Faraja ya Tasnia ni zaidi ya tamasha, mastaa wanyoosha mikono juu

Faraja ya Tasnia ni zaidi ya tamasha, mastaa wanyoosha mikono juu

Mastaa mbalimbali nchini waliofika kwenye tamasha la Faraja ya Tasnia linalolenga kuwaenzi wasanii waliofariki dunia, wameonesha kuvutiwa na tamasha hilo ambalo limeanzishwa na mwigizaji Steve Nyerere.

Ikiwa ndiyo kwa mara ya kwanza limeanza nchini na kufanyika leo Septemba 7, katika viwanja vya Leaders Club mwigizaji wa vichekesho Lucas Lazaro 'Joti' amesema amefarijika na kufurahi baada ya kuona picha ya aliyekuwa mwigizaji Alhaji Amri 'Mzee Majuto' katika tamasha hilo.

“Kwa kumuona mmoja kati ya wasanii nguli baba yangu (Mzee Majuto), nimefarijika sana lakini pia nimefarijika kuwaona baadhi ya wasanii wengine ambao nimewahi kufanya nao kazi.

“Uzuri King Majuto nishafanya naye kazi Mama Abduli, Kanumba, kina Korongo na wengine wengi kwa hiyo mimi najisikia faraja sana na hii itaweka historia kubwa sana katika tasnia yetu,” amesema Joti

Naye Masatu Ndaro 'Mjeshi Kikofia' ambaye pia ni mchekeshaji amesema tamasha hilo linakumbusha watu kuwa siyo siku zote watakuwepo duniani.

“Tamasha hili litaendelea kuwepo kwa sababu kama tumeweza kuungana kwa pamoja tukatengeneza hili kesho na kesho kutwa hata kama sisi tukiondoka wanaokuja inabidi wajifunze kupitia tulichokifanya sisi,” amesema Ndaro.

Hata hivyo mwigizaji mkongwe nchini Ahmed Olotu, 'Mzee Chillo', hakuacha kumtaja aliyekuwa mwigizaji Steven Kanumba kwa kusema mpaka leo bado pengo la mwigizaji huyo halijazibika

Mbali na hao mwigizaji wa vichekesho Hemed Maliyaga 'Mkwele' amesema marehemu Max Makanda na Mzee Matata ni kati ya waliomvuta kusogea katika tamasha hilo



"Tumekutana na picha za wakongwe mbali mbali waliotuwakilisha wengi walipambana kwenye tasnia hii wazee wetu walifanya kama kujiburudisha lakini leo sisi tunafanya sanaa kama kazi tunapata kipato isingekuwa wao kulianzisha sisi tusingeweza kuiheshimu sanaa,"amesema

Huku kwa upande wa mwigizaji Chuchu Hans amesema katika tamasha hilo ameguswa na wazee waliokuwa wakimpa moyo wa kuongeza bidi.

“Wapo wengi walionigusa kuna Mzee Korongo, Mzee Majuto, Huda yaani kila mtu amenigusa kwa nafasi yake, kwa mfano kama King Majuto ni mtu ambaye ananijua tangia sijakuwa Chuchu Hans ni mtu ambaye alikuwa ananipa moyo.



"Nilikuwa nafarijika sana kufanya kazi naye anachekesha na Mzee Jengua ni mtu ambaye alikuwa ananikubali sana na nishawahi kufanya naye kazi ananipa moyo, kwahiyo hao ndio wazee walionipa nguvu zaidi yakuweza kuthubutu mpaka kufika hapa,” amesema Chuchu Hans

Ikumbukwe kuwa tamasha hilo limefanyika kwa mara ya kwanza nchini likihudhuriwa na mastaa mbalimbali huku kwa mujibu wa mwanzilishi wake Steve Nyerere aliiambia Mwananchi kuwa litakuwa endelevu hivyo litafanyika mara moja kila mwaka.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags