na kuvihifadhi kwa ajili ya kazi zangu za urembo,” aliongeza.

Akielezea namna utengenezaji wa urembo huyo unafanyika, alisema huwa anachukua karatasi hiyo ngumu na kuanza kuikunja kwa rula kisha huzikata kwa kutumia kisu au mkasi kwa mtindo wa kupishanisha.

“Baada ya hapo huwa ninazikunja hizo karatasi kwa umakini mkubwa kisha nazipaka gundi, nikimaliza naingiza mshipi imara na kupaka vanishi ya kung’arisha, na kuweka kwenye sehemu nzuri ipigwe na upepo,” alisema.

Zoezi la kutengeneza urembo huo huchukua muda wa siku mbili na kuongeza kuwa vifundo cha karatasi vikikauka, anakuwa na kazi moja ya kuunda mkufu wa shingoni au hereni.

Pamoja na mafanikio anayoyapata kupitia biashara hiyo, Mariam hajawa mchoyo, amekuwa akiwaita vijana wenzake kwa lengo la kuwafundisha utengenezaji wa mapambo hayo lakini wakija na kujifunza kwa siku moja, wengi hukata tamaa na kudai kazi ni ngumu.

“Nimeshawaita baadhi ya vijana niweze kuwafundisha lakini wakija wakijifunza siku moja wanasema kazi ngumu na wanaacha, nawakuta vijiweni wamekaa bila kazi yoyote,” anasema.

 

 

 

 

Kuhusu masoko

Binti huyo alibainisha kuwa soko la bidhaa hizo lipo na mara nyingi amekuwa akiyatumia matamasha, mikutano, pamoja na maonesho mbalimbali kuuza bidhaa zake hizo.

“Soko lililopo bado si kubwa sana ila linalipa kwani wateja wangu wengi huwa ni raia wa kigeni, na bei ya mkufu, hereni zake na bangili naziuza kati ya tshs 40,000 hadi tshs 50,000, wakati kwa watanzania ni tshs 10,000 hadi tshs 15,000,” aliongeza.

Malengo yake

Kijana huyu amethubutbu na ametia nia kufika malengo yake ya kuwa mjasiriamali mkubwa katika masuala ya utengenezaji wa mapambo hasa ya asili na mengine, kwani ni jambo analolipenda katika maisha yake.

“Niwaambie vijana wenzangu mtaji wa hii kazi wala sio mkubwa. Unaweza kuanza na kiasi cha tshs 50,000 tu, mimi nilishawahi kwenda kwenye onesho moja, wazungu walikuwa wengi, niliuza bidhaa zangu na kurudi nyumbani na tshs 650, 000,” Mariam alinena. 

Changamoto ya biashara hii

Kati ya changamoto ambazo Mariam anakumbana nazo ni kukosa masoko ya uhakika wa bidhaa zake pamoja, na baadhi ya watu wakiwemo vijana wenzake kumkatisha tamaa.

“Vijana wenzangu wamekuwa wakinikatisha tamaa kwa kuniambia kuwa nitamuuzia nani bidhaa zangu, kwani watu hawavai mikufu ya asili bali wanavaa dhahabu na almasi, hii ni moja ya changamoto ninayokumbana nayo ila nashukuru Mungu naweza kuikabili,” Mariam alisema.

Anavyojengewa uwezo

Mariam na Jukwaa la Vijana la Adoado ni miongoni mwa majukwaa 37 ya vijana yaliyoanzishwa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala ya kijamii (CAFLO) kwa lengo la kuwainua kiuchumi vijana.

Mratibu wa Miradi wa CAFLO, Emmanuel Ngazi aliiambia InstaScoop kuwa Mariam amekuwa ni kati ya vijana wanaofanya vizuri katika masuala ya ujasirimali, hasa wa utengenezaji wa bidhaa za urembo.

Aidha aliongeza kuwa mijadala elimishi na makongamano wanayoyaandaa chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) yameleta mabadiliko kwa vijana ambao wengi wao kwa sasa wamepata mikopo ya kuanzishia biashara kutoka kwa halmashauri.

"Hivi sasa kuna muamko mkubwa sana wa vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi, tofauti na zamani. Majukwaa yamewajengea ujasiri na uwezo mkubwa wa kufikiria mambo ya kimaendeleo," alisema

 Kwa juhudi na ubunifu wa Mariam, ameweza kujiingizia kipato kupitia biashara ambayo wengine  hawakuifikiria. Wewe kijana pia una nafasi kubwa ya kuweza kujiendeleza endapo utatumia ubiunifu uliokuwa nao, kujiendeleza. Mariam ni moja kati ya mifano hai ya kuigwa na wewe kijana ili kujikwamua kiuchumi.

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post