Na Glorian Sulle,
Dar es Salaam. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia sekta ya burudani inaendelea kuzalisha ajira kila kukicha huku ikirahisisha baadhi ya mambo kufanyika kwa wepesi tofauti na ilivyokuwa awali.
Kutokana na maendeleo hayo watu wengi wameendelea kujipatia kipato kupitia vipaji vyao vya kutafsiri filamu kutoka lugha moja hadi nyingine (Dubbing).
Baadhi ya tamthilia nchini ambazo zimekuwa zikipitishwa katika mchakato huo na kuwekwa kwenye Lugha ya Kiswahili licha ya kuwa siyo filamu za Tanzania ni pamoja na Golden Boy, Alparslan, Sultan, Husband Family, The City zinazoonesha kwenye visimbuzi mbalimbali.
Awali tamthilia hizo za kigeni zilikuwa zikirushwa bila kutafsiriwa jambo lililofanya kupata wafuatiliaji wachache kutokana na wengi kutofahamu lugha za kigeni.
Lakini baada ya tamthilia hizo kutafsiriwa kwa sauti zimeanza kufanya vizuri siku hadi siku huku zikileta ushindani mkubwa katika soko la tamthilia la ndani.
Akizungumza na Mwananchi, Mkama Khamis, aliyewahi kuigiza uhusika wa sauti ya “Shivan” kwenye Tamthilia ya ‘The City’ amesema kazi za kutafsiri sauti imemsaidia kutoka kimaisha.
“Safari yangu ya kutafsiri sauti nilianza rasmi mwaka 2021 katika Tamthilia ya ‘The City’ nilivaa uhusika wa “Shivan” kazi hii ilinisaidia sana maana nilikuwa sina kazi yoyote baada ya kumaliza chuo,” amesema
Khamis akieleza kwamba baada ya kubobea katika kazi hiyo imemsaidia kutoka hatua moja kwenda nyingine kimaisha na ndiyo kazi pekee anayoitegemea.
Aidha, Prisca Nkyo msanii wa kutafsiri sauti anayefanya kazi chini ya Kampuni ya Pilipili inayohusu kutafsiri tamthilia mbalimbali zinazorushwa DSTV pamoja na Star Times amesema safari yake katika fani hiyo ilianza rasmi miaka mitatu iliyopita.
Msanii huyo anayevaa uhusika wa “Tamara” katika Tamthilia ya “Mpali" inayorushwa Maisha Magic Bongo ameeleza faida anazopata katika tasnia hiyo.
“Ukiachana na faida za pesa lakini pia nimefikia lengo langu la kuitumia sauti yangu kwa njia mbalimbali ukiachana na ile ya utangazaji,” amesema.
Naye Mzome wa Mzome ambaye wengi wanamfahamu kama Kazim Agah, jina la mwigizaji wa Uturuki aliyecheza kwenye Tamthilia ya The Golden Boy amesema anajivunia kupitia sanaa yake tangu alipoanza kwenye Kipindi cha ‘Jambo na Vijambo’ hadi sasa kwenye udurufishaju sauti (Dubbing).
“Nilivyoingia kwenye 'dubbing' ndiyo nimezidi kupata umaarufu sana na kukusanya maokoto kuliko hata kwenye kipindi chetu cha ‘Jambo na Vijambo’ ambacho kwa sasa kimesimama kwa muda,” anasema Mzome na kubainisha changamoto anazokumbana nazo katika kazi yake hiyo.
“Japo kuna muda kama binaadamu lazima kuwe na changamoto pia, kama kupata matatizo ya kiafya mfano mafua na kukohoa hivyo vinakuondoa kwenye ‘mudi’ kabisa ya kuvaa uhusika kwa muda huo lakini hainipi shida nikiona hivyo najipumzisha kidogo kisha naendelea.
“Mfano kwenye Tamthilia ya The Golden Boy uhusika niliopewa wa Kazim Agah ni mtu ambaye anaongea sana so muda mwingi anaongea kunakuwa hakuna majibizano hivyo inakuwa ngumu na mara nyingi huwa kinanisumbua kifua kwa sababu muda mrefu naongea.”
Hata hivyo wasanii hao wameeleza baadhi ya changamoto wanazokutana nazo katika tasnia hiyo huku uchache wa kazi wakitaja kama kero kubwa.
Aidha wameeleza kuwa tasnia hiyo inategemewa na vijana wengi na pengine ikisimamiwa vizuri itapunguza tatizo la ajira kwa baadhi ya vijana wenye vipaji hapa nchini.
Leave a Reply