Fahamu visababishi na dalili za mtu mwenye Msongo wa Mawazo

Fahamu visababishi na dalili za mtu mwenye Msongo wa Mawazo

Mara nyingi sana umesikia mtu akisema “nina stress”, mwingine akasema ana msongo wa mawazo na mara chache katika mazungumzo ukasikia mtu akitumia neno mfadhaiko.

Haya ni maneno yanayoingiliana kimazungumzo mitaani na mara nyingi mtu hutumia neno moja katika hayo bila kujua tofauti zake.

Hata hivyo inaelezwa kuwa karibu watu milioni 450 duniani wanakabiliwa na tatizo la msongo wa mawazo, hali inayofanya wengi wao kupata matatizo ya kiafya.

Baadhi ya watu hao wanakabiliwa na wakati mgumu kutafuta matibabu kutokana na unyanyapaa unaohusishwa na matatizo ya kiakili.

Katika Makala yetu leo daktari atatueleza kwa kina tatizo hilo la msongo wa mawazo, visababishi vyake na namna ya kuweza kukabiliana nalo.

Dk. Rahel Mwinuka ni Daktari wa Magonjwa ya Binadamu kutoka Hospitali ya Anglikana iliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam alisema maisha ya dunia ya leo yamejaa pilikapilika za kila aina, kuna vitu vingi vya kuvifanya katika muda uliopangiwa (deadlines), vitu vingi vya kukukatisha tamaa na matakwa mengi ya binafsi na watu walio karibu na wewe.

Anasema mtindo huu wa kuishi umekuwa karibu ni wa kila mtu kwani kila wakati watu upatwa na msongo wa mawazo (Stress).

“Msongo wa mawazo kwa kiasi fulani siyo mbaya, unakusaidia kutekeleza majukumu yako ukiwa umebanwa na kukupa nguvu ya ziada ya kuyafanya vizuri kadiri ya uwezo wako.

“Lakini kama utaendelea kufanya shughuli zako kwa mtindo huu, wakati utafika ambapo ubongo wako utachoka na kupata tatizo la kiafya linaloitwa mfadhaiko (Depression),” anasema

Anasema msongo wa mawazo unaweza kumsaidia mtu kukabiliana na vikwazo mbalimbali.

“Utakuwa makini sana wakati unawasilisha mada mbele ya kadamnasi, utakuwa na umakini zaidi wakati unashiriki kwenye mechi na timu pinzani na utasukumwa kwenda kusoma ili ujiandae kwa mitihani yako badala ya kuangalia kipindi kizuri cha kwenye luninga unachokipenda,” anasema.

Anasema pamoja na hayo, kiwango cha msongo wa mawazo kikizidi, badala ya kumsaidia mtu kinamletea matatizo ya afya, kinaathiri utendaji wake wa kazi, kinavuruga mahusiano yake na wengine na kudunisha maendeleo ya maisha.

Visababishi Vya Msongo Wa mawazo

Dk. Mwinuka anasema kuna vitu vingi vya kimazingira au kimsukumo vinavyoweza kusababisha mtu kupata msongo wa mawazo.

Anasema jamii inapaswa kutambua kuwa Stress ni kitu chochote kinachodai matumizi ya juu ya uwezo na nguvu zako za mwili. Inawezekana kuwa kikawa kitu kizuri tu, kama kuoa/kuolewa, kununua nyumba, kujiandaa kwenda chuoni au hata kupandishwa cheo kazini.

 

“Msongo wa mawazo unaweza kutokana na fikra zako binafsi mbali na sababu hizo ambazo ni za nje ye mwili wako. Unaweza kuwa na msongo wa mawazo kutokana na kukifikiria na kukiogopa kitu ambacho kinaweza kutokea au ambacho hakiwezi kutokea au tu ukawa na mawazo chanya kuhusu maisha,” anasema

Anasema vitu ambavyo vinasababisha msongo wa mawazo ni pamoj na mabadiliko ya maisha, kazi au shule, matatizo katika mahusiano, matatizo ya kifedha, kubanwa na shughuli nyingi, watoto na familia.

Dk. Mwinuka anasema vitu vingine ni wasiwasi wa muda mrefu, tabia ya kuona kila kitu ni kibaya, kupenda yasiyowezekana, kutaka kila kitu kiwe sahihi (kikae juu ya mstari) kila wakati, kutopenda kushauriwa au kubadilika kutokana na hali halisi pamoja na kujidharau mwenyewe kwenye mazungumzo.

Dalili Za Kuwa Na Msongo Wa Mawazo

Anasema dalili za kawaida za kuwa na msongo wa mawazo ni mfadhaiko uitwao pyschotic depression, kupata usingizi kwa shida, kuona kuwa kila wakati umezidiwa na shughuli, kukosa kumbukumbu, kukosa uwezo wa kutuliza akili kwenye jambo moja

Dalili zingine ni mabadiliko katika tabia ya mtu ya kula, kuwa na wasiwasi, kusikia uchungu, hasira au kukata tamaa haraka, kuona kuwa huwezi kufanikisha mambo yako katika maisha.

Anasema matatizo yanayowapelekea watu kwa wingi kuwaona wataalamu wa tiba ya akili ni msongo wa mawazo, mfadhaiko na wasiwasi.

Dk. Mwinuka anafafanua kuwa wasiwasi ni hali ya kuwa na hofu kuwa kuna jambo kubwa na baya litatokea juu yako. Wasiwasi unaweza kuwa wa kawaida tu au ukalenga sehemu fulani, kikundi fulani cha watu au kitu fulani.

Tafadhali ndugu msomaji wetu, usisite kutoa maoni au kuuliza swali kuhusu hili somo letu la leo. Itakuwa furaha kubwa kwetu kukujibu.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post