Kawanda cha muziki wa Hip-hop nchini kimebarikiwa kuwa na wasanii wengi wanaofanya kazi kwa kujitegemea. Lakini pia kuna makundi kadhaa ya muziki huo ambayo yamekuwa yakifanya vizuri kama vile Fresh Boys.
Hilo ni moja ya kundi la muziki huo linaloundwa na Gran Geez, 10k Degrees, 6ixtoogood na Tboymill. kundi hilo limekuwa na mapokezi makubwa kwa mashabiki hususani wale wanaotokea mtaani, hii ni kutokana na nyimbo ambazo wamekuwa wakiziimba.
Kundi hilo ambalo lipo chini ya label ya Iam Music ya kwake Ibrahim Mandingo 'Country Boy' tangu 2023, tayari limeachia mikwaju kama Maana Ake Nini, Kiu, Vitasa, STATEMENT, Vitasa, Emoji, Tupa Kule (Ghetto), Ileile na Usawa Huu.
Wiki hii Mwananchi Scoop imepiga story na kundi hilo mazungumzo yalikuwa hivi…
Mnadhani nini chanzo, majina yenu mmoja mmoja kutotambulika kwa mashabiki?
"Kwanza sisi hatujaweka nguvu kutambulika msanii mmoja mmoja tumeweka nguvu kutambulika kama kundi ndiyo maana hata watu ni ngumu kututambua sisi kama sisi" amesema Gran Geez.
Inasemekana label yenu ina mchango mdogo kwenu, ni kweli?
"Wanasema mara nyingi kitu ambacho unakuwa unakiona kwa nje hujui kwa ndani ni ngumu kuzungumzia taarifa zake. Lakini sisi maadili yetu ya kufanya kazi na Contry ni tofauti na watu wengi wanavyodhani.
“ Ni kweli tupo chini ya Iam Music lakini tumepewa uhuru wa kufanya kitu ambacho tunakitaka kwa uwezo wetu na mwendo wetu ndiyo maana tukitaka kuachia dude tunaachia,"amesema 6ixtoogood.
Fresh Boys mnajiona kuwa pamoja kwenye safari ya muziki kwa muda gani?
"Sisi kabla ya kuwa Fresh Boys tulikuwa tunajuana kama ndugu tu, lakini pia tulikaa mwaka mzima bila kutoa wimbo tulikuwa tunaelekezwa na kaka zetu kina ConBoy, Salmin Swaggs kila siku tukikutana nao wanatupa ushauri na kuna vitu vingi tunajifunza.
“Ukizingatia pia sisi ni vijana wadogo kabisa na tuna pambana kwahiyo kwa sasahivi ni ngumu kuvunjika kwa kundi kwa sababu ndio bado tunajitengeneza" amesema Tboymills.
10k Degrees nini kinakupa utofauti kwenye ngoma zeni?
"Kiukweli sikujua kama itakuwa hivi, ilivyo kwa sababu mimi naweza kutumia sauti yangu kwenye kuimbia na kurap ila napendelea zaidi kutumia bezi kwa sababu inanipa utofauti.
“Haikunichukua muda mwingi kujitengeneza na watu wanapenda utofauti na bidhaa adimu inapendwa sokoni lakini watu wangu wa karibu ndio wamechangia zaidi kunipa ushauri kuwa hii kitu ni nzuri "amesema 10k Degrees.
Aina gani ya uandishi mnapenda kuitumia?
"Kiujumla sisi huwa tunaandika pamoja Geez anaweza kuandika verse yangu, mimi nikaandika ya 6ix, kisha tukaunga na ngoma ikawa kali na usijue. " amesema 10k Degreez.
Nini siri ya mashairi yenu?
"Unajua hip-hop ni kuelezea maisha halisi kwa hiyo sisi tunapenda kuisha uhalisia ambao sisi tunaisha na wanaisha watu wengi wa mtaani ndiyo maana inakuwa ni rahisi sana kwetu kupata maudhui ya namna hiyo na mapokezi mazuri ya mtaani. Watu wanakuwa wanaona kama tunawawakilisha," amesema Gran Geez.
Kwanini hamna ngoma na boss wengu Country?
"Nadhani sijui naweza sema ni ratiba lakini pia hatukutaka kuonekana tunabebwa na Country mtu akisikia ngoma tupo na Wizzy anaweza kuona kama tumebebwa.
“Kwa hiyo tunajipa muda twende sisi kama sisi watu waamini kile kitu ambacho tunacho alafu tukija kufanya ngoma na Wizzy waone ok hiki ndio tulikuwa tunakisubiria," amesema Gran geez.
Mmejipanga vipi kwa mwaka 2025?
"Kwanza kabisa tumetoa ngoma mpya inaitwa ‘Usawa Huu’ ipo YouTube wakaifatilie lakini mwezi huu pia tunatoa wimbo mwingine na mwezi ujao kama kawa kwahiyo watu waendelee kuwa karibu " amesema Tboy Mills.

Leave a Reply